Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo |
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma jana, waziri huyo alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio mijini.
Profesa Muhongo alisema pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni zilizokuwa zikilipwa awali.“Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”
Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.
Machi 18 mwaka jana, Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.
Chanzo. http://www.mwananchi.co.tz
Post a Comment