Social Icons

Loading...

Wafanyakazi Wakatae Hadaa Za Mifuko Ya Jamii


HATUSHANGAI hata kidogo kuona moto unaendelea kuwaka nchi nzima kutokana na wafanyakazi kupinga Mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012,  ambayo inazuia wanachama wa mifuko hiyo kulipwa mafao yao kabla ya kufikia umri wa miaka 55 na 60.Hatushangai pia kuona mabadiliko ya sheria hiyo yanazua mtafaruku mkubwa kiasi cha maelfu ya wafanyakazi nchini kuapa kuwa liwalo na liwe, wataendelea kupinga mabadiliko hayo hata ikibidi waache au wafukuzwe kazi.
Kitu kinachotushangaza, ambacho hakika hakikutegemewa na wengi ni hatua ya wabunge kutaka sheria hiyo walioipitisha wenyewe Aprili mwaka huu irudishwe bungeni ili kipengele kinachowazuia wafanyakazi kuchukua mafao yao kabla hawajafikisha umri huo kiondolewe.
Wabunge walifadhaika bungeni juzi, wakati mmoja wao alipowaumbua kwa kusema ni aibu kwamba Bunge lililopitisha sheria hiyo ndilo linalogeuka na kuikana na kuwa, huo ni uthibitisho kwamba wabunge wote siyo makini.Kitendawili kinachopaswa kuteguliwa ni jinsi gani wabunge walipitisha sheria hiyo bila kuona udhaifu wanaozungumzia sasa, licha ya Bunge hilo kuwa na wabunge wengi wenye taaluma na weledi katika tasnia ya sheria.
Ndiyo maana tunashawishika kukubaliana na wakosoaji wanaosema kwamba wabunge walipitisha sheria hiyo pasipo kuisoma kwa kuwa sheria hiyo haina masilahi kwao, kwani wao wanalipwa kiinua mgongo na Serikali kila baada ya miaka mitano, badala ya pensheni zinazolipwa kwa wafanyakazi na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii.    Tunaambiwa sasa kwamba zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane nchini tayari wameacha kazi na wengine 4,000 wakiwa wamewasilisha barua za kufanya hivyo kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo.Kama kelele zinazopigwa kila kona nchini ni kielelezo cha hasira walizonazo wafanyakazi katika sekta mbalimbali nchini kutokana na mabadiliko ya sheria hiyo, basi tutegemee hali ya sintofahamu ya mivutano na migomo inayoweza kuathiri uchumi na amani yetu kwa kiasi kikubwa.
Sisi hatuoni namna Serikali na viongozi wa mifuko hiyo wanavyoweza kujikwamua kutoka katika mgogoro huo au kuzima hasira na vuguvugu za wafanyakazi wanaopinga sheria hiyo pasipo kuirudisha sheria hiyo bungeni na kufuta kipengele hicho kandamizi na chenye utata mkubwa.Pia tunapata shida kuelewa kwa nini mabadiliko hayo yanakuja wakati huu, ambapo mifuko hiyo imetumia matrilioni ya fedha za wafanyakazi katika miradi mingi mikubwa, ukiwamo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini imeshindwa kupata marejesho ya fedha hizo.
Tunaishauri Serikali na viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), zibadilishe sheria ya mifuko hiyo ya jamii ili iwanufaishe wafanyakazi.
Tunadhani pia wakati umefika sasa kwa wafanyakazi kuhakikisha wanafaidika zaidi na mifuko hiyo, ikiwamo kulipwa riba ya fedha wanazowekeza katika mifuko hiyo miaka nenda miaka rudi.
chanzo : Mwananchi
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top