Social Icons

Loading...

KWA NINI MWALIMU ANADHARAULIKA?

MIMI nionavyo Mwalimu ni sawa na kibao kielekezacho mtaa. Yaani unapokuwa katika makutano ya barabara unatafuita njia ya kwenda uendako na kando yako huna mtu wa kuuliza basi utakuta kuna kibao, hiki kitakusaidia sana kuelekea uendako.
Angalia hata wakati unapokuwa safarini na njia hiyo umeanza kuipita kwa mara ya kwanza, na upo mahari hujui umefika wapi, bahati mbaya unamuuliza jirani yake pembeni ya kiti anakujibu pia kuwa hajui hapo ni wapi, lakini unaona kibao kielekezacho mtaa, utakisoma na kutambua kuwa kumbo upo katika kijiji cha Nshamba.
Ukweli ni kuwa kibao kiuelezeao mtaa kina faida sana, lakini bahati mbaya sana faida yake ipo wakati ule kihitajikapo kuelekeza mtu. Ndiyo huu ndiyo ukweli, angalia, Ukijua kule uendako huhitaji kuelekezwa tena na kibao.sasa ingawa kitakuwepo faida ya kibao kile haionekani, hivyo kuficha umuhimu wake!
Hebu rudi nyuma, kule uliko soma shule ya msingi, pengine miaka 30 au fanya hata 45 iliyopita, ukiwa hujui kusoma na kuandika, mambo yalikuwaje na pima na sasa wakati ambapo unaandika na hata kusoma mamabo mbalimbali halafu fikiria kama ungekuwa hujui kusoma na kuandika, nini ungekuwa umepungukiwa? Je, katika fikra zako umebahatika kufikiri aliyekufanya ujue hayo? Basi hicho ni ‘kibao’ kilichokufanya uelewe.
Juzi nilirejea kijijini kwetu Busisi na kukuta mabadiliko makubwa sana kwanza nilikuta barabara ya lami ikiwa imejengwa na nyumba zile nilizokuwa nimezizoea zilikuwa zimebomolewa na kujengwa mpya, kwa hakika mji ulikuwa umebadilika sana. Sikujua nianzie wapi, lakini niliogopa kuuliza kwani, kama ningekosea na kuuliza kwa mtu ambaye nilicheza naye utotoni sijui ingekuwaje, nadhani ngenicheka na hata kunibeza kuwa nimesahau kwetu kutokana na kukulia mjini.
Nilijipa uhakika wa kutembea huku nikijaribu kuangaza angaza iwapo nitapata kumbukumbu ya eneo ambalo lingerejeleza kumbukumbu na taswira ya kule niendako. Kama hatua chache baada ya kutembea nilibahatika kuona kibao cha shule kilichokuwa kimeandikwa Shule ya Msingi Busisi.
Nilipata faraja, na kuanza kuvuta taswira ya enzi hizo nikiwa mwanafunzi. Nilisimama na kukiangalia, ukuta wake ulikuwa ni ule wenye maandishi. Tena bahati nzuri niliweza kuyakumbuka kuwa ni yale tuliyoandika miaka ile iliyopita. Nilisita, na kusimama kwa muda kukiangalia, lakini si kwa kukipatia heshima kibao licha ya kunipa kumbukumbu za uelekeo wa nyumbani kwetu, bali kukumbuka ya miaka iliyopita wakati nikisoma.
Sasa nilijua wapi niendako, sikuhitaji kuelekezwa na kibao cha kuelekeza ulekeo wa shule au jina la shule, cha nini kwangu tena? Lakini kimenisaidia kujua wapi nielekee.
Wakati nikielekea nilikutana na mzee mmoja sura yake haikuwa ngeni kwangu, nilimtizama kwa muda kasha nikataka kuendelea na safari lakini nilisita kwani kumbukumbu zilinijia, alikuwa ni Mwalimu wangu. Mbona yuko hivi, sikujua, lakini baada ya kumsogelea nilitambua kuwa alikuwa vile kutokana na hali ya maisha tu. Ila mfukoni alikuwa na chupa mbili za bia zikiwa na kimiminika, nadhani pombe aina ya Gongo.
Moyoni nilijiuliza, ndiye, ni mwalimu, tena aliyenifundisha a, e, i, o, u, lakini nilisha jua kusoma na kuandika simhitaji tena . Na wala sihitaji tena kujifunza kusoma na kuandika na mwalimu wa masomo hayo ana faida gani kwangu?
Nilianza kuondoka kuendelea na safari yangu huku mwalimu Yule nikimpuuza kama mlevi nisiyemjua, lakini looo..! alikuwa makini kumbe aliweza kunitambua, aliniita jina langu na kunieleza, "  fulani  umekua, najua umehitimu chuo kikuu, lakini mimi ndiye kibao chako kilichokuonyesha njia ya kufika huko, japo ungenisoma tu, kuliko kunipita hivyo" Nilisimama.
Nikakumbuka kibao cha awali jinsi kilivyonisaidia kujua uelekeo wa nyumbani kwetu, nikajiopna mpumbavu kwa kutomsaliamia hata mwalimu wangu ambaye alinitoa katika elimu ya UPE aliyenifundisha kwa bidii zake zote, na hatmaye kuhitimu elimu ya juu, leo nikiwa mkurugenzi wa kampuni ya D.
Mwalimu hubadilika umri, umbile, lakini habadiliki maana na umuhimu wake kwa mfano wa kibao kilekezacho mtaa. Mwalimu ni mwanafunzi wa kudumu, Mwalimu huendelea kujifunza na kufundisha kwa uvumilivu wote, raha yake siyo malipo ya mshahara wa shilingi bali ni kuona aliyemfundisha a, e, i, o, u akiwa katika mafanikio. Mwalimu halisi hufundisha kwa wito na mvuto na si kwa faida ipimwayo na uwingi wa fedha. Ndiyo maana aliyenifundisha miaka hiyo bado mpaka leo yupo, hajaacha kukimbilia kazi kama yangu.
Isipokuwa sisi tuliofundishwa na walimu walio sawa na vibao nilivyovielezea hapa ndiyo tubadilikao kutoka katika hali tete na ujinga hadi na kufikia kupata maarifa mengi ya hali ya juu na kukosa nidhamu hata kudiriki kusahau njia tuliyopitia, achilia mbali kumtengenezea mshahara mzuri mwalimu.
Walimu amesahaulika na sisi wote kabisa siyo serikali tu. Ndiyo sisi wote! Wanafunzi tukiwakumbuka na kuwaenzi walimu katika maisha yao ya kila siku watasahaulikaje?. Nani mwenye cheo kikubwa sana hapa Tanzania liyefika hapo alipo hakukunjwa akingali mbichi na walimu na kupewa ujanja wote alionao leo? Siyo anayeandaa mishahara wala anayehusika na kuwalipa mishahara. Masikini Mungu atuhurumie kwani sisi wanafunzi tumejaa dharau kubwa na kiburi hii ndiyo asili ya walimu kudharauliwa.
Watu wengi tunachukia kwenda tuliko soma, wale wa umriwangu na zaidi wanadai maeneo ya shule yanawakumbusha mboko walizo rambwaenzi zile hadi kutoa mchozi mbele ya ndito zao (washikaji) wapowaliozichukia jumla leo wanazililia kwa kukosa elimu. Wengine walikuwa nachuki biafasi na walimu wao.
Angalia wabunge wanavyokopeshwa magari, mwalimu mhmm! Angalia wanavyosotea mishahara wakati wabunge wao kule kumaliza tu kikao cha bunge miaka mitno kiinua mgogo anakilamba mapema bila bugudha, tena anatumbukiziwa beki haraka. Mwalimu je, yeye mshahara wake mpaka tarehe 49 masikini! Tumewasahau ukweli walimu, na hata kama tukikwakumbuka, tunawaita na kuwafanya mashahidi wa kusimamia kura zetu katika uchaguzi ili waone jinsi utakavyoingia Bungeni kulamba mkopo wa gari na kiinua mgogo cha milioni 46 baada ya miaka mitano.
Ni ukweli, tumewasahau walimu! Tumesahau walimu kwa sababu tulichotaka walisha tupatia siku nyingi, na sasa wamekuwa kama ganda la muwa la jana ambalo ulishalifyonza usukari wake wote na kulitupa sasa walikanyaga.
Ndipo baada ya fikra zote hizo nilipoweka mkono mfukoni mwangu na kutoa noti ya Tsh. 10,000 na kumpatia mwalimu wangu na kuendelea na safari yangu. Nilimwambia; Pole mwalimu, naye kunijibu ‘asante lakini siku  ya kesho, Sijui  itakuwaje!?’.
  Makala  hii  kwa  hisani  ya  http://gsengo.blogspot.com/2012/07/kwa-nini-mwalimu-anadharaulika.html

