Kufuatia
uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali
kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa
maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini na mbunge:
Kwa
maoni yangu uamuzi huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi
kurejesha heshima ya bunge kwa ukamilifu wala hautaweza kushughulikia
uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na kwenye serikali ikiwa
hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande mwingine,
uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu
uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.
Ukiondoa
tuhuma za wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya
kifedha kwenye wizara, taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye
kamati mbalimbali, heshima ya bunge imeathiriwa vile vile na maamuzi
mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa wa ufisadi wa Rada Mbunge
Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
Hivyo
hatua zaidi zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye
wajumbe waliotuhumiwa na pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe
wa kamati mbalimbali za kudumu za bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha
ama tuhuma za rushwa miongoni mwa wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili
majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge lijadili kupitisha
maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi
na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani.
Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge
wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa
maslahi ya umma.
Hata
baada ya hatua hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye
uzembe ikiwa litatimiza kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali
kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa udhaifu wa serikali kwenye sekta ya
nishati na sekta nyingine muhimu za taifa kwa kuhakikisha maazimio yote
ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka kama nilivyoeleza
kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe 15 Julai 2011 na
tarehe 27 Julai 2012.
Nilisema
bungeni kwamba “Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya
TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC yangetekelezwa
yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji
wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa
haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na
Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka
2011 yangechukuliwa kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia
mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara”.
Mathalani,
Waziri wa Nishati na Madini ameeleza bungeni tarehe 28 Julai 2012 kuwa
wapo wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye kulihujumu Shirika la
Umeme (TANESCO) na Spika wa Bunge akahitimisha kuwa Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge itachunguza tuhuma husika na pia kwamba
inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za Maadili (Code of Conduct) ili
kudhibiti hali hiyo.
Hata
hivyo, Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka
2008 baada ya Kashfa ya Richmond iliazimiwa katika Azimio Na. 11, kwamba
“Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995 (The Public
Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho makubwa ili
kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi Waandamizi
wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa
madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze
rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje
ya Bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”
Bunge
lilitaarifiwa Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba
kikundi kazi (Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye
mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura
398) ambao ulikuwa katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu
Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa serikali ilitarajia
kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la
tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama ilivyoshauriwa
na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu azimio hilo
halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.
Aidha,
kumetolewa madai ya baadhi ya wabunge kupokea ama kudai rushwa suala
ambalo nalo Spika wa Bunge ametoa uamuzi kuwa litashughulikiwa na Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Lakini Serikali na Uongozi wa
Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si mara ya kwanza kwa tuhuma za
namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa kamati mbalimbali za
bunge.
Hata
hivyo, kwa sababu ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa ukamilifu
tuhuma kama hizo zitaendelea kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa kamati
ya bunge ya nishati na madini. Izingatiwe kwamba madai ya rushwa
kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza kuhusu Kamati ya Nishati na
Madini na binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena kwa Kamati Teule
ya Bunge iliyochunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na
Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni mwaka
2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi wabunge kwa rushwa hata hivyo
hatua hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa au kuwachukulia
hatua wahusika.
Suala
hili likatajwa tena na Mbunge wa Kigoma Kaskazini David Kafulila kuhusu
Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na likatajwa tena na Kiongozi wa
Upinzani Freeman Mbowe na Mbunge wa Kyela Dr Harrison Mwakyembe kuhusu
uchaguzi wa Afrika Mashariki lakini hatua hazikuchukuliwa kuchunguza
wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo maazimio kuhusu uhalali wa
utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya
kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 (Maarufu kama Sakata la Jairo),
yangetekelezwa na wahusika wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu pia
kwa watendaji wa wizara na mashirika ya umma kuhusu rushwa na matumizi
mabaya ya fedha za umma yenye kulenga kuwaathiri wabunge kwa rushwa na
maslahi mengine ya kifedha.
Katika
hali inayoonyeha kwamba Serikali bado haioni uharaka na ulazima wa
kuchukua hatua, wakati bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012
kupitisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi
kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa maazimio
hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya utekelezaji iliyowasilishwa
bungeni toka yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011; lakini Waziri akajibu
tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini, bila kujali kwamba
nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali maazimio ya bunge
baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji wahusika na
kupata pia vielelezo.
Kwa
hiyo, ni muhimu Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea kwenye Hotuba
niliyowasilisha bungeni na kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais, Waziri
Mkuu na Spika wa Bunge juu ya masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na
kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa wabunge kuhusu suala la ununuzi
wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO nilieleza pia masuala
mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu mabilioni ya
shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta na gesi asili
pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa kuchukuliwa.
Nimetoa maoni hayaleo jumapili tarehe 29 Julai 2012:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Chanzo kwa hisani ya Mjengwa Blog.
Post a Comment