Social Icons

Loading...

Mbunge Mtarajiwa Aliyeokoka Aongelea Sakata La Gesi Mkoani Mtwara

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MADAI YA WANAMTWARA KUSHINIKIZA KUCHAKATWA KWA GESI KATIKA MJI WA MTWARA NA KUTOSAFIRISHA GESI GAFI KWA BOMBA KWENDA DAR ES SALAM.
TAREHE 07-01-2013.
Ndugu waandishi wa Habari kwanza ningependa kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wenu kuja hapa leo kuyasikiliza yale ambayo nimekusudia kuyaongea.
Pili ningependa kuwapongeza sana kwa namna mnavyoripoti habari hizi kila wakati bila kuchoka na kuyafuatilia matukio na kueleza hoja na hisia za wananchi wa Mtwara kila kunapokucha.
Najua ziko shutuma zilizotolewa na viongozi wa serikali kwamba wanaozungumzia jambo hili wanatafuta umaarufu wa kisiasa,nadhani hiyo ilikuwa mbinu ya kuziba mdomo tusizungumze.Swala hili ni nyeti na lina sura ya kitaifa ni wajibu wa kila mpenda maendeleo ya nchi hii kulizungumzia kwa ustawi wa watu wetu,ndicho ninachofanya leo,uzalendo unanitaka kufanya hivyo.Nikinukuu maneno ya mpigania haki za wanawake nchini Afghanistan Mama Malalai Joya aliyewahi kusema”The silence of Good people is worse than the actions of Bad people ” Hivyo kukaa kwangu kimya ni kubaya zaidi kuleta matendo mabaya ya mtu yeyote yule,ili nisiwe kwenye kundi hilo naomba nivunje ukimya huo.
Nianze kwa kusema kuwa ningependa kutoa maoni yangu kama mwananchi wa kawaida ninayeguswa na jambo hili na ninatumia haki yangu ya kikatiba kwa mujibu ya ibara ya 18 kipengele (A).Ingawa ukweli utabaki kuwa mimi ni mwanachama wa chama cha mapinduzi na historia inajieleza kuwa  nimeshawahi kuwa katibu msaidizi wa CCM wilaya  na mgombea wa ubunge katika kura za maoni mwaka 2010 katika uchaguzi wa ndani ya chama kwa jimbo la Mtwara Mjini.
Tangu kuanza kwa vuguvugu la mradi wa ujenzi wa bomba la gesi nimetumia  muda mwingi kuwa Mtwara kuliko Dar es Salaam ambako hasa ndiko ninakofanya shughuli zangu.
Kabla vuguvugu hili halijachukua sura kubwa ya kitaifa yalikuwepo manun’guniko mengi kwa wananchi yaliyoonyesha kutoridhishwa na kufanyika kwa mradi huu.Ikumbukwe kuwa ingawa mkataba wa kupata mkopo wa ujenzi wa bomba kutoka benki ya Exim china(Takribani usd 1Bill) ulisainiwa nchini china tarehe 26 september 2011 na ujumbe uliiongozwa na waziri wa wakati huo wa Nishati na Madini William ngeleja,kujulikana kwa utekelezwaji wa mradi huu kwa watu wengi ulikuwa ni pale mheshimiwa Rais alipozindua mradi wa kujenga mtambo wa kufua umeme kinyerezi tarehe 8/November/2012 ambao ungetokana na gesi kutoka Mtwara ikiungana na bomba la songosongo,hapa ikiwa ni takribani mwaka mmoja kupita tangu kusainiwa.
Kwa kulitazama jambo hili kutokea mbali na kwa kutoridhishwa na ukimya uliotawala kwa viongozi wa serikali na wawakilishi wa wananchi,nilichukua hatua za makusudi kufanya ufuatiliaji mbalimbali.Hatua yangu ya kwanza ilikuwa kwenda TPDC ofisi ya mkurugenzi tarehe12 december 2012 ikiwa ndiyo mwakilishi wa serikali anayesimamia mradi huu ili kuhoji mambo kadhaa na kutoa mtazamo wangu wa umuhimu wa kusimamishwa kwa mradi huu ili kusikiiliza kilio cha wananchi.Ingawa sikufanikiwa kuonana na mkurugenzi nilifanikiwa kukutanishwa na wakuu wa kitengo cha malalamiko yanayohusu mradi huu ambao kwa ukweli ni kwamba walisisitiza tatizo kubwa ni kutokuelewa kwa wananchi na kupuuza hoja yangu ya msingi ya kutaka ujenzi wa bomba hili usimamishwe ili kusikiliza hoja za msingi za wananchi.