CCM Yajibu hoja za Mh Lisu kuhusu tuhuma za rushwa


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinalaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wana siasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;
"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".
Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.
Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.
"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.

"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.

Mgomo wa Walimu Mkoani Singida hali ilikuwa hivi ...

MGOMO Uliondaliwa na CWT nchini, umeleta madhara katika Manispaa Singida, baada ya wanafunzi wa shule za msingi kuandamana hadi ofisi ya RC jana.
Kwenye maandamano hayo, watoto wa shule ya msingi Nyerere, Singidani, Ipembe na Unyankindi, walitembea kilomita tatu hadi ofisi ya Mkuu Mkoa, huku barabarani wakiimba ‘tunataka haki zetu, walimu wamegoma, tunataka haki zetu’.
 Baada ya askari polisi kubaini usalama wa watoto hao upo hatarini, waliingilia kati na kuongoza maandamano hayo hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Wanafunzi hao zaidi ya 600 walijazana katika uwanja wa mbele, jengo la Mkuu wa Mkoa kuanzia saa tatu hadi saa 4:30 asubuhi.
 
Hatimaye Serikali ya Mkoa kupitia katibu wa tume idara ya Utumishi wa walimu Samweli Ole Saitabau, aliwataka kurudi nyumbani hadi kesho, wakaendelee na masomo katika shule zao.
Kwa  hisani  ya  Mjengwa Blog.

Baada Ya Walimu Kugoma; Wanafunzi Washushiana Nondo Darasani Huko Mbeya...!


Kambi ya upinzani yasema Mhe: ZITTO achunguzwe

KAMBI rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka kuchunguzwa kwa madai ya Naibu Kiongozi wa wa kambi hiyo, Zitto Kabwe, kuhongwa.

