Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinalaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya
wana siasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu
ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza
na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri
Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi
za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la
tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano
mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa
Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa
aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na
kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na
kuongeza;
"Cha
kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote
tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa
Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa
hii".
Nape
alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na
kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
"Tunamtaka
Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala
yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya
uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti",
alisena Nape.
Alisema
CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao
wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga
sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa
tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape
alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na
Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake,
Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na
umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara
hiyo.
"Tunaamini
uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi
wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi
zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia.
Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema,
pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na
rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya
maendeleo.
"Tunawaomba
waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na
uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.
Post a Comment