Baada ya hapo nilichukua hatua ya kuomba msaada wakisheria kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu ili kusitisha mradi huu kwa kuwasiliana na mkurugenzi wa kituo hicho Bi hellen Kijo bisimba mnamo tarehe 17dec 2012 ambaye alinieleza kuwa alishatuma ujumbe wake Mtwara na wako katika hatua za kuandika ripoti hivyo niisubirie.Kwa bahati mbaya sana bado sijafanikiwa kuipata ripoti yao.
Sikuishia hapo,niliamua kuandika barua kwa ngazi za manispaa ya Mtwara mnamo tarehe 18 dec 2012 ikiwa na madai kadhaa na mapendekezo ya nini kifanyike kuhusiana na mradi huu.Kati ya madai yangu ilikuwa kumtaka meya wa manispaa kuitisha kikao cha haraka cha baraza la madiwani kulijadili jambo hili kama la dharura wakiwa ndio wawakilishi wa wananchi na kutoa msimamo wao kwa serikali kuitaka kusitisha mradi huu na kusikiliza kilio cha wananchi.Juhudi hii nayo haikuzaa matunda kwani sikupata jibu lolote la barua yangu wala utekelezaji wake hadi hii leo.
Baada ya hapo nilishiriki kikamilifu katika mijadala ya sera na vipindi mbalimbali vya redio nikihimiza kusitishwa kwa ujenzi wa bomba hili hadi pale hoja za wananchi zitakapojibiwa kama vile nilivyonukuliwa katika gazeti la mwananchi la tarehe 26 december 2012 ukurasa wa kumi ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika maandamano makubwa siku ya tarehe 27.
Nimeeleza haya yote ili kuonyesha kuwa kwa mtu yeyote anayeona mbali ni lazima alijua kuwa bila ya kusikilizwa kwa kilio hiki cha wananchi ni lazima tungefika hapa tulipo na kuna uwezekano wa kwenda mbali zaidi kuliko hapa kama hatua stahiki hazitachukuliwa.
Baada ya kusema hayo ningependa kutoa masikitiko yangu kwa kauli za kejeli,dharau na kukatisha tamaa zilizotolewa na viongozi waandamizi wa serikali Mh.Waziri Sospeter Muhongo na mkuu wa mkoa wa Mtwara(Joseph Simbakalia)  mara baada ya maandamano ya tarehe 27 dec.Pia napenda kueleza kusikitishwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa kuhusu ujenzi wa bomba hili katika salamu zake za mwaka mpya,napenda kutumia nafasi hii kumshauri Mh.Rais,Waziri wa Nishati na Madini na Mkuu wa mkoa kupitia upya madai 9 yalisomwa siku ya maandamano ili kutoupotosha mjadala na madai ya watu wa Mtwara.
Nimetoa rai hiyo kwasababu ukipitia hotuba za viongozi hawa wote utagundua kuwa aidha wamepewa taarifa zisizo sahihi kuhusu madai ya wanamtwara ama wamefanya haraka kujibu au hawajaelewa kabisa madai ya wanamtwara.Kwani kilichofanyika si kujibu madai yao bali kuonyesha jinsi ambavyo hawako tayari kuwasikiliza,nadhani mtazamo huu ndio unaochochea jambo hili kuwa kubwa kila siku na kuwapa mtazamo wananchi kuwa kuna ajenda ya siri katika hili.
Naomba kuchukua nafasi hii kueleza kuwa WANANCHI WA MKOA WA MTWARA HAWAPINGI WANANCHI WA MIKOA MINGINE KUNUFAIKA NA FAIDA ZA GESI BALI KINACHOPINGWA NI KUSAFIRISHA GESI GAFI TOFAUTI NA AHADI YA SERIKALI YA KUJENGA MTAMBO WA KUZALISHA UMEME MKOANI MTWARA UTAKAOVUTIA WAWEKEZAJI WA VIWANDA.UMEME HUU UNAWEZA KUSAFIRISHWA KWENDA MAHALI POPOTE TANZANIA/NJE YA NCHI BAADA YA MTAMBO KUJENGWA MTWARA.