Kambi hiyo pia imetaja majina ya wabunge sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, mwishoni mwa wiki, ikidai kuwa kwa namna moja ama nyingine walihusika na vitendo vya rushwa.

Wabunge hao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta ili kuipigia debe menejimenti ya Shirika la Ugavi wa umeme nchini (TANESCO).

Soma zaidi:http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=38749

GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA KWA MUDA USIOJULIKANA.


TAMKO LA SERIKALI
GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA
 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini. Katika matoleo yake hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
 Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.  Mhariri, mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
     Uamuzi wa Serikali
   Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai, 2012. Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
 Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia  taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na wajibu. 
 Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
 
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012.

Kibonzo


Maoni ya Mh: Mnyika kufuatia maamuzi ya kuvunja kamati ya kudumu ya Bunge ya nishati na madini

Kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:
Kwa maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.
Ukiondoa tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
Hivyo hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani. Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma.
Hata baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.

Nilisema bungeni kwamba “Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara”.
Mathalani, Waziri wa Nishati na Madini ameeleza bungeni tarehe 28 Julai 2012 kuwa wapo wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye kulihujumu Shirika la Umeme (TANESCO) na Spika wa Bunge akahitimisha kuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itachunguza tuhuma husika na pia kwamba inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za Maadili (Code of Conduct) ili kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo, Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka 2008 baada ya Kashfa ya Richmond iliazimiwa katika Azimio Na. 11, kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995 (The Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje ya Bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”
Bunge lilitaarifiwa Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba kikundi kazi (Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura 398) ambao ulikuwa katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa serikali ilitarajia kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama ilivyoshauriwa na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu azimio hilo halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.
Aidha, kumetolewa madai ya baadhi ya wabunge kupokea ama kudai rushwa suala ambalo nalo Spika wa Bunge ametoa uamuzi kuwa litashughulikiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Lakini Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si mara ya kwanza kwa tuhuma za namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa kamati mbalimbali za bunge.
Hata hivyo, kwa sababu ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa ukamilifu tuhuma kama hizo zitaendelea kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa kamati ya bunge ya nishati na madini. Izingatiwe kwamba madai ya rushwa kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza kuhusu Kamati ya Nishati na Madini na binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena kwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni mwaka 2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi wabunge kwa rushwa hata hivyo hatua hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa au kuwachukulia hatua wahusika.

Suala hili likatajwa tena na Mbunge wa Kigoma Kaskazini David Kafulila kuhusu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na likatajwa tena na Kiongozi wa Upinzani Freeman Mbowe na Mbunge wa Kyela Dr Harrison Mwakyembe kuhusu uchaguzi wa Afrika Mashariki lakini hatua hazikuchukuliwa kuchunguza wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 (Maarufu kama Sakata la Jairo), yangetekelezwa na wahusika wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu pia kwa watendaji wa wizara na mashirika ya umma kuhusu rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma yenye kulenga kuwaathiri wabunge kwa rushwa na maslahi mengine ya kifedha.
Katika hali inayoonyeha kwamba Serikali bado haioni uharaka na ulazima wa kuchukua hatua, wakati bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012 kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa bungeni toka yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011; lakini Waziri akajibu tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini, bila kujali kwamba nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali maazimio ya bunge baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji wahusika na kupata pia vielelezo.
Kwa hiyo, ni muhimu Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea kwenye Hotuba niliyowasilisha bungeni na kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge juu ya masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa wabunge kuhusu suala la ununuzi wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO nilieleza pia masuala mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu mabilioni ya shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta na gesi asili pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa kuchukuliwa.
Nimetoa maoni hayaleo jumapili tarehe 29 Julai 2012:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Chanzo  kwa  hisani  ya  Mjengwa Blog.

Liwalo na liwe , Walimu watangaza kuanza mgomo.

Viongozi wa  Chama  cha  walimu wakitangaza  msimamo  wao  kuhusu  mgomo  wa  walimu  nchi nzima.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetangaza kuanza kwa mgomo wa walimu kwa nchi nzima kuanzia July 30, mwaka huu baada ya asilimia 95.7 ya walimu kupiga kura za ndiyo kuridhia kuwepo kwa mgomo huo wa kutetea maslahi yao.Rais wa CWT Gratian Mkoba amesema kwa mujibu wa sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, kifungu cha 80 Moja (d) hatua zote zimefuatwa katika kuandaa mgomo huo na kuwataka walimu wote washiriki kwa kukaa nyumbani mpaka hapo watakapopewa maelekezo mengine.Akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam, MUKOBA amesema mgomo huo ni halali na hauna uhusiano wowote na zoezi la Sensa ya watu na Makazi linalotarajia kufanyika usiku wa kuamkia tarehe 26, Agosti mwaka huu.
Kuhusiana na shauri la walimu kuwepo mahakamani Mukoba amesema kitendo hicho hakiondoi utaratibu wa kuendelea na taratibu za mgomo kutokana na kutokuwepo kwa amri yoyote ya mahakama kusitisha mgomo huo.

