Rais Jakaya Kikwete amekemea vikali vurugu zilizotokea jana
mkoani Mtwara baada ya kusomwa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati
na Madini.
Akizungumza katika eneo la Kizota, Dodoma wakati
wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Dodoma kwenda Iringa,
Rais Kikwete alisema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na
kuchukuliwa hatua kali.
Rais Kikwete alisema rasilimali inayopatikana
mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote... “Hivi
watu wa Nyarugusu wadai dhahabu ya pale au kinachopatikana Chalinze
basi kisitumiwe na watu wa Morogoro! Hivi tutakuwa na taifa kweli?,”
alihoji kwa ukali Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa Serikali itawasaka
wale wote wanaoongoza vurugu hizo na watawajibishwa kwa makosa hayo...
“Tutawasaka hawa watu na viongozi wao hata kama wana mapembe kiasi gani,
tutayakata.”
Alichosema Waziri Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo amesema mradi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda
Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda
huko wiki ijayo kuweka jiwe la msingi.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini jana, Waziri Muhongo alisema:
“Mradi wa kujenga bomba la gesi uko palepale na
unaendelea kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ataenda kuweka jiwe la
msingi wiki lijalo.”
“Tumezungumza mengi kuhusu suala hilo na hata
viongozi wa watu wa Mtwara walipelekwa nje kujifunza faida zake, lakini
hata kama hawajaelewa, nimetoa kijitabu kinachozungumzia faida
mbalimbali watakazopata wana Mtwara katika mradi huo.”
Profesa aliyeanza hotuba yake kwa kueleza
machapisho mbalimbali yaliyotolewa na wizara yake kufafanua faida za
gesi ya Mtwara kwa taifa, alisema mradi huo uliozinduliwa Novemba mwaka
jana na Rais Kikwete, unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa
532 na kipenyo cha nchi 36.
“Bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za
ujazo za gesi milioni 784 kwa siku. Mradi utahusisha mitambo miwili ya
kusafirisha gesi asilia katika maeneo ya Mnazi Bay- Madimba (Mtwara) na
Kisiwa cha Songosongo (Lindi). Utagharimu Dola za Marekani 1,225.3
milioni,” alisema.
Alisema kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia
kwa wananchi wapatao 3,092 waliopisha maeneo ya mradi, zimekamilika na
hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asilia zimeanza.
Post a Comment