MSHAMBULIAJI Lionel Messi amevunja rekodi kwa kutwaa tuzo ya Ballon D’Or kwa mara ya nne mfululizo – kisha akafungua
mdomo kumwambia kiungo aliyemshinda Andres Iniesta: Nisingeweza kufanya vema
kiasi hiki bila wewe.
Messi, 25, alimbwaga mkali
mwenzake huyo klabuni Nou Camp Iniesta na hasimu wake na nyota wa Real Madrid Cristiano
Ronaldo katika kubeba tuzo hiyo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka ya Fifa.
Na Messi nyota wa kimataifa wa
Argentina, ambaye anakuwa mwanasoka wa kwanza kutwaa tuzo hiyo mara nne
mfululizo duniani, alisisitiza kuwa ameyaweza yote katika msaada wa rafikiye
huyo Iniesta.
“Ni jambo la kuvutia sana
kupokea tena tuzo hii kwa mara ya nne mfululizo. Kila mmoja anastahili tuzo hii.
Huwezi kuja hapa ukitambua na kufikiria kwamba ni wewe tu unayestahilio na
kwamba unakuja kushinda.
“Ningependa kushirikisha
furaha hii na nyota wengine wa FC Barcelona – hasa Andres Iniesta, ambaye yuko hapa
na mimi.
“Najisikia fahari kubwa
kufanya naye mazoezi kila siku. Mimi pia nawafikiria wachezaji wenzangu wa timu
ya taifa ya Argentina.
“Shukrani za dhati kwa wote
ambao walipiga kura kunichagua mimi kushinda tuzo hii, miongoni mwa manahodha, makocha
wa klabu na makocha wa timu za mataifa mbalimbali.
“Shukrani zaidi ziifikie
familia yangu, rafiki zangu na bila shaka kwa mke na mwanangu wa kiume, ambao
kwao hiki kilichotokea kwangu leo ni kitu bora.”
Messi ameshinda tuzo hiyo
katika mwaka aliofululiza kuvunja rekodi moja baada ya nyingine katika
ulimwengu wa soka, akifunga jumla ya mabao 91 na kuivunja rekodi iliyodumu kwa
miaka 40 ya Gerd Muller kufunga mabao 85 kwa kalenda ya mwaka.
Kocha wa timu ya taifa ya
Hispania, Vicente Del Bosque alijishindia tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka, akibebwa
na ubingwa wa Mataifa Ulaya ‘Euro 2012’ katika fainali zilizopigwa nchini Poland
na Ukraine mwaka jana.
Post a Comment