Wafanyakazi Wakatae Hadaa Za Mifuko Ya Jamii


HATUSHANGAI hata kidogo kuona moto unaendelea kuwaka nchi nzima kutokana na wafanyakazi kupinga Mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012,  ambayo inazuia wanachama wa mifuko hiyo kulipwa mafao yao kabla ya kufikia umri wa miaka 55 na 60.Hatushangai pia kuona mabadiliko ya sheria hiyo yanazua mtafaruku mkubwa kiasi cha maelfu ya wafanyakazi nchini kuapa kuwa liwalo na liwe, wataendelea kupinga mabadiliko hayo hata ikibidi waache au wafukuzwe kazi.
Kitu kinachotushangaza, ambacho hakika hakikutegemewa na wengi ni hatua ya wabunge kutaka sheria hiyo walioipitisha wenyewe Aprili mwaka huu irudishwe bungeni ili kipengele kinachowazuia wafanyakazi kuchukua mafao yao kabla hawajafikisha umri huo kiondolewe.
Wabunge walifadhaika bungeni juzi, wakati mmoja wao alipowaumbua kwa kusema ni aibu kwamba Bunge lililopitisha sheria hiyo ndilo linalogeuka na kuikana na kuwa, huo ni uthibitisho kwamba wabunge wote siyo makini.Kitendawili kinachopaswa kuteguliwa ni jinsi gani wabunge walipitisha sheria hiyo bila kuona udhaifu wanaozungumzia sasa, licha ya Bunge hilo kuwa na wabunge wengi wenye taaluma na weledi katika tasnia ya sheria.
Ndiyo maana tunashawishika kukubaliana na wakosoaji wanaosema kwamba wabunge walipitisha sheria hiyo pasipo kuisoma kwa kuwa sheria hiyo haina masilahi kwao, kwani wao wanalipwa kiinua mgongo na Serikali kila baada ya miaka mitano, badala ya pensheni zinazolipwa kwa wafanyakazi na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii.    Tunaambiwa sasa kwamba zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini tayari wameacha kazi na wengine 4,000 wakiwa wamewasilisha barua za kufanya hivyo kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo.Kama kelele zinazopigwa kila kona nchini ni kielelezo cha hasira walizonazo wafanyakazi katika sekta mbalimbali nchini kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo, basi tutegemee hali ya sintofahamu ya mivutano na migomo inayoweza kuathiri uchumi na amani yetu kwa kiasi kikubwa.
Sisi hatuoni namna Serikali na viongozi wa mifuko hiyo wanavyoweza kujikwamua kutoka katika mgogoro huo au kuzima hasira na vuguvugu za wafanyakazi wanaopinga sheria hiyo pasipo kuirudisha sheria hiyo bungeni na kufuta kipengele hicho kandamizi na chenye utata mkubwa.Pia tunapata shida kuelewa kwa nini mabadiliko hayo yanakuja wakati huu, ambapo mifuko hiyo imetumia matrilioni ya fedha za wafanyakazi katika miradi mingi mikubwa, ukiwamo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini imeshindwa kupata marejesho ya fedha hizo.
Tunaishauri Serikali na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), zibadilishe sheria ya mifuko hiyo ya jamii ili iwanufaishe wafanyakazi.
Tunadhani pia wakati umefika sasa kwa wafanyakazi kuhakikisha wanafaidika zaidi na mifuko hiyo, ikiwamo kulipwa riba ya fedha wanazowekeza katika mifuko hiyo miaka nenda miaka rudi.
chanzo : Mwananchi

Ngorongoro Heroes yanyukwa 2 - 1 na Nigeria.

TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imeanza vibaya kampeni za kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo, zitakazofanyika nchini Algeria mwakani, baada ya kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wasaniii tunakula miziki emama tunakula miziki kasimbaghooo

Yanga Yatetea Ubingwa wake wa Kombe la Kagame


Mgeni  rasmi Mh:  Said Mecky Sadick Mkuu  wa  mkoa  wa  Dar  es Salaam  akikabidhi kombe   kwa  nahodha  wa Yanga Nadir Haroub Canavaro
MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imefikia tamati jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa klabu ya Yanga, kufanikiwa kutetea taji lao, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0.
 Shukrani kwao Hamisi Kiiza Diego na Said Bahanuzi, wafungaji wa mabao hayo moja kila kipindi na sasa Yanga inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, inaingia kwenye orodha ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, kwa kutwaa taji hilo mara tano.
Yanga sasa imebakiza mara moja kufikisha idadi sawa na wapinzani wao wa jadi, Simba (1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002) kutwaa Kombe hilo, mara tano kwa sita. Yanga ilibeba taji hilo 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012.
Kiiza alifunga bao lake, baada ya kuuwahi mpira aliokuwa anarudishiwa kipa Deo Munishi ‘Dida’ na beki Said Mourad na kumpiga chenga kipa huyo kisha kuusukuma mpira nyavuni.
Bahanuzi aliuwahi mpira mrefu uliopigwa na beki Oscar Joshua na kuwazidi ujanja mabeki wa Azam kabla ya kumtungua Dida.
 Mechi hiyo ilichezeshwa vema na refa Thierry Nkurunzinza kutoka Burundi, aliyekuwa akisaidiwa na Simba Honore wa Rwanda na Peter Sabatia wa Kenya.
Katika mchezo huo kikosi kilichoweka historia ya Kombe la tano la Kagame, Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo/Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzoma, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende.
Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Tcheche/Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco ‘Adebayor’, Ibrahim Mwaipopo na Ramadhan Chombo ‘Redondo’. Benchi; Mwadini Ally, Samir Haji Nuhu, Joseph Owino, George Odhiambo, Mrisho Ngassa, Khamis Mcha ‘Vialli’ na Gaudence Mwaikimba.
Katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, AS ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Magola Mapanda dakika ya 18 na Mutombo Kazadi dakika ya 67, wakati la kufutia machozi la timu ya jeshi la Rwanda, lilifungwa na Jean Mugiraneza dakika ya 89.  

