Social Icons

Loading...

Kiwango Cha Maisha Yako Ya Uchumi Kinapima “Financial IQ” Uliyonayo.

Makala   kwa hisani ya : Albert Sanga,  toka Iringa.
  Mapema mwezi wa saba mwaka huu nilikutana na mzee mmoja msataafu kutoka katika moja ya wilaya za mkoani Iringa. Mzee huyu ambaye ndio kwanza alikuwa ametoka kustaafu kazi yake ya ualimu nilimfahamu kwa njia ya simu kupitia kwa rafiki yangu. Haja ya mzee huyu ilikuwa ni kukutana nami nimsaidie kutafuta gari aina ya Hiace ili anunue. 

Kwa kutumia mawasiliano ya simu nilimuelekeza na hatimaye alifika mahali ninapoishi mjini Iringa mtaa wa Ngome-Kihesa. Mzee huyu alifika nyumbani kwangu akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Cresta GX 100. Katika maongezi mstaafu huyu alinieleza kuwa gari ile (Cresta) ni ya kwake na ameinunua wiki moja iliyopita kwa thamani ya shilingi milioni 10. 

Vile vile akanijuza kuwa amepata mafao yanayofikia shilingi milioni 47 ndipo katika hizo akaona aanze kwanza kujipongeza kwa kununua gari la kutembelea. Ingawa mazungumzo haya hayakuwa sehemu ya shida iliyomleta kwangu (yaani kusaidiwa kununa Hiace) lakini yalinipa funzo kubwa na nikajikuta nayatumia kama msingi wa maamuzi yangu kwa shida iliyomleta kwangu. 

Kwa kifupi ni kwamba mstaafu huyu alishabahatika kujenga nyumba ya kuishi huko kijijini kwao, lakini baada ya kustaafu na kukabidhiwa “mamilioni” akaona kijijini hakumfai. Alichoamua ni kutafuta nyumba ya kuishi maeneo ya mjini na mradi alioona utamsaidia kwa maisha yake baada ya kustaafu ni kufanya biashara za daladala! Angalia mchanganuo wa mafao aliyoyapata na matumizi aliyoyafanya. Gari akanunua milioni 10, nyumba ya mjini akanunua kwa milioni 22.

 Wakati anakuja kwangu kutaka tutafute Hiace alikuwa amebakiwa na shilingi milioni 12 katika akaunti yake. Milioni tatu katika zile 47 alitumia kwa matumizi madogo madogo kama anavyosema mwenyewe. Nikainama kwa muda, nikatafakari na ghafla moyo wangu ukaingiwa na hofu pamoja na huruma. Haraka haraka nikajua kuwa maisha ya mstaafu huyu yatakuwa magumu siku chache zijazo. Nilipotafakari adha ya biashara ya daladala nikaona kama nikimsaidia kununua Hiace anayoitaka nitakuwa nimechangia kummaliza. Nikamshauri mzee huyu kuwa kwa fedha alizobakiwa nazo (milioni 12) hawezi kupata gari nzima, sana sana atapata Hiace banzi (wafanyabiashara wa Iringa tunaziita hiace zilizochoka kwa jina la mabanzi). 

Ili kumuokoa dhidi ya msiba unaomsubiri nikatumia muda mwingi kueleza matatizo yaliyopo katika biashara ya daladala huku nikimshauri aachane na wazo hilo mfu. Nikampa neno hili la mwisho, “Kwa kuwa umeshatumia fedha nyingi kununua nyumba na gari ambavyo vyote havizalishi fedha, usiingie tena kwenye mradi ambao hauna uhakika mzuri wa kuzalisha fedha. 

Nakushauri ufikirie kilimo na ufugaji”. Pamoja na juhudi zangu hizo za kufafanua hayo lakini aliendelea kusisitiza nimsaidie kutafuta Hiace! Nikaona isiwe tabu, ndipo nikamwambia kwa fedha aliyonayo sitaweza kumtafutia gari na sitaki kumtafutia gari halafu kesho na keshokutwa likisumbua aje aseme kijana Sanga alinitia umasikini.

