Social Icons

Loading...

MTIKILA Ashinda kesi ya Uchochezi

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameshinda kesi iliyofunguliwa na serikali, akidaiwa kuchapisha na kumiliki waraka wa uchochezi unaomkashifu Rais Jakaya Kikwete.
Hukumu ya kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi nchini, ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Elvin Mugeta.
Katika kesi hiyo ya jinai iliyofunguliwa mwaka 2010, Hakimu Mgeta alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.
Mchungaji alikuwa akikabiliwa na makosa mawili.
La kwanza ni kuchapisha kusambaza waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1),(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002 na kosa la pili ni la kumiliki waraka huo kinyume na kifungu cha 32(2) cha sheria hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mugeta alisema Mtikila katika utetezi wake alikiri kuandaa na kuumiliki waraka huo uliotolewa mahakamani hapo kama kielezo cha tatu na jumla ya mashahidi wanne waliletwa na upande wa serikali.
Alisema wakati serikali ikileta mashahidi hao, Mchungaji Mtikila hakuleta shahidi hata mmoja na badala yake alijitetea mwenyewe kwa madai kuwa hakuona sababu ya kuwaleta mashahidi kwani kufanya hivyo ni kumaliza fedha na kupoteza muda wa mahakama.
Hakimu Mugeta alisema kabla ya kutoa hukumu hiyo, alijiuliza maswali kuwa je, ni kweli waraka huo ni wa uchochezi? Je, waraka huo ulileta madhara katika jamii? Je, waraka huo ulikuwa ukitaka kumpindua Rais Kikwete kinyume na sheria za nchi?
“Mimi nimeusoma waraka huo unaodaiwa na upande wa jamhuri kuwa ni uchochezi na nimebaini kuwa si wa uchochezi kwani Mtikila ni mwanasiasa, pia ni kiongozi wa dini na waraka ule ulikuwa umejaa maneno ya kidini ambayo ndani yake Mtikila alikuwa akiwataka Wakristo wenzake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watumie haki yao ya msingi ya kumpigia kura mgombea ambaye ni Mkristo.
“Na kumng’oa madarakani Rais Kikwete kwa njia ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu si kosa la jinai.
“Mahakama hii kwa kauli moja imeona upande wa jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha Mtikila alikuwa anataka Wakristo wamuondoe Rais Kikwete Ikulu kwa njia haramu.
“Pia upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kwamba kusambazwa kwa waraka huo kulileta madhara, na wameshindwa kuleta ushahidi unaoonyesha waumini wa dini ya Kikristo walishawishika na waraka huo na wakajaribu kumuondoa Rais Kikwete madarakani kwa njia haramu,” alisema Hakimu Mugeta.
Alisema mshtakiwa angeweza kukutwa na hatia kama ingethibitika kuwa alikuwa akitumia karata ya dini kuligawa taifa na kuongeza kuwa mahakama hiyo imejiridhisha kuwa waraka huo haukuibua chuki baina ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo na kwa sababu hiyo mahakama imemuona Mchungaji Mtikila hajatenda kosa la uchochezi.
Hakimu Mugeta alisisitiza kuwa hakuna madhara yaliyojitokeza katika taifa kupitia waraka huo na kwa sababu hiyo mahakama yake inamwachilia huru Mchungaji Mtikila.
Baada ya kuachiwa huru, Mtikila alisimama kizimbani na kupaza sauti akisema: “Haleluya, Haleyula… Kesi hii ni ya Mungu na hakuna binadamu yeyote anayeweza kushindana na Mungu.”
Aidha aliwataka Watanzania wakasome Bibilia, Waraka wa Pili wa Timotheo sura 4:2 ambao unasema: “Fanya kazi yako wewe mhubiri wa Injili; onya, karipia na kemea dhambi.”
Mtikila akasema alichokifanya katika waraka ule ni kukemea dhambi na kutangaza neno la Mungu, lakini cha kushangaza serikali ikamfungulia kesi hiyo.
Hii ni kesi ya 43 ya jinai katika zile ambazo Mchungaji Mtikila ameshafunguliwa na serikali tangu aanze kile anachokiita harakati za ukombizi wa Mtanganyika.
Kati ya kesi hizo, serikali ilishinda na kumfunga jela kwa kesi moja tu ya kutoa maneno ya uchochezi ambapo alisema Chama cha Mapinduzi (CCM), kilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba.
Kabla ya hukumu ya jana, Mtikila aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama kuwa angeibuka mshindi dhidi ya serikali katika kesi hiyo.
Hata hivyo wakati Mtikila akiendelea kushangilia ushindi, ghafla aliibuka mtu aliyejitambulisha kuwa mfanyabiashara, Gotem Ndunguru, akiwaamrisha askari wamkamate Mchungaji Mtikila kwa madai kuwa alikuwa na amri ya kumkamata iliyotolewa na Kituo cha Polisi cha Kimara, namba RB/10482/12 ambapo alidai Mtikila alimtishia kumuua kwa maneno.
Askari walishindwa kumkamata Mtikila kwa sababu alianza kumfokea askari mmoja wa cheo cha chini, akimwambia kwa ukali kwamba hana hadhi ya kumkamata kwani yeye ana hadhi ya kukamatwa na mwenye cheo cha mrakibu wa polisi.
“We askari, nani kakuhonga uje unifanyie fujo hapa? Kwa taarifa yako mimi najua sheria, wewe huna mamlaka ya kunikamata na huwezi kunikamata kihuni hivi… hata huyo bosi wako IGP Saidi Mwema kabla ya kunikamata ananipigia simu kwa adabu na mimi mwenyewe ndiye naenda polisi… sasa nakuambia hivi huna hadhi ya kunikamata,” alifoka Mtikila na kusababisha askari huyo kunywea.
Chanzo  kwa  hisani  ya http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=40916 
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top