Ndoto ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushiriki
fainali za Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) ‘zilipeperuka’
jana kwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka Timu ya Taifa ya Uganda, The Cranes
katika mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Namboole, Kampala.
Safari ya Stars imepotea kwenye michuano hiyo
itakayopigwa Afrika Kusini mwakani, baada ya kufungwa nyumbani na
ugenini na kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 4-1.
Taifa Stars, ambayo ilishiriki fainali za kwanza
za CHAN kule Senegal mwaka 2009 chini ya Kocha Mbrazil, Marcio Maximo,
sasa itasubiri kucheza tena michuano hiyo mwaka 2016.Matokeo hayo yanaifanya Uganda kuendelea kuifunga
Tanzania inavyotaka, kwani katika mechi 41 walizokutana, wameshinda
mechi 25 dhidi ya mechi 11.
Katika mchezo huo, wenyeji Uganda wakicheza kwa
kujiamini, walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Tanzania katika dakika
ya kwanza na sita baadaye waliandika bao la kwanza.
The Cranes walifunga bao hilo wakitumia makosa ya
mabeki wa Stars walioshindwa kujipanga vizuri na kumruhusu Mpande Joseph
kuruka juu bila kukabwa na kupiga kichwa mpira uliomkuta Kalanda Frank
aliyemtungua kipa Juma Kaseja.
Uganda walirudi kwenye uongozi mwanzoni mwa
kipindi cha pili kwa kufunga bao la pili lililotokana na kiki ya penalti
ya Brian Majwegwa kutokana na beki wa Stars David Luhende kuucheza
mpira kwa mkono alipokuwa kwenye harakati za kuondoa hatari.
Safari ya Taifa Stars kwenda Afrika Kusini ilizidi
kupotea baada ya wenyeji Uganda kufunga bao la tatu kutokana na
shambulizi la kushtukiza katika dakika ya 47.
Hakuna shaka, bao hilo lililofungwa na Frank
Kalanda lilitokana na uzembe wa kiungo Abubakary Salum, ambaye jaribio
lake la kutaka kuumiliki mpira mbele ya wachezaji wawili wa Uganda
lilishindikana na hivyo kuwapa mwanya wa kufanya shambulizi la
kushtukiza.
Bao pekee la Stars lilifungwa dakika ya 17 na Amri
Kiemba kwa shuti la nje ya 18 akimalizia kazi nzuri ya winga Mrisho
Ngasa aliyecheza vizuri kipindi cha kwanza.
Mbali na mabao hayo, Stars wangeweza kuwa mbele
kwa mabao 2-1 katika dakika ya 35, kama siyo kiki kali ya umbali mrefu
iliyopigwa na Ngasa na kugonga ‘paa’ la Uganda na mpira kurudi uwanjani.
Kipa na nahodha wa Stars, Kaseja alifanya kazi ya
ziada kupangua shuti kali la Mpande Joseph, huku dakika ya 11 mpira wa
kichwa kutoka wa beki Aggrey Morris ukipaa juu kidogo ya lango kufuatia
kona ya Erasto Nyoni.
Post a Comment