Naomba kukumbusha kuwa madai haya hayajotoka hewani,bali yametokana na sababu kadhaa:
1.     Ni ahadi za mara kwa mara zilizokuwa zilizotolewa na Mh.Rais na mawaziri wa Nishati na Madini katika nyakati tofauti.Tangu mara ya kwanza Mh.Rais alipohojiwa clouds(kipindi cha power breakfast) tarehe 29 october katika  kampeni ya mwaka 2010,pia alipokuja kwenye kampeni Mtwara na hata alipokuja kushukuru baada ya kuwa Rais aliendelea kuahidi kuufanya Mtwara kuwa mji wa viwanda kwa kuupatia umeme wa uhakika kupitia ugunduzi wa gesi hii,pia alieleza katika kipindi hicho cha radio kusudio la serikali yake kujenga mtambo wa 300MW.Hii yote ilitengeneza matumaini makubwa kwa wananchi wa Mtwara wa kufaidika na gesi hii.Leo tunaposikia gesi ghafi inahamishwa na bado hakuna mtambo huo wala kiwanda sawa na ahadi zilivyotolewa,kuna kosa gani wananchi wakihoji?
2.     Mpango wa Mtwara power project uliolenga kuufanya mradi huu kuwa sehemu ya National power Development plan(3920MW) ukilenga kuwa na mtambo wa kuzalisha 300MW Mtwara zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa na kuondoa tatizo la umeme nchini uliokuwa umelenga kukamilika mwaka 2012.Ingawa ni wazi kuwa kampuni iliyokuwa itekeleze mradi huu Artumas ilishindwa kutokana na mtikisiko wa kiuchumi wa mwaka 2008,iliweka bayana kuwa ingepata dola za kimarekani milioni 7 ingeweza kuutekeleza.Kwa nini serikali haikuweka kama sharti mojawapo kwa kampuni ya Wentworthy resource Limited iliyoinunua artumas kuutekeleza mradi huu uliokuwa umekubalika kuingia katika mpango wa kitaifa?kwa nini uliachwa?Hili nalo hatuna majibu kama ilivyo kwa mipango mingine kama vile Mtwara Corridor.
3.     Ikumbukwe kuwa kisiwa cha songosongo ndio eneo la kwanza kugunduliwa kwa gesi asilia mwaka 1974 na kampuni ya AGIP kukiwa na takriban cubic feet 783 billion.Kati ya mipango mingi iliyowekwa kwa wakati huo kuhusiana na kubadilisha maisha ya wanasongosongo na kilwa kwa ujumla ni kujenga kiwanda cha mbolea KILWA AMMONIUM COMPANY,kilicholenga kutatua tatizo la ajira na kutosheleza uzalishaji wa mbolea nchini.Waliambiwa wasiwe na hofu gesi kwenda Dar es Salaam kwani viwanda vitajengwa kilwa,Ingawa eneo lilitengwa kwa ujenzi wa kiwanda hicho na wataalamu kusomeshwa,hadi hivi leo kiwanda hakijajengwa. Hivi hali kama hii haitoshi kuleta wasiwasi kwa wananchi?kuna tatizo gani wakihoji jambo hili?Waswahili husema ukiona mwenzako ananyolewa,wewe tia maji.
Kama viwanda hivi vitafanikiwa vitaleta tija na ulazima wa kuifufua bandari ya Mtwara ambayo tangu mwaka 2006/2007 imekuwa ikitumika kwa 31% ya uwezo wake(Tani 122,862 kwa mwaka badala ya tani 400,000 kwa mwaka).Mbinu hii itasaidia kupunguza msongamano wa bandari ya Dar kama ambavyo nchi Jirani ya Kenya wamefanya kwa kuipanua bandari ya Lamu ili kupunguza msongamano bandari ya mombasa.