 Tutaachana, akaenda zake. Baada ya wiki moja nikapokea taarifa kuwa mzee yule alifanikiwa kupata na akanunua Hiace kwa milioni 8! Ninapoandika makala hii ni miezi miwili tu imepita tangu mzee Yule aliponunua Hiace ile lakini imeshaua injini na imepaki nje ya nyumba aliyonunua. Huhitaji kuwa mtabiri kubaini kuwa maisha ya mstaafu huyu yatakuwa ni magumu na ya taabu hadi kufa kwake. Yaliyompata mstaafu huyu yanawapata wastaafu wengi, yanawakumbuka watanzania wengi kuanzia wasomi na wasio soma, walioajiriwa na wasioajiriwa, wafanyabiashara, wanasiasa na wananchi wa kawaida. Wengi hawana akili ya fedha.

 Hawajui wapataje fedha, hawajui wakishapata fedha waziongezaje na hawajui wazitumiaje wakiwa nazo. Huu uwezo wa kutafuta, kuongeza na kutumia fedha ndio ninaouita “Financial IQ”. Huko nyuma kupitia gazeti hili nimewahi Kuandika makala iliyokuwa na maudhui kuwa wafanyakazi (hasa walimu na madaktari) hawahitaji kuongezewa mishahara. Licha ya kwamba maudhui yale yalipokelewa kwa hisia tofauti lakini maana yangu ilikuwa na picha kubwa.

 Hata kama ukiongezewa mshahara ukawa mkubwa kiasi gani kama huna akili ya kuutumia vema mshahara unaolipwa hutafika popote kimaendeleo. Watu wawili wanaweza kuwa katika kazi moja, wakawa wanalipwa mshahara mmoja na wakawa na majukumu sawa, lakini mmoja akawa na maendeleo makubwa kuliko mwingine. Mara nyingi mtu asipojipa muda wa kufanya ulinganisho huo; ni rahisi sana kuhamishia uduni wa maisha yake kwa wengine; hasa hasa serikali! 

Kiwango cha “Financial IQ” kinapimwa kwa kuangalia unatumiaje unachokipata kuzalisha vingi. Katika hili kila fedha inayopita katika mikono yako inatakiwa kuchukuliwa kama mbegu. Kama ninalipwa shilingi laki tano kwa mwezi halafu nikatumia laki tano yote katika matumizi yasiyo zalisha (kama pango, chakula na mavazi) basi “Financial IQ” yangu inahesabika kuwa ni sifuri! Lakini pengine kuna mfanyakazi mwenzangu anayelipwa hiyo hiyo laki tano halafu kila mwezi akawa anatenga shilingi elfu hamsini unapoisha mwaka atakuwa na shilingi laki sita.

 Tuchukulie imepatikana fursa sehemu kuwa kuna kiwanja kinauzwa laki sita; moja kwa moja mfanyakazi mwenzangu atakuwa na nafasi ya kununua kile kiwanja. Kwa kuwa ardhi inapanda thamani, kila siku kiwanja alichonunua kitakuwa kinapanda thamani hivyo utajiri wake utakuwa unapanda nafasi wakati mimi nitakuwa pale pele ama nitakuwa ninashuka kwa sababu sina uwezo wa kutumia fedha ninayopata kuzalisha fedha nyingine. 

Unaweza kujiuliza “Nitajuaje ikiwa nina financial IQ, na kwa kiwango gani?”. Jibu ni rahisi. Kiwango cha maisha yako ya uchumi kinapima “financial IQ” uliyonayo. Kama unaishi maisha ya uhaba na “kuunga-unga” katika eneo la fedha basi ujue una “financial IQ” ndogo. Kama unaishi maisha yenye viwango vya juu kiuchumi basi ujue una financial IQ kubwa. 

Ni vema nikaeleweka kuwa hapa siongelei kiwango cha fedha ama mali unazomiliki, la hasha! Ila naongelea mfumo wa fikra zako katika kupata, kuongeza na kutumia fedha. Kwa lugha rahisi ni kuwa kuna watu wa aina mbili. Kundi la kwanza ni wale wanaopata fedha na kuzitumia “zooote”. Kundi la pili ni wale ambao kila wapatapo fedha hufikiria namna bora ya kuzizalisha ziongezeke kabla ya kuzitumia. 

Kundi la pili wana “financial IQ” kubwa wakati kundi la kwanza wana “financial” IQ ndogo. Ili ukuze “Financial IQ” yako kuna mambo unahitaji kujifunza na kuyazoea. La kwanza ni imani yako kuhusu fedha. Kila mtu anamiliki kiwango cha fedha sawa sawa na imani yake kuhusu fedha. Kuna watu wanaamini kuwa mtu mwenye fedha nyingi (tajiri) hawezi kumpendeza Mungu na wala hawezi kuingia mbinguni. Kwa kuwa wanaipenda Mbingu na kwa kuwa kwao umasikini ndio utakatifu, basi hubaki kuwa na uhaba wa kifedha. Kuna watu wameunganisha fedha na imani za ushirikina.

