Marehemu John Evans Atta Mills |
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
atakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi 16 na wageni wengine wengi maarufu,
akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mheshimiwa Hillary Clinton,
kushiriki mazishi ya aliyekuwa Rais wa Ghana, Mheshimiwa John Evans
Atta Mills kesho , Ijumaa, Agosti 10, 2012, mjini Accra.
Rais
Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kuwasili mjini Accra, mji mkuu wa
Ghana, adhuhuri ya leo, Alhamisi, Agosti 9, 2012, kuhudhuria mazishi ya
kiongozi huyo aliyefariki dunia mchana wa Jumanne, Julai 24, 2012 kwa
ugonjwa wa kansa ya koo kwenye Hospitali ya kijeshi inayoitwa 37
Military Hospital mjini Accra.
Rais
Mills ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 69 anatarajiwa
kuzikwa kwenye makaburi yaliyoko eneo la bustani la Geese kwenye Mtaa wa
Castle Drive karibu na Hekalu ya Osu mjini Accra baada ya kuwa mwili
wake umeagwa kwenye shughuli maalum itakayofanyika kwenye bustani ya
Independence Square kesho Ijumaa.
Rais
Mills ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais John Dramani Makama
atazikwa katika kaburi lililojengwa na kampuni ya ujenzi ya Serikali ya
China ya HL Construction. Mwili utazikwa baada ya kupitishwa katika
mitaa maarufu ya jiji la Accra ili kutoa nafasi ya mwisho kwa wananchi
wa Ghana kuuona na kuuaga mwili huo kwa mara ya mwisho.
Jana,
Jumatano, Agosti 8, 2012, mwili wa Mheshimiwa Mills ulihamishwa kutoka
kwenye Hospitali ya 37 ya Jeshi la Ghana ambako umekuwa umehifadhiwa
tokea kufariki dunia na kupelekwa kwenye nyumba ya familia iliyoko
katika Barabara ya Spintex kwa ajili ya kufanyiwa taratibu za mila.
Baada
ya shughuli hiyo, mwili wa Mheshimiwa Mills ulihamishiwa kwenye jumba
la kulia la Ikulu ya Ghana ambako wananchi wamekuwa wanatoa salamu zao
za mwisho kwa mwili wa kiongozi wao. Mwili wa Rais Mills utabakia
katika sehemu hiyo mpaka utakapohamishiwa Independence Square kwa ajili
ya shughuli ya mazishi.
Miongoni
mwa watu waliotoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Rais leo ni
pamoja na Rais John Kuffor ambaye Rais Mills alichukua madaraka kutoka
kwake. Vikundi vya muziki na vikundi vya utamaduni viliendelea
kutumbukiza Ikulu siku nzima jana na usiku kucha.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
8 Agosti, 2012
Post a Comment