BADO miezi michache kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya
tayari mashirika mbalimbali ya utafiti yameshaanza kubashiri washindi
wa uchaguzi huo utakaofanyika mwezi Machi mwakani watakuwa kina nani.Ni Kawaida kwa mashirika ya utafiti ulimwenguni kote kufanya utafiti hususan kipindi cha karibia na uchaguzi wa nchi husika.
Nchini Kenya Utafiti uliofanywa na Kampuni ya
Synovate umebaini kwamba muungano wa Coalition for Reform and Democracy
(CORD) unaoshirikisha vyama vya ODM, Wiper Democratic Movement na Ford –
Kenya ungeibuka na ushindi endapo uchaguzi mkuu ungefanyika mwezi huu
wa Desemba.
Hata hivyo, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo
uliofanywa kati ya tarehe 6 na 11, ushindi huo haungetambulika kikatiba
kwani mgombea urais wa CORD angepata asilimia 47 dhidi ya asilimia 41 ya
washindani wakuu, Muungano wa Jubilee. Hii ni endapo Waziri Mkuu Raila
Odinga na Naibu wake Uhuru Kenyatta watatawazwa wagombea urais wa
miungano hii huku Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na Mbunge wa Eldoret
Kaskazini William Ruto wakiwa wagombeaji wenza.
Hata hivyo, utafiti huo, uliofanywa na kudhaminiwa
na Kampuni ya Ipsos Synovate, CORD ilipata asilimia 48 dhidi ya
asilimia 38 ya Jubilee iwapo Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi
atateuliwa kupeperusha bendera ya muungano huo. Watu 1,625 wenye umri wa
miaka 18 na zaidi walihojiwa kwa njia ya simu ya mkononi.
Mtafiti Mkuu wa kampuni hiyo Dk Tom Wolf, hata
hivyo alisema kuwa bado kuna maswala mengi ambayo yanaweza kubadili
matokeo hayo, ikizingatiwa kuwa miungano hiyo na vyama tanzu vina muda
wa hadi Februari 11, 2013 kabla ya kuwasilisha orodha kamili ya
watakaogombea nyadhifa mbali mbali kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Vilevile, uteuzi wa mgombea urais wa muungano wa
Jubilee, unaoshirikisha vyama vya TNA, URP na UDF Jumanne ijayo, na
makubaliano ya mwisho kuhusu suala hilo katika CORD jana alisema, huenda
yakabadili mambo.“Matokeo hayo yanaweza kubadilika baada ya
miungano mikuu kufanya teuzi zao za wagombea urais na pale teuzi za
wagombezi wa nyadhifa nyingine zitakapokamilika kabla ya Februari 11
mwaka ujao, “ akaeleza Dk Wolf.
Kumekuwa na hali ya vuta nikuvute katika muungano
huo kuhusu mbinu na utaratibu wa kumteua mgombea urais kati ya Uhuru
Kenyatta na Musalia Mudavadi. Wafuasi wa Uhuru wanapendelea mfumo wa
wajumbe huku wenzao wa UDF wakionekana kuegemea ule mfumo wa mwafaka.
Kulingana na umaarufu wa wawaniaji urais
kibinafsi, Raila anaongoza kwa umaarufu wa asilimia 34 huku akifutwa na
Uhuru kwa asilimia 27, ishara kwamba umaarufu wao umepanda kwa alama
moja tangu mwezi uliopita.Hata hivyo, kutokana na dhana iliyokolea wengi
kwamba Makamu wa Rais na kiongozi wa URP, William Ruto watakuwa
wagombezi wenza, umaarufu wao ulishuka kwa asilimia 5 na 7 huku ule wa
Mudavadi ukishuka kwa asilimia 1. Kalonzo ana asilimia 3 kutoka 8
alioandikisha mwezi wa Novemba. Naye Ruto akiwa na umaarufu wa asilimia 2
kutoka 9 mwezi uliopita.
Chanzo : http://www.mwananchi.co.tz/habari/afrika-mashariki/-/1597272/1645034/-/euf695/-/index.html
Chanzo : http://www.mwananchi.co.tz/habari/afrika-mashariki/-/1597272/1645034/-/euf695/-/index.html
Post a Comment