 Hawa wanaamini kuwa matajiri wengi (kama sio wote) wanatumia ushirikina katika biashara zao. Mtu wa hivi hawezi kuwa na fedha za kutosha kwa sababu katika fikra zake ameunganisha fedha na ushirikina-na kwa kuwa hapendi kuwa mshirikina basi anabaki kuwa masikini! Wafanyakazi wengi (pengine kutokana na mishahara isiyotosha) huamini kuwa mfanyakazi hawezi kujenga nyumba ama kununua gari isipokuwa awe amefanya ufisadi kazini kwake. Ukiunganisha maendeleo na wizi katika fikra zako hutaendelea na wala hutakuwa tayari kujifunza kutoka kwa walioendelea. 

Kwa wale wanaofuatilia makala zangu nimewahi kuchambua imani hizi kwa kina huko nyuma katika makala iliyokuwa na kichwa “Huhitaji fedha kuzalisha fedha” Jambo jingine litakalokuongezea “Financial IQ” ni nidhamu yako ya kujiwekea akiba. Kabila la Wakinga tuna mila moja imara sana kuhusu uwekaji akiba. Mkinga huwa kuna akiba anaweka ambayo hawezi kuitumia hata kama anakufa na njaa. 

Akiba hii iitwayo “Ekhefumbato” hutakiwa kutumika pale tu inapopatikana akiba nyingine ya kubadilisha na ni lazima itumike kwa kusudi la msingi. Bahati mbaya watanzania wengi hatuna utamaduni wa kujiwekea na kuheshimu akiba zetu. Ukiweka akiba benki ambayo labda umepanga ni kwa ajili ya kusomeshea watoto, halafu unakutana na tatizo la kufiwa na unaenda kuichukua ujue bado nidhamu yako ya kujiwekea akiba ni ndogo na “Financial IQ” yako iko chini. Kwa haraka haraka nigusie jambo la mwisho litakalokusaidia kuongeza “Financial IQ” yako. Hili ni nidhamu ya matumizi. 

Unapopata fedha, Je, ni vipaumbele gani unaviweka katika maisha yako? Je, vipaumbele vyako vina tija gani katika kuboresha uchumi wako sasa na baadae? Je, vitu unavyonunua vina umuhimu sawa na umuhimu unaovipa? Huenda umeamua kuchukua mkopo benki kwa dhamana ya mshahara wako na ukaamua kununua gari la kutembelea. Je, gari la kutembelea lina umuhimu “halisi” kwako? Au umeamua kununua ili na wewe uonekane kuwa umo kati ya wanaomiliki magari? 

Hata kama umenunua hilo gari, hamna shida! Lakini, Je, una kipato kinachokidhi gharama za uendeshaji wa gari ikiwemo mafuta na vipuri? Kuna kitu tunatakiwa kuwa nacho makini hapa kwa sababu wapo watu ambao licha ya kuwa na mishahara ya kawaida, bado wanakopa mikopo na kununua magari yanayotumia mafuta mengi kwa ufahari tu. 

Ni kawaida kuona mtu ana gari la kutembelea la kifahari lakini anahangaika hata hela ya mafuta. Tabu yote ya nini? Kwa mtu mwenye “Financial IQ” kubwa ataanza kutengeneza vitega uchumi kwa kutumia mshahara ama mkopo kabla ya kufikiria kununua vitu vya starehe kama gari la kutembelea. Nihitimishe kuhusu kisa cha yule mzee mstaafu. 

Kama mstaafu Yule angalinifuata akiwa na milioni 47 zote pengine ningemshauuri tofauti. Nisingemwambia kununua nyumba mjini badala yake ningemwambia akae zake kule kule kijijini alikojenga afuge na kulima. 

Kama anatamani gari la kutembelea ningemsaidia kutafuta “Pick-up” ambayo akitaka kwenda harusini anaenda nayo na akitaka kufanyia shughuli za shamba inafanya. Bahati nzuri “Financial IQ” mtu huzaliwi nayo isipokuwa unajifunza kwa kuwa na mtazamo na maamuzi sahihi kuhusu fedha. Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi. Wasalaam!.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top