Jogoo mwenye hirizi, shanga azua kizaazaa

WAKAZI wa Mtaa wa Nyanchenche Road mjini Sengerema juzi walifurika kushuhudia tukio la  kuonekana jogoo asiye na manyoya akitembea huku akiwa amefungwa shanga na hirizi mbili shingoni na mabawa yake yakiwa yamechanjwa chale na kupakwa dawa nyeusi.Tukio hilo lililovuta umati wa watu lilitokea juzi  saa 7:00 mchana kwenye moja ya familia ya mtaa huo[jina limehifadhiwa]ambaye alidai kwamba kuku huyo alijitokeza nyumbani kwake bila kufahamu alikotokea.
Kuku huyo wa ajabu alikutwa na wananchi katika mji huo ulioko  kando kando ya barabara,jambo lililowashtua wakazi wa Sengerema waliofika kulishuhudia huku wakilihusisha na imani za kishirikina.Katika tukio hilo hakuna  mwananchi aliyejitokeza kumshika kuku huyo,  huku wenyeji wa mji husika wakiendelea na shughuli zao licha ya kuonyesha mshituko.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mwenyekiti  wa kitongoji hicho Leah James alieleza kushangazwa na tukio hilo aliloliita la ajabu, na kwamba halijawahi kutokea  katika kitongoji hicho kwani limeibua hisia tofauti miongoni mwa wanajamii.
Nimepata taarifa za tukio hili ilikuwa mchana muda wa saa saba na tumefika mpaka eneo la tukio, kwa kweli inashangaza na kusikitisha, huyo kuku wa ajabu hana nyoya hata moja wala alama ya kidonda na amechanjwa chale kwenye mbawa zake,kavishwa hirizi mbili shingoni na amefungwa shanga kwenye mbawa zakeîalisema mwenyekiti.

Baada ya tukio hilo uongozi wa eneo hilo na sungusungu uliamua kuitisha mkutano siku iliyofuata leo(jana) ambapo walifuatilia na kumbaini mmiliki wa kuku huyo kuwa ni  Leticia Makoye ambaye alidai kuku huyo ni wake na  humtumia katika shughuli za uganga wa kienyeji .
Kikao hicho kiliamua kumrudishia kuku huyo ingawa alikuwa tayari amekufa kutokana na kupigwa baridi usiku kucha,maamuzi yaliyopingwa na wananchi na hivyo kulazimika kumshambulia kwa mawe hadi nyumbani kwake huku viongozi wa mtaa huo wakimpatia ulinzi hadi alipoingia ndani ya nyumba.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Gazeti hili eneo la tukio wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi yao wakilihusisha na imani za kishirikina kutokana na vitu alivyokutwa navyo kuku huyo ikiwa ni pamoja na shanga,hirizi,na chale alizochanjwa kwenye mbawa zake.Grece Michael (32), Fadhili Alfani (45), na Daniel Marco walisema  matukio ya ajabu kama hilo ni dalili za mwisho wa dunia kutokana na vitendo vya kishirikina kuongezeka na kwamba njia pekee ya kuepukana navyo ni kudumu katika sala na imani.

Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Jogoo mwenye hirizi, shanga azua kizaazaa

WAKAZI wa Mtaa wa Nyanchenche Road mjini Sengerema juzi walifurika kushuhudia tukio la  kuonekana jogoo asiye na manyoya akitembea huku akiwa amefungwa shanga na hirizi mbili shingoni na mabawa yake yakiwa yamechanjwa chale na kupakwa dawa nyeusi.Tukio hilo lililovuta umati wa watu lilitokea juzi  saa 7:00 mchana kwenye moja ya familia ya mtaa huo[jina limehifadhiwa]ambaye alidai kwamba kuku huyo alijitokeza nyumbani kwake bila kufahamu alikotokea.
Kuku huyo wa ajabu alikutwa na wananchi katika mji huo ulioko  kando kando ya barabara,jambo lililowashtua wakazi wa Sengerema waliofika kulishuhudia huku wakilihusisha na imani za kishirikina.Katika tukio hilo hakuna  mwananchi aliyejitokeza kumshika kuku huyo,  huku wenyeji wa mji husika wakiendelea na shughuli zao licha ya kuonyesha mshituko.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mwenyekiti  wa kitongoji hicho Leah James alieleza kushangazwa na tukio hilo aliloliita la ajabu, na kwamba halijawahi kutokea  katika kitongoji hicho kwani limeibua hisia tofauti miongoni mwa wanajamii.
Nimepata taarifa za tukio hili ilikuwa mchana muda wa saa saba na tumefika mpaka eneo la tukio, kwa kweli inashangaza na kusikitisha, huyo kuku wa ajabu hana nyoya hata moja wala alama ya kidonda na amechanjwa chale kwenye mbawa zake,kavishwa hirizi mbili shingoni na amefungwa shanga kwenye mbawa zakeîalisema mwenyekiti.