4.     Hoja nyingine ni ya kihistoria,Tangu tupate uhuru watu wa kusini wamesota katika janga la kukosa nishati ya umeme  kwa muda mrefu na hawakuunganishwa na gridi ya taifa kwa sababu lukuki ingawa iliwezekana kuvusha umeme baharini kwenda Zanzibar ilishindikana kuuleta Mtwara.Kama wameweza kusahauliwa kwa miaka 51 katika swala la nishati,hofu ni kuwa gesi itakapoisha vizazi vyao vitasahauliwa tena kwa kubaki na bomba tupu,na hakuna atakayekumbuka tena kuunganisha mikoa hii na Gridi ya Taifa ili kuwa na umeme wa uhakika ambao ndio hitaji kubwa mojawapo la wawekezaji.Hoja ya gesi kuwa nyingi sana na itachukua muda mrefu kuisha  haina mashiko kwani hata dhahabu tuiyokuwa tunajivunia kuwa ni nyingi sana katika mgodi wa Nzega uliokuwa unachimbwa na kampuni ya Resolute umefungwa mwaka jana august,dhahabu imeisha,hivyo hata gesi itaisha tu,tufanye maamuzi ya busara.
5.     Ilani ya chama cha mapinduzi(2010) katika ibara ya 63(h) na (k) ilianisha miradi ya kinyerezi(240MW) na mradi wa Mnazi bay(300MW) kama miradi miwili tofauti inayojitegemea.Hivyo tunashangaa leo inapoonekana kuwa ni mradi mmoja.Tunataka kila mmoja uendelee kama ulivyopangwa na si vinginevyo.Hii ndiyo itawezesha ahadi ya ujenzi wa kiwanda cha UREA kilichopangwa kujengwa Mtwara kama inavyoainishwa katika Ibara ya 49(e) kufanikiwa.Lakini hii pia itawezesha uhakika wa uanzishwaji wa kiwanda cha kubangulia korosho kama makubaliano(Memorandam of understanding) yaliyoingiwa kati ya TIB(80% Tanzania Investiment bank) na Tandahimba Newala Cooperative union(20%TANECU) kukamilika.Nadhani Kuyatekeleza tuliyoahid ndio njia bora ya kutimiza ahadi na kuboresha maisha ya watanzania.
6.     Kwa kuwa kipaumbele cha watu wa Mtwara si kuwa na umeme majumbani ambao ni ongezeko la gharama la maisha kiuchumi(na kwa kuzingatia kuwa nyumba nyingi za mji wa Mtwara hazina sifa ya kuunganishiwa umeme kwani ni za nyasi,udongo na makuti na kipato chao cha sasa kinawanyima uwezo wa kuipa bili za kila mwezi)Kipaumbele kinabaki ni kupunguza makali ya maisha kwa kuwa na uhakika wa kipato kwa njia ya ajira kwa shughuli za uzalishaji viwandani na shughuli zitakazoambatana na hizo,Ni vema serikali ikazingatia kauli ya Mkurugenzi mkuu wa Wentworthy resource Limited Inayochimba gesi ya Mnazi Bay Bwana Bob Mcbean iliyoripotiwa tarehe  6 December  London mwaka 2012 kuwa watapata faida kubwa kwa kuwekeza katika kiwanda cha mbolea na kemikali nyingine,hivyo ni vyema mkazo ukawa katika  kuhimiza uwekezaji zaidi kupitia gesi hii na uhakika wa nishati ya umeme kutokana na mtambo wa kufua umeme utakaojengwa Mtwara.
TUJIFUNZE KWA WENZETU.
Tanzania si nchi ya kwanza kuchimba gesi katika dunia wala Afrika.Katika bara la afrika tunazo nchi kama Algeria,Misri na Nigeria ambazo husafirisha gesi nje ya nchi.Tukiwa nchi ya 66 duniani tukizalisha 658,000,000cubic metres,jirani zetu msumbiji ni wa 50 wakizalisha 3,600,000,000cubic metres(takwimu za mwaka 2012).
Tanzania kwa sasa inasadikika kuwa na kiasi cha 43 Trillion Cubic feet (TCF) ukilinganisha na kiasi cha 2.8Trillioni cubic Metres(98.896Trillion cubic feet) za msumbiji ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango tulichonacho hivyo si vibaya tukijifunza kwao.
