Social Icons

Loading...

Kwa nini wanafunzi 'High School' waruhusiwe kuwa na simu ?

KUNA mambo mengi tuliyorithi kutoka kwa wakoloni, ambayo katika miaka hii, nina wasiwasi kama yanafaa na kutusaidia au yanatuharibia. Mojawapo ni lile la utunzaji au malezi na makuzi ya watoto na vijana wetu.

Ninaamini kwamba sisi kama Watanzania, ukifananisha na nchi nyingi ulimwenguni tumekuwa tukiwalemeza vijana wetu kwa kushindwa au kukataa kuwapa nafasi ya kujaribu, kuthubutu na kukuza utundu, ambao hatimaye humsaidia mtu katika maisha yake ya baadaye.

Siasa za ujamaa na taratibu za zamani zilizomwaminisha kijana kuwa kazi yake ni kukaa tu shule, kusoma, kulala na kutofanya au kutokujaribu kazi yoyote ya akili au ya mikono nje ya mitaala ya elimu au shule zimechangia zaidi katika hili.Mtoto wa Kitanzania anayeingia kidato cha tano, kila mwaka siyo mtoto tena. Ni mtu mzima. Kwa kawaida anatakiwa kuwa na umri wa miaka 17 au 18. Hawa ni wachache, walio wengi ni kwenye miaka 19, 20 na kuendelea.
Tusipotumia saikolojia na sosholojia ipasavyo, tutajikuta tukiingia kwenye migogoro isiyoisha kila mwaka na vijana wetu hawa.Itakuwa hivyo kwa sababu, kisaikolojia watoto hao siyo watoto tena, bali watu wazima. Na wengine wana uwezo na akili kutupita wazazi na walimu wao. Kwa kujikinza pia, bado watu wazima hawa hawajawa watu wazima kamili. Kama hatua ya mwanzo, awali ya yote ningelipendekeza kwamba somo la sosho-saikolojia liwe somo la lazima shuleni. Somo hilo litasaidia mambo kadhaa.

Kwanza, litawasaidia vijana kujitambua; pili litawasaidia walimu kujitambua; tatu, litawafanya wajitambue kama wao ni wanajamii moja na siyo kondoo na wachungaji; na nne litakuwa chachu ya kuwafanza vijana kutoa kilicho bora kuisaidia jamii husika.Nitachukulia mfano mmoja tu, nao sio mwingine ila matumizi ya simu za mikononi na teknohama au teknolojia ya kileo ya mawasiliano duniani. Hali ilivyo ni kwamba shule nyingi za 'high school' zinakataza matumizi yake kiujumula. Je, hili ni sahihi? Je, tuko kwenye kwenda na wakati au tunapitwa na wakati?Je, jambo hili linawasaidia vijana hao ambao tunaamini kwa wakati wao ndiyo wenye akili kuliko wenzao wengi Tanzania?
Na je, wenye kuhamanika ni wanafunzi tu wakikosa simu au pia kuna wazazi wanaoumwa wakikosa mawasiliano na watoto wao kwa muda mrefu?Katika makala haya nitajaribu kuonyesha kiujumla jinsi kukataza matumizi ya simu ni makosa. Nitaonesha pia kwa kuazuia vijana hawa kwenda na wakati, tunalirudisha taifa zima nyuma kimaendeleo na hasa katika matumizi ya teknolojia mpya. Binafsi, nina hakika jambo hili kisaikolojia na kisosholojia haliwasaaidii baadhi ya watoto hao.
Katika kujumlisha, nitabainisha kwamba kuna uwezekano wa kuruhusu matumizi ya teknohama hii katika 'High school' kwa faida kwa wanafunzi, walimu, shule na jamii husika kwa ujumla.Katika baadhi ya shule simu za mkononi zinaruhusiwa kwa upendeleo. Hususan viongozi wa wanafunzi wana ruhusa lakini siyo wenzao. Sababu inayotolewa hapa ni kwamba wao wataitumia kwa dharura (emergency) kama vile kukitokea ugonjwa, ajali kama moto na vitu kama hivyo.
Lakini, ukishampa mwanafunzi kiongozi simu, hatoishia kungoja ajali tu ndiyo aitumie. Ataitumia pia kwa masuala yake binafsi. Je, hapo hapatakuwa na walakini?Baadhi ya benki zilipokataza matumizi ya simu ndani ya benki, lakini wakaona agizo hilo linapuuzwa na kila mtu walichokifanya siyo kuzuia watu kuingia na simu. Walitumia teknolojia. Ukiwa ndani ya benki simu yako inakuwa 'disable' ki-oto, yaani, haipokei wala kutoa sauti yoyote, ila unaweza kutuma ujumbe. Twende na wakati, twende na teknolojia. Hizi ndizo kazi wataalamu wetu wa teknohama wanazotakiwa kuzifanya na siyo kuigeuza mitandao makazi ya mashushushu na umbeya. Shule na vyuo zinaweza kabisa kuwa na maeneo ambayo upuuzi wa kupiga na kupokea simu haukubaliki na hauwezekaniki.
Hivi leo simu siyo chombo tu cha kuzungumza bali ni chombo chenye zana kadhaa muhimu katika maisha ye kila siku.
Watumiaji wengi wa simu wanatumia tu pengine asilimia 5-10 ya uwezo wake. Kwani hivi leo simu ni saa, kalenda, kompyuta, gazeti, maaktaba, modemu, redio, tivii, intaneti na vikorombwezo vyake vyote, dakisu (diary), sanduku la barua, ujumbe wa sauti unaohifadhiwa, daftari la kuhifadhi vitu vingi kiurahisi na katika mpangilio makini, sahili na fasili kuutumia.Je, baada ya kuzitambua sifa zote hizo hapo juu kweli ni nani kama siyo kijana wa kidato cha tano-sita anayetakiwa kuzing'amua na kuzifanzia kazi, wakati wengi wetu ndiyo kama hivyo tunaziogopa hata kompyuta?
Na je, siyo kweli kwamba tutakuwa tunairudhisha nyuma nchi kwa kuwazuia vijana hao ufikivu kwa teknohama?Ikumbukwe kuwa vijana wanaomaliza kidato cha sita ni wachache watakaoingia moja kwa moja chuo kikuu ikilinganishwa na wingi wao. Lakini wengi wao ni soko muhimu la ajira kwa wasiotaka kuanza na waliohitimu shahada ya kwanza. Aidha, kuna vyuo ambavyondani ya mwaka mmoja au miaka miwli vinakuwa vimemfunza na kumpeleka sokoni mwanafunzi husika. Je, kwa kuutumia muda huu kuielewa na kuitumia vyema teknohama hatutakuwa tumemsaidia kijana huyu kuajiriwa kiurahisi akiwa na aina fulani ya ufundi ambao kajisomea yeye mwenyewe?Na kwa namna hiyo tunashindwa kuwaandaa wanafunzi hao tayari kuingia chuo kikuu, ambako wanafunzi wana uhuru mkubwa na hakuna wa kuwasimamia kwa athari mbaya hasa kwa waliokuwa wakilindwa kupita kiasi.