Baada ya tukio hilo uongozi wa eneo hilo na sungusungu uliamua kuitisha mkutano siku iliyofuata leo(jana) ambapo walifuatilia na kumbaini mmiliki wa kuku huyo kuwa ni  Leticia Makoye ambaye alidai kuku huyo ni wake na  humtumia katika shughuli za uganga wa kienyeji .
Kikao hicho kiliamua kumrudishia kuku huyo ingawa alikuwa tayari amekufa kutokana na kupigwa baridi usiku kucha,maamuzi yaliyopingwa na wananchi na hivyo kulazimika kumshambulia kwa mawe hadi nyumbani kwake huku viongozi wa mtaa huo wakimpatia ulinzi hadi alipoingia ndani ya nyumba.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Gazeti hili eneo la tukio wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi yao wakilihusisha na imani za kishirikina kutokana na vitu alivyokutwa navyo kuku huyo ikiwa ni pamoja na shanga,hirizi,na chale alizochanjwa kwenye mbawa zake.Grece Michael (32), Fadhili Alfani (45), na Daniel Marco walisema  matukio ya ajabu kama hilo ni dalili za mwisho wa dunia kutokana na vitendo vya kishirikina kuongezeka na kwamba njia pekee ya kuepukana navyo ni kudumu katika sala na imani.

Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Kuunganishiwa Umeme Sasa Kuanzia Sh180,000



Waziri  wa Nishati na  Madini Prof Sospeter Muhongo
SERIKALI imetangaza kushusha gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa viwango ambavyo ni kati ya asilimia 60 na 77 kwa wakazi wa vijijini na kati ya asilimia 29 na 65 kwa wananchi waishio sehemu za mijini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma jana, waziri huyo alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio mijini.
 Profesa Muhongo alisema pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo.
 Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni zilizokuwa zikilipwa awali.“Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”

Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.
Machi 18 mwaka jana, Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.
Chanzo. http://www.mwananchi.co.tz

Sherehe ya Kumpongeza Mchungaji Kiongozi wa TAG Revival Kinondoni Yafana

Mchungaji Kiongozi Askofu Zakayo Rogathe Swai wa Kanisa  la   Tanzania Assemblies of God (TAG) Kinondoni maarufu  kama Kinondoni Revival Church   afanyiwa sherehe  kwa kuhitimu  mafunzo ya Shahada ya kwanza ya Theologia  toka Chuo  kikuu cha East  Nairobi  sherehe  zilizofanyika leo  kanisani Kinondoni Dar  es  Salaam.

Mchungaji  Swai akiwa na  mkewe Eshemendi, wengine kutoka kushoto ni Askofu mkuu wa makanisa  ya TAG  Tanzania  Dr Barnabas Mtokambali  na  mkewe  , Kulia kabisa ni   Mr & Mrs  Rev Dr.   Moris Mwarandu toka   kanisa la  RGC  Nairobi, Kenya  

                                           Askofu  Swai  na  mkewe  wakilishana  keki .



Taarifa ya Serikali kuhusu Mgomo wa Walimu

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU KUGOMA
____________________________________________
SERIKALI kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Ijumaa, Julai 27, 2012 majira ya saa tisa alasiri, imepokea notisi ya saa arobaini na nane (48) ya kusudio la walimu wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma kuanzia Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 saa moja na nusu asubuhi.
Kabla ya notisi hii kutolewa, Serikali imekuwa ikifanya jitihada nyingi za kujadiliana na viongozi wa CWT kuhusu jinsi ya kuboresha maslahi ya walimu kwa nia ya kumaliza suala hili kwa maelewano kwa kutumia vyombo na ngazi mbali mbali za kisheria.
Kwa sasa, shauri hili liko Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii siku ya Ijumaa tarehe 27 Julai, 2012 majira ya saa sita mchana pande zote mbili zilifika Mahakamani, na Mahakama ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne tarehe 31 Julai, 2012 saa sita mchana, ili kuiwezesha Mahakama kuendelea kusikiliza shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi.
Kwa hiyo, Mgomo huu siyo halali kwa sababu shauri hili bado liko Mahakamani.
Kwa msingi huo hatua ya CWT kutoa notisi ya kuanza kwa mgomo kabla ya kukamilika kwa shauri hili ni kukiuka taratibu halali za Kimahakama ambazo kila mmoja anawajibika kuziheshimu.
Serikali inapenda kuwafahamisha walimu wote kuwa kujihusisha na mgomo huu ni kwenda kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi. Hivyo, walimu wanapaswa kupima madhara ya mgomo huu usiokuwa halali na Serikali inawataka walimu kupuuza mgomo huo na kutokujihusisha nao. Walimu wote wanatakiwa waendelee na kazi kama kawaida.

