Dar es Salaam. Moto mkubwa umeua mtu mmoja na kujeruhi wengine
19 waliokuwa wanachota mafuta ya petroli yaliyomwagika baada ya lori
kupinduka.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 5.15 usiku wakati
lori hilo liliposhindwa kukata kona kwenye mzunguko wa Mbagala Rangi
Tatu jijini Dar es Salaam na kuanguka kwenye mtaro.
Kaimu Kamanda wa Polisi Temeke, Nyigesa Wankyo
alimtaja aliyekufa katika tukio hilo kuwa ni Masoud Masoud mkazi wa
Mbagala Charambe.
Alisema baadhi ya majeruhi wa moto huo wamelazwa katika Hospitali ya Temeke na wengine Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mlipuko wa tanki hilo ulisababisha taharuki kwa
wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani ambao walidhani ni mlio wa bomu,
kutokana na kumbukumbu ya milipuko ya mabomu katika kambi ya jeshi
iliyotokea Aprili 29 mwaka 2009.
Fatma Mburalala mkazi wa Nzasa alisema juzi usiku saa 5.30 usiku ulisikika mlio unaofanana na bomu uliokuwa ukijirudiarudia.
“Wakazi wa mtaa wetu wote walitoka nje na familia
zao wakidhani kwamba ni mabomu. Tuliingia ndani saa 9.00 usiku baada ya
kupata taarifa kwamba ni lori limelipuka moto,” alisema.
Alisema wakazi wengi walikaa nje ya nyumba zao usiku kutokana na mlipuko huo wakidhani kuwa ni mabomu.
Kamanda Wankyo alisema mlipuko huo umesababishwa na watu waliokuwa wakiiba mafuta.
“Wezi waliiba mafuta na kwenda kuficha kwenye
nyumba za jirani na ulipotokea mlipuko huo moto ukafuata mafuta yalipo
na kuleta madhara,” alisema.
Wankyo alisema polisi haijafahamu thamani ya mali
zote zilizoteketea kwa moto na kwamba linafanya tathmini kwa
kushirikiana na wamiliki.
Post a Comment