Kwa nini shule zinakubali kukataza simu?
Uchunguzi unabainisha kuna sababu kadhaa zinazowafanya wakuu wa shule wakubali kupigwa marufuku simu za mkononi.
Sababu ya kwanza ni ile ya kimataifa. Shule zinafuata mkumbo wa mataifa ambao umeamua kuwa simu isiruhusiwe kwenye shule fulani fulani.
Tofauti na wenzetu, wao wanazingatia pia kama mhusika anayezuiwa amefikia umri wa utu uzima au la. Karibu nchi zote zinafanya hivyo kwa nia njema, lakini wakati mwingine kuwahami vijana kumezaa balaa kubwa zaidi kuliko kama wangekuwa na uhuru kiasi fulani.
Huko Korea ya Kusini baada ya vijana kuwa huru kwa miaka kadhaa, ghafla walianza kunyang'anywa uhuru huo. Matokeo yake yakawa ongezeko la kutisha la watoto na vijana wanaojiua.
Katika baadhi ya nchi kutoruhusiwa simu shuleni ni amri iliyotoka ngazi za juu yaani wizarani au serikalini.Baadhi ya shule zinaamini kwamba kimasomo pamoja na kwamba hakuna utafiti wala ushahidi wa kutosha kama simu siyo rafiki wa matokeo mazuri ya mitihani.
Utaona kigezo hapa si elimu, bali kukariri na kufaulu mitihani.
Hili linaendana na lile la kisaikolojia kwamba wanafunzi wanaweza kupata matatizo kwa kupokea taarifa zisizo nzuri au vitisho kutoka kwa wanaowapigia simu.

Aidha, upo ushahidi wa kutosha wa ulevi wa simu siyo tu kwa wanafunzi bali kwa watu wengine. Yaani, watu wanaotumia simu kupita kiasi na kuiona simu kama ni sehemu ya mwili wao kwa madhara ya afya yao ya kimwili na kiakili. Wanafunzi wa aina hii ukiwanyang'anya simu upo uwezekano mkubwa kwao kufanya vibaya katika masomo na mitihani. Je, hili tunalichukuliaje?

Katika baadhi ya shule kutokana na kipato kidogo cha walimu, baadhi ya wanafunzi wana simu nzuri na aghali kuliko za walimu. Kwa mfano, katika shule moja binafsi mwalimu mwenye simu kimeo aliamua mradi wa kuzikamata simu za wanafunzi ili angalau abahatishe kupata simu bora na ya kisasa zaidi. Alifanikiwa.

Kwa nini simu zinaogopwa mashuleni?
 Hofu mbalimbali zinachangia kwa shule na walimu kukataa kuwepo kwa simu mashuleni. Hofu hizo ni pamoja na shule kuhofia wanafunzi kufeli kutokana na kuendekeza simu zaidi kuliko masomo; kiutawala simu inakuwa kimapokeo ni kitu kisichoruhusiwa moja kwa moja.
Kwa upande mwingine kuzuka upya kwa matabaka ya kimaskini na kitajiri Tanzania kunachangia sana kuona vitu kama simu kuwa ni njia mojawapo ya kuwaathiri kisaikolojia walimu na wanafunzi kwa hasara ya shule na masomo; walimu wakuu na walimu wneye udikteta au utawala mbovu watapendelea simu kupigwa marufuku ili ukorofi, ugandamizaji, unayanyasaji na dhuluma dhidi ya wanafunzi isigundulike kiurahisi.Kutokana na uchache wa nafasi wiki ijayo katika sehemu ya pili nitaonesha ni kwa namna gani simu zinaweza kutumika mashuleni kwa faida ya wote, na hasa simu hizi za leo, ambazo wakati huo zinakuwa ni sawa na kompyuta, kitabu, redio, gazeti na tivii.
Makala  kwa  hisani  ya : http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/39-hoja-binafsi/25778-kwa-nini-wanafunzi-high-school-waruhusiwe-kuwa-na-simu-i
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top