Waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL)
inayochapa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti wameibuka
tena kidedea kwenye tuzo za umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania
(EJAT) kwa mwaka 2012, baada ya kushinda tuzo 13, ikiwamo ya mshindi wa
jumla.
Sherehe za utoaji wa tuzo hizo ilifanyika jana
katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali
akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad ambaye alimwakilisha
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Mshindi wa jumla kwa mwaka 2012 ni Lucas Liganga
wa gazeti la The Citizen, ambaye ameifanya MCL kunyakua tuzo hiyo kwa
miaka miwili mfululizo ambapo mwaka 2011 tuzo hiyo ilichukuliwa na
Neville Meena wa gazeti la Mwananchi.
Washindi walipewa zawadi za magodoro, televisheni,
Ipad na vyeti, huku mshindi wa jumla akipewa dola 4,000 za kujiendeleza
kimasomo.
MCL iliingiza fainali waandishi 14 kati ya 66
walioteuliwa kuwania tuzo hizo ambao ni pamoja na Samweli Mwamkinga,
Florence Majani, Polycarp Machira, Tom Musoba, Elias Msuya, Leon Bahati,
Lucas Liganga, Shija Felician, Fredy Azzah, Joseph Zablon, Zephania
Ubwani, Tumaini Msowoya, Anthony Mayunga na Edward Qorro.
Mbali na kutoa mshindi wa jumla, waandishi sita wa
magazeti hayo walikuwa ndio wagombea pekee wa tuzo mbili za habari bora
ya Uchumi na Biashara na Majanga, huku Azzah akishinda tuzo ya habari
bora ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambapo alikuwa peke yake na alichaguliwa
mara mbili kuwania tuzo hiyo.
Waandishi wa MCL walioshinda na tuzo zao katika
mabano ni Edward Qorro (Uchumi na Biashara), Lucas Liganga (Mazingira na
Malaria), Fredy Azzah (Ukimwi na Elimu), Anthony Mayunga (Utawala
Bora).
Wengine ni Florence Majani (Sayansi na Teknolojia
na Afya ya Uzazi), Samwel Mwakibinga (Mchora katuni bora), Zephania
Ubwani (Kilimo), Polycarp Machira (Majanga), Shija Felician (Tuzo ya
wazi).
Katika tuzo ya jumla MCL iliingiza waandishi watatu kati ya waandishi wanane waliochaguliwa kuwania tuzo hizo ambao ni Lucas Liganga, Fredy Azzah na Florence Majani.
Katika utoaji wa tuzo hizo, MCL ilifuatiwa na Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilizoa tuzo nane, Afya Redio (6) na Kilimanjaro Film Institute (5).
Chanzo: gazeti la mwananchi
Katika tuzo ya jumla MCL iliingiza waandishi watatu kati ya waandishi wanane waliochaguliwa kuwania tuzo hizo ambao ni Lucas Liganga, Fredy Azzah na Florence Majani.
Katika utoaji wa tuzo hizo, MCL ilifuatiwa na Shirika la Utangazaji (TBC) ambalo lilizoa tuzo nane, Afya Redio (6) na Kilimanjaro Film Institute (5).
Chanzo: gazeti la mwananchi
Post a Comment