Kwa sababu ya mipango mizuri ya kiuchumi ya Msumbiji haikuwa lazima kujenga kila kitu Maputo/beira ambayo ni miji ya biashara lakini mtambo wa kuzalisha gesi ya 107.5MW umejengwa na kampuni ya Aggreko katika mji wa pembeni wa Ressano Garcia utakaopeleka umeme  Maputo na miji mingine ya Afrika kusini ambako katika miji hii umeme huu utasafirishwa  na kutumika kwani ndio miji mikubwa ya kibiashara kama ilivyo Dar Es Salaam .Ingawa umbali wa Maputo na Ressano Garcia ni 1/5 ya umbali wa Dar-Mtwara,tunaweza kujifunza kwao katika hili.
 Akizindua mradi huo mwezi July 2012 Rais wa msumbiji Mh.Armando Guebuza alieleza kuwa wanakusudia kujenga mitambo ya kuweka gesi katika hali ya kimiminika ipatayo 10(liquefied natural gas (LNG) plants) katika maeneo mbalimbali ya msumbiji.Hii yote ni kutawanya uchumi na kutengeneza fursa mbalimbali kwa wananchi wa kawaida wa Msumbiji.Hili nalo linaweza kufanyika Tanzania.
NINI KIFANYIKE?
1.     Kwa sababu bomba hili halisafirishi chakula cha dharura kwamba likisitishwa watu watakufa katika jiji la Dar Es Salaam,Serikali itangaze rasmi kusitishwa kwa mradi huu wa ujenzi wa bomba mara moja kutokana na kilio cha wananchi na izijibu hoja 9 za wananchi zilizotolewa katika maandamano ya tarehe 27 december 2012.
2.     Mkuu wa mkoa na waziri wa nishati na madini wawaombe radhi wananchi wa Mtwara kwa maneno yao ya kuudhi kwa kuita maandamano yao kuwa ni ya kipuuzi,wahaini na wasioelewa ili kuonyesha kuwa walikosea.Wasipofanya hivyo ni kusema walikusudia kuyasema hayo na kwa jinsi hiyo ni kuchochea mikutano na maandamano yanayoendelea,hivyo kwa lolote litakotokea watastahili kuwajibishwa.
3.     Uwekwe mpango maalumu wa viongozi waandamizi wa serikali kuja mtwara na kukutana na wananchi wa mtwara Haraka ndani ya siku 14 zijazo.Nia sio kuwaambia gesi lazima itoke bali ni kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja zao.
4.     Wabunge wa mkoa wa Mtwara na Lindi waache malumbano kati yao bali wajitokeze hadharani na kueleza msimamao wao wa pamoja kuhusiana na jambo hili.
ANGALIZO
Swala la gesi linalenga kuwafaidisha wananchi wote wa Tanzania kama vile sera ya serikali inavyosema.Wananchi wa Mtwara ni sehemu ya Taifa hili nao wanahaki ya kuhoji na kutathmini utekelezwaji wa  yale waliyoahidiwa na viongozi wao.Kuwanyima fursa hiyo ni kuwatenga na utajiri wa Taifa lao.
Ningependa kurudia kwa kusema kuwa,wananchi wa Mtwara hawasemi wananchi wa maeneo mengine ya Tanzania hawapaswi kufaidika na gesi inayozalishwa Mtwara,hoja yao ni kuhusu faida zilizozungumzwa na viongozi hapo kabla kuhusiana na viwanda na umeme.Hili ndilo linalotakiwa kufanyiwa kazi kwa sasa.Ingawa ni kweli kwamba sio serikali inayojenga viwanda hivi lakini ndiyo yenye dhamana ya kufanya hivyo kama ilivyoahidi.
Ikumbukwe kuwa kufanikiwa kwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme Mtwara utatoa mwongozo wa utekelezaji wa miradi kama hii katika maeneo mengine ya Nchi yetu ambako gesi inaendelea kugundulika.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Mtwara,
Mungu Ibariki Gesi Asilia isaidie kuinua maisha ya watanzania Maskini,
Ahsanteni Sana.
JOEL NANAUKA
0713-243 244
                MDAU WA MAENDELEO.
Chanzo:   http://samsasali.blogspot.com/2013/01/mbunge-mtarajiwa-aliyeokoka-aongelea.html
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top