Tume ya kuchunguza ajali ya boti ya MV Skagit,
imekamilisha uchunguzi wake na kubainisha kuwa Nahodha aliyekuwa
akiendesha boti hiyo hakuwa na sifa wala ujuzi na kupendekeza viongozi
kadhaa wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Kutokana
na kutokuwa na ujuzi, Nahodha huyo alishindwa kuwaandaa abiria wake
kujiokoa wala kutoa taarifa ya dharura kwa vyombo vinavyohusika na mambo
ya usalama, licha ya kuona boti yake ipo katika hatari za kuzama.
Katibu
Mkuu Kiongozi wa SMZ, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema serikali
imeyakubali mapendekezo yote na kuyafanyia kazi kwa kuwachukulia hatua
za kisheria na kinidhamu waliohusika na uzembe na kusababisha vifo vya
watu wasio na hatia.
Dk.
Abdulhamid ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, alisema
Nahodha Makame Mussa Makame alikuwa akiendesha boti ya MV Skagit bila
kuwa na cheti cha umahiri.
Alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria kifungu 167(1), cha sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006.
Aidha
alisema ripoti hiyo imebaini Nahodha alikuwa akiendesha meli hiyo, huku
akijua meli hiyo haipo salama kwa kutokuwepo Mhandisi Mkuu wakati wa
safari zake, na badala yake alikuwepo Mhandisi Msaidizi asiye na sifa
kitu ambacho ni kinyume na kifungu cha sheria ya usafiri wa baharini
321(1) namba 5 ya mwaka 2006.
Aliongeza
kuwa uzembe umebainika baada ya meli hiyo kupakia abiria 431 badala ya
uwezo wake wa abiria 250 kitu ambacho ni kinyume na kanuni ya 4 na 5 za
kanuni ya hesabu na usajili wa abiria ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano
ya mwaka 2011.
Alisema
ripoti hiyo imebaini maiti 81 zilipatikana na kutambuliwa majina yao,
na watu 212 wamepotea kusikojulikana, na 154 waliokolewa katika ajali
hiyo wakiwemo raia wa kigeni 18, na watatu walikufa.
Alisema tume imependekeza mmiliki na nahodha wa boti hiyo washitakiwe kwa kosa la kusababisha vifo kutokana na uzembe.
Jaji
Abdlhakim Ameir Issa, ambaye alikuwa akiongoza tume hiyo alisema tume
imependekeza aliyekuwa Kaimu Mkaguzi wa meli, Juma Seif Juma, achukuliwe
hatua za kinidhamu kwa kuisajili boti ya MV Skagit na kuipatia cheti
cha usajili wa muda pamoja na cheti cha usajili wa kudumu bila ya
kufuata masharti ya usajili yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria katika
kifungu cha 31 namba 5 ya mwaka 2006.
Tume
hiyo pia imependekeza Mkaguzi wa kujitegemea, Captain Saad Shafi Adam,
kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufutwa uteuzi wake wa kuwa
mkaguzi wa meli anayetumiwa na ZMA, kwa kutoa mapendekezo ya kusajiliwa
MV Skagit, baada ya kuifanyia ukaguzi ambao haukufuata masharti ya
vifungu vya 192 na 194 vya sheria ya usafiri wa baharini, namba 5/2006.
Wengine
waliopendekezwa na tume hiyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni Maafisa
Usalama wa Bandari ya Dar es salaam, Johari Mikidadi, Ndumbati na Peter
Ndimbwa Mwasi, kwa kushindwa kudhibiti uingiaji wa abiria kinyume na
majukumu yao ya kazi.
“Tume
inapendekeza Mmiliki wa meli hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya
Seagull Sea Transport Said Abdulrahman Mbuzi achukuliwe hatua za
kisheria kwa kufanya biashara ya usafiri wa baharini kwa kutumia chombo
ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria ya usafiri wa baharini
Zanzibar namba 5/2006,” alisema Dk. Abdulhamid Mzee.
Aidha,
tume hiyo imependekeza fidia za aina tatu za kuwalipa waathirika sawa
na kima cha chini cha mshahara kwa muda wa miezi 80. Kima cha chini cha
Zanzibar Sh. 150,000 kitakipwa kwa waliofariki, wakati walionusurika na
kupata ulemavu walipwe asilimia 75 ya kiwango hicho, na asilimia 50 ya
kiwango hicho walipwe walionusurika bila ya kupata ulemavu.
HABARI NA MWINYI SADALLAH
SOURCE: NIPASHE
Post a Comment