WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewapiga marufuku
wafanyakazi wote walio chini ya wizara yake kusafiri kwa ndege katika
daraja la kwanza, akieleza kuwa huo ni ubadhirifu wa fedha za
umma.Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga jana, Mwakyembe
alisema atakayekaidi agizo hilo, atakatwa fedha katika mshahara wake.
Mwakyembe ambaye tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Uchukuzi amekuwa akifanya uamuzi magumu, alisema hawezi kuvumiliamtu
yeyote ambaye atatumia hovyo fedha za walipa kodi, huku akiwataka
wafanyakazi wa wizara yake kufanya kazi kwa maadili na kuwatumikia
wananchi.“Kulingana na hali halisi ya maisha ya baadhi ya ya Watanzania, wizara yangu haitakuwa tayari kuona fedha zikitafunwa na watu wachache kwa njia za kifisadi. Matumizi yafanyike kulingana na hali halisi ya Watanzania,” alisema Mwakyembe na kuongeza;“Kuanzia leo nawapiga marufuku watendaji wote wa wizara yangu kusafiri na ndege kwa kutumia daraja la kwanza.”
Akizungumzia hali za Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA), Dk Mwakyembe alisema, Wizara yake imeunda bodi ya watu wanane ambao wataanza kazi Januari mwakani. Alisema kikosi kazi hicho, kitaleta mapinduzi ya utendaji wa kazi katika mamlaka hiyo.
Alisema bodi hiyo itatambulishwa mara baada ya kukamilika kwa baadhi ya mambo muhimu na hivyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.Alisema kwa sasa bodi hiyo imeanza mikakati ya kuhakikisha Tanzania inaingia kwa nguvu zote katika soko la ushindani la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alisema Wizara yake inakusudia kuleta mageuzi katika sekta ya usafirishaji katika bandari zake (PTA) ili kuweza kuleta ushindani wa kibiashara na nchi jirani na kuweza kuwavutia wafanyabiashara watakaoweza kushusha shehena zao katika bandari zake.‘Baada ya kuunda bodi mpya ya watu wanane ya (PTA), tumedhamiria kwa dhati kuondoa madudu ambayo yalikuwa yanatusumbua katika bandari zetu na kuonekana kama tumeshindwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Akizungumzia kuhusu Bandari Mpya ya Mwambani ambayo ujenzi wake bado haujaanza, Waziri Mwakyembe, alisema wale ambao wana ubeza mradi huo mwisho wake wataumbuka kwani ndani ya miezi sita ijayo utaanza.
Chanzo Gazeti la Mwananchi.
Post a Comment