KAMA Arsene Wenger alihitaji ukumbusho
wowote wa kosa alilofanya katika usajili akiwa kazini Arsenal, Didier
Drogba alifanya hivyo Uwanja wa Emirates Jumapili.
Mabao mawili ya Drogba ya dakika za lala
salama dhidi ya Arsenal yaliyowezesha Galatasaray kubeba Kombe la
Emirates yameendeleza rekodi ya mshambuliaji huyo dhidi ya The Gunners
na kufika mabao 15 katika mechi 15.
Kwamba, katika dakika 1175 ambazo Drogba
amecheza dhidi ya Arsenal, amefunga wastani wa bao moja katika kila
dakika 78 na sekunde 20.
Ulikuwa usiku wa pigo kwa Wenger, ambaye alikataa kumsajili Drogba kwa Pauni 100,000.
Akiwa anachipukia nyota huyo wa Ivory
Coast katika miaka yake minne Le Mans kati ya mwaka 1998 na 2002, jicho
la skauti wa Wenger lilimnasa mchezaji huyo.
Wenger alikataa kumsajili, na Drogba akahamia timu nyingine ya Ligue 1, Guingamp akiwa ana umri wa miaka 23 kwa Pauni 80,000.
Wenger alisema mwaka 2009:
"Tumemuangalia kwa umakini alipokuwa Le Mans. Siyo sisi tu
tuliomuangalia. Lakini tulifikiri hawezi tayari kiasi cha kutosha.
"Lilikuwa ni kosa, lakini ukiwa kwenye
soka, kila mmoja anaweza kuelewa. Tulikuwa na Thierry Henry. Tulisema
tutafuatilia maendeleo ya Drogba. Hatukuwahi kumkataa,"
Mwaka 2004, kufuatia msimu wa mafanikio makubwa akiwa Marseille, Drogba alisaini Chelsea kwa ada ya Pauni Milioni 24.
Kana kwamba hilo halikuwa pigo tosha katika jino la Wenger, Drogba aliifanyizia ile mbaya timu yake uwanjani.Alifunga mabao 13 katika mechi 14 dhidi ya Arsenal enzi zake akiwa Stamford Bridge, mengi kati yao akifunga katika mechi muhimu.
Wenger alipata ahueni wakati Drogba
alipoondoka Chelsea kuhamia Shanghai Shenhua mwaka jana, akisema wakati
huo: "Sijui ni kiasi gani Chelsea wamempoteza, lakini hatumkumbuki.
Amefanya madhara mengi dhidi yetu katika kila mechi,".
Drogba anaweza kuwa ukingoni mwa soka
yake akiwa na umri wa miaka 35 sasa, lakini kwa Emirates atabakia
kukumbukwa kama kiboko ya timu ya Wenger hadi siku atakapotungika daluga
zake.
Mfaransa huyo sasa atakuwa anaomba dua
Arsenal isipagwe kundi moja na Galatasaray katika Ligi ya Mabingwa
katika droo inayotarajiwa kupangwa mjini Monaco Agosti 29.
Taarifa na picha kwa hisani ya bin Zubeiry.
Taarifa na picha kwa hisani ya bin Zubeiry.
Post a Comment