HOJA binafsi ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, imeibua mapya
bungeni mjini Dodoma, baada ya Kambi ya Upinzani kukutana kwa dharura,
kupinga kufifishwa hoja hiyo na Naibu Spika, Job Ndugai, wakidai anataka
kuizima.Juzi Mbatia aliwasilisha bungeni Hoja Binafsi
kuhusu udhaifu wa elimu Tanzania, akitaka mfumo mzima unaosimamia elimu
nchini ufumuliwe.Baada ya majadiliano marefu kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitalaa, sera namihutasari
ya elimu, hoja mbalimbali zilitolewa, baadhi ya wabunge wakitaka Kamati
ya Bunge, huku wengine wakitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala
hilo.Mjadala huo uliendelea jana asubuhi kwa Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kusimama na kutetea
mfumo wa elimu uliopo na mtalaa, kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia
kuhitimisha.
Akiwasilisha hoja yake, Mbatia aling’ang’ania kupatiwa mtalaa wa masomo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari, jambo ambalo, Waziri Kawamba alijibu kuwa ulikuwapo ingawa hakuwa nao bungeni.
Baada ya majibu ya Dk Kawambwa, Mbatia aliomba hoja yake iahirishwe hadi mtalaa utakapowasilishwa bungeni.Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama na kusema akihoji: “Katika kikao kilichopita, hata katika Hansard, tulisema mtalaa utawasilishwa katika kikao hiki, sasa wasiwasi wa mbunge (Mbatia) ni nini? Hata siku ya mwisho ya Bunge tutaleta.”
Baada ya kauli hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipiga kura kwa kuuliza wanaotaka hoja imalizike na baada ya majibu, aliruhusu Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla kuwasilisha Hoja Binafsi kuhusu ajira kwa vijana na kilimo.Hata hivyo, baada ya kumruhusu Dk Kigwangalla, wabunge wa upinzani walitoka nje ya Bunge na kufanya mkutano wa dharura uliochukua dakika 38 katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
1 comments:
Safi sana mheshimiwa Mbatia,Mungu akubariki.
ReplyPost a Comment