Harakati za kuwania urais ndani ya CCM zimeingia katika hatua
mpya baada ya mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru kuibuka na
kudai kuwa wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa
wanatumia fedha kutaka kuingia Ikulu.
Kauli ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja
kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda
ikitajwa kuwa suala la maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa
hao ambao wanaongezeka kila kukicha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kingunge alisema:
“Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi ya pesa na
nikwambie ukweli, hao wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia
faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”
Kwa miezi kadhaa sasa, baadhi ya makada wa CCM
wamekuwa wakitajwa kufanya harakati kichinichini na wengine kushiriki
shughuli za wazi zinazoashiria kuwa wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu.
Hadi sasa makada wanne tayari wameweka wazi nia yao hiyo.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli
zinazowashutumu makada wengine wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya
fedha katika kushawishi uungwaji mkono.
Hata hivyo, kauli za wanasiasa hao zimedaiwa kuwa
ni fitina za kisiasa kwa kuwa wagombea wote wanatoa fedha, bali
wanazidiana viwango tu.
Chanzo: gazeti la mwananchi .
Post a Comment