Peniel M. Lyimo
KAIMU KATIBU MKUU KIONGOZI
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Julai, 2012

Fahamu Sakata la Shigongo na Jose Chamelion

Ndg: Erick  Shigongo



MKURUGENZI wa Global Publishers, Erick Shigongo amewataka Wasanii kuacha
tofauti zao katika kutetea maslahi ya nchi na si vinginevyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana, na Mkurugenzi huyo alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kuzulumiwa dola 3500 na msanii wa Uganda Jose Chameleone.
Alisema ameshangazwa na baadhi ya Watanzania kumchafua kwenye mitandao kwa kitendo chake cha kumdai msanii huyo wa Uganda, fedha walizokubaliana katika mkataba ili kufanya onyesho la Tamasha la Usiku wa Matumaini.
Shigongo alisema huu ni wakati kwa watanzania kufahamu ukweli kuhusu hilo kutokana na ukweli kwamba msanii huyo, amekiuka makubaliano ya mkataba wa kwanza ambao walikubaliana kufanya onyesho hilo ghafla akageuka kudai fedha zaidi.Alisema hata hivyo, Mkurugenzi huyo alikubali kuingia mkataba mwingine kwa mara ya pili kutokana na ukweli kwamba alikwishafanya matangazo kuwa msanii huyo angekua mmoja wa wasanii ambao wangefanya onyesho katika tamasha hilo.“Kweli tulikubaliana mkataba mwingine nikamlipa dola 8000 na kweli alikuja akafanya onyesho lakini baada ya hapo ndipo nilipomdai fedha zangu dola 3500 alizochukua katika makubaliano ya awali”alisema Shigongo.
Shigongo alisema si kweli kwamba alizuia pasipoti ya msanii huyo wakati alipokuwa amepangisha chumba kwenye hoteli yake bali kilichotokea ni msanii huyo kuondoka mwenyewe baada ya kudaiwa fedha hizo.
Katika hatua nyingine, Shigongo alisikitishwa na kitendo cha msanii huyo akishirikiana na vijana wenzake kuvamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda kwa madai ya kudai kurudishiwa pasipoti yake.
Chanzo: Global publisher

Ujasiria mali ndani ya National Stadium

Jana  wakati  wa  michezo  ya   nusu   fainali  ya michuano ya  kombe  la  Kagame  inayoendelea jijini  Dar es Salaam,  Kijana  mmoja   Mpiga  picha (Jina  Kapuni )  akiwa  na  kombe   mfano  wa  la  Kagame   akipiga  washabiki  picha   kabla  ya  mchezo  wa  pili  kati  ya  Yanga  Vs   APR   ya  Rwanda








































Nani hinoo  aka  Blogger   , pembeni  ni  Mnazi na  mdau wa Dar Young African Mh: Michael Yona KIBINDU  ,akicheki  na kusifu    ubunifu  wa  kijana  huyo  uwanjani , SAFI   SANA  KIJANA .....

Mtafaruku Zaidi Sheria Mifuko Ya Hifadhi Ya Jamii

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
MABADIKO ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012, iliyopitishwa Aprili mwaka huu, imeendelea kuzua mtafaruku sehemu mbalimbali nchini, huku wabunge wakishinikiza kuwa, sheria hiyo inapaswa kurejeshwa bungeni ili ijadiliwe upya.
Jana, wabunge waliunga na wafanyakazi kupinga kipengele cha sheria hiyo kinachomtaka mfanyakazi kupata mafao yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, au miaka 60 kwa mujibu wa sheria.Hoja ya kutaka suala hilo lijadiliwe upya ilitolewa na Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.
Hoja ya Jafo ilitokana na kuwapo kwa taarifa kuwa, zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini wameacha kazi huku wengine zaidi ya 4,000 wakiwa tayari wamewasilisha barua za kuacha kazi kutokana na sheria hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitofautiana na wenzake pale aliposema kuwa sheria inayolalamikiwa ilishapitishwa na Bunge, hivyo angependa kujua uhalali wa kujadiliwa tena bungeni.
Jijini Dar es Salaam, mjadala mzito uliendelea huku baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wakisema: “Marekebisho hayo ni kandimizi na yanalenga kuwanyima haki wanachama ambao wanaweza kupata matatizo mbalimbali wakiwa kazini”.Kwa upande wake Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), jana ilitoa taarifa iliyoweka bayana kuwa, fao la kujitoa kazini limefutwa na kwamba jambo lolote linalohusu mafao ya aina hiyo linapaswa kusubiri kutolewa kwa miongozo husika.

