Mr Joseph Muganda |
NMG inamiliki vyombo vya habari Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda.
Uteuzi wa Muganda umekuja baada ya Mkurugenzi
Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu aliyepo, Linus Gitahi kuomba kustaafu
mapema ili aendelee na shughuli zake binafsi.
Taarifa iliyotolewa na NMG ilieleza kuwa Muganda
ni mtendaji mwandamizi mwenye uzoefu mkubwa katika tasnia ya utawala na
masoko na amejiunga na kampuni hiyo ya habari Afrika Mashariki na Kati
akitokea Kampuni ya Bia ya Kenya (KBL) akiwa pia ni Mkurugenzi Mtendaji.
Akitangaza mabadiliko hayo jana, Mwenyekiti wa
Bodi ya NMG, Wilfred Kiboro alitoa shukrani kwa Gitahi kwa mchango wake
katika maendeleo ya kampuni kwa kipindi cha miaka minane aliyotumikia
katika cheo hicho.
Alisema Gitahi alisimamia uanzishwaji wa bidhaa na
huduma mpya na upanuzi wa kampuni katika masoko mapya na kuongeza mauzo
kutoka Sh116.5 bilioni hadi Sh247.9 bilioni. Pia, aliongeza faida ya
kampuni kabla ya kodi kutoka Sh22.2 bilioni hadi Sh66.6 bilioni.
Kiboro alimweleza Gitahi kuwa alikuwa mfano wa
kuigwa kiuongozi katika kipindi kigumu katika uendeshaji wa sekta ya
habari nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Gitahi ataendelea kusimamia shughuli za NMG hadi
Juni 30 mwaka huu kabla ya kukabidhi ofisi kwa Muganda na pia atatoa
huduma za ushauri hadi mwishoni mwa mwaka.
Akimkaribisha Muganda katika kampuni ya NMG
inayomiliki pia kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)
inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, Kiboro
alisema:
“NMG inayo furaha kumkaribisha Muganda katika timu
yetu ambapo analeta utaalamu wa masuala ya masoko, usimamizi wa
mawasiliano, mashirika na udhibiti na utendaji ambao umejengwa na uzoefu
wa kipindi kirefu katika mashirika mbalimbali ya kimataifa barani
Afrika.”
Kwa upande wake, Muganda alisema anayo furaha
kujiunga na NMG na kujumuika katika utekelezaji wa kazi na wajibu wa
kuwa chombo cha habari chenye ubora wa hali ya juu na huru katika kukuza
maendeleo ya jamii.
Post a Comment