Bungeni Dodoma
Jafo alitoa hoja akitaka Bunge liahirishe mjadala wa hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara jana ili kujadili kwa dharura sheria hiyo aliyosema kuwa imeanza kuzua mtafaruku na sintofahamu miongoni mwa jamii."Mheshimiwa Mwenyekiti, Wafanyakazi wa sekta mbalimbali wamepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga kuwanyima haki ya fedha zao wanazokatwa kwa mujibu wa sheria. Naomba mwongozo wako, Bunge tujadili suala hilo kwa dharura," alisema.Jafo alitoa hoja hiyo akitumia Kanuni ya 47 (1)(2) na (3) ambayo huruhusu jambo la dharura kujadiliwa.
Hoja ya Jafo iliungwa mkono na Mhagama ambaye alisema kuwa hilo ni jambo kujadiliwa lakini kwa wakati huo lilikuwa limekosa kitu kimoja ambacho ni mdai halisi ya wafanyakazi ambayo yanalalamikiwa.
“Hoja yako imeungwa mkono na ni kitu muhimu kujadiliwa, lakini imekosa kitu kimoja. Naomba unisaidie, ni mambo gani hasa ambayo wafanyakazi wanayohitaji yajadiliwe,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Tunatakiwa tuwasaidie wafanyakazi nchini, kwani hali imekuwa tete kwa wafanyakazi kuhusu suala hili na ili tuwatete ipasavyo ni vizuri tukajua madai halisi kuhusu jambo hilo.”
Alipomaliza kutoa mwongozo huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisimama na kukieleza kiti cha Spika kuwa jambo hilo ambalo Jafo amelizungumzia ni zito na hadi sasa kauli ya Serikali haijatoka hadi hivi sasa.“Kwa busara yako mwenyekiti, naomba uitishe kamati ya uongozi ili tuweze kujadili jambo hili,” alisema Zitto.
Lissu kwa upande wake alisema kuwa, jambo aliloeleza Jafo ndicho kiini cha kelele zilizopo mtaani hivi sasa, hivyo anaiunga mkono.
Baada ya Lissu kumaliza, alisimama Mhagama na kueleza kuwa tayari alishatoa mwongozo kuhusu jambo hilo kwamba, ni muhimu Jafo akafanya mawasiliano na wafanyakazi ili kujua wanachohitaji kifanyike.
“Nilichokisema hapa nampa muda Jafo afanye ‘consultation’ na wafanyakazi hao ili atengeneze hizo hoja zake vizuri na kulileta suala hilo bungeni,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Ifikapo 7:15 mchana (jana) Kamati ya Uongozi itakaa ila Jafo awasiliane na wafanyakazi ili tuweze kujua matatizo yao...”Lakini Lugora alitoa mawazo tofauti akisema: “Wanalalamikia kitu ambacho ni sheria iliyopitishwa hapa bungeni. Nataka kujua uhalali wa kujadiliwa suala ambalo tulilipitisha hapa bungeni”.
Mhagama alisimama na kumweleza Lugola kuwa Bunge linatakiwa kujadili maslahi ya wananchi na kwamba, sheria zilizopitishwa na Bunge siyo msahafu ambao hauwezi kubadilishwa.Baadaye jioni, Mhagama alisema Jafo ameelekezwa kwamba akaandae hoja yake kisha aiwasilishe kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda ili iwasilishwe bungeni kwa taratibu za kawaida.

Wanasheria
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Kaki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema wanapinga marekebisho ya Sheria hiyo kwa kuwa yanawanyima haki wanachama wa mifuko hiyo kupata stahili zao wanapozihitaji.“Mimi kama mwanasheria naona kuwa, marekebisho haya yanalenga kuwakandamiza wanachama wa mifuko hiyo, kwani kila mtu ana mahitaji yake na majukumu yake sasa sio vema kumpangia mtu lini anapaswa kuchukua stahili yake,” alisema Sungusia na kuongeza:
“Tunafahamu kuwa, Serikali inadaiwa fedha nyingi na mifuko hii kutokanana mikopo mbalimbali; kwa mfano ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Machinga Complex pamoja na jengo la Bunge. Sasa wameamua kufanya marekebisho haya ili kufidia fedha zilizotumika na kusababisha ukandamizaji kwa wanachama.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Sengondo Mvungi alisema marekebisho ya sheria hiyo ni kandamizi wa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wanachama wanapaswa kuamka kupinga sharia hiyo.Alisema wananchi wanachama wanapaswa kupinga sharia hiyo kwani haijawashirikisha na ina lengo la kuwakandamiza.
Dk, Mvungi alifafanua kuwa, sharia hiyo imepitwa na wakati kwani wafanyakazi hawakushirikishwa na kwamba sharia hizo zilitungwa wakati wa chama kimoja.
Kauli ya SSRA
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji Dar es Salaam jana imesema kuwa, maombi yote ya kujitoa katika mifuko ya hifadhi yamesimamishwa hadi baada ya miezi sita.Taarifa hiyo ilisema usitishaji huo wa kujitoa hautayahusu maombi ya wale ambao wamejitoa kabla ya Julai 20 mwaka huu 2012 na uamuzi huo imebainisha taarifa hiyo kuwa imefuatia mkanganyiko uliojitokeza hivi karibuni na kuleta mgongano baina ya wadau.
 Taarifa hiyo imekanusha madai kuwa sitisho la fao la kujitoa linatokana na shinikizo la Serikali, au madai mengine kuwa, mifuko imefilisika.“Mamlaka inawaomba wanachama na wadau wote kuwa na utulivyu wakati wa mchakato ukiendelea kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya wanachama” sehemu ya taarifa hiyo imesema.Taarifa hiyo imebainisha na kufafanua kuwa marekebisho hayo ambayo yamezua migongano na wadau yamepitia hatua zote za kisheria na ushirikishwaji wa wadau muhimu katika sekta hiyo, ambao ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, chama cha waajiri pamoja na serikali.
“Mchakato umefanyika kwa kuzingatia tofauti ya ajira, mazingira ya kazi na hivi sasa mamlaka inaendelea kuandaa miongozo na kanuni za mafao kwa lengo la kuboresha maslahi ya wanachama na majadiliano yatahuisha wadau wote muhimu” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Chanzo: Mwananchi 
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top