Jiji moja nchini Indonesia ambalo
limekuwa likifuata sheria za kiislamu maarufu kama sharia, liko mbioni
kupitisha sheria ya kuwapiga marufuku wanawake kukaa kiume kwenye
pikipiki, zenye kuendeshwa na wanaume, kwa madai kuwa mkao huo
huwaondolea uthamani wao
Suaidi Yahya, ambaye ni meya wa jiji
hilo la Lhokseumawe, ameeleza kuwa, mpango huo umelenga katika kutunza
mila na desturi za watu na tayari vipeperushi kwa ajili ya kusambaza
taarifa juu ya kusudio la mpango huo, vimeshaanza kusambazwa mitaani.
Chini ya sheria mpya, meya huyo anasema
kuwa, wanawake wataruhusiwa tu kupanda pikipiki wakiwa wamekaa kiupande
upande (kike), kwakuwa kukaa kiume ni ukiukwaji wa sheria za kiislamu.
“Ukimuona mwanamke amekaa kiume kwenye
pikipiki, anaonekana kama mwanaume tu, lakini akikaa kike, anaonekana
kama mwanamke kweli” amesema meya huyo na kuongeza pia kuwa, watu wenye
kupanda pikipiki na kukaa mkao wa kike, pia hawapati ajali za kuanguka
kwa urahisi.
Mamlaka za mji huo, zinatarajiwa kuanza
kufanya mapitio ya muswada huo katika muda wa mwezi mmoja na ikiwa
wataridhia basi utapitishwa na kuwa sheria ndogo ya jiji hilo.
Alipoulizwa ikiwa wanawake ambao
hawatatimiza sharti hilo watachukuliwa hatua, meya huyo alijibu “ndio,
mara tu itakapopitishwa na kuwa sheria rasmi, hakika kutakuwa na adhabu
itayotolewa”
Hata hivyo, muswada huu, umekutana na
vipingamizi toka kwa watu mbalimbali akiwemo mwanaharakati wa masuala ya
kiislamu, Ulil Abshar Abdalla, mwenye makazi yake kwenye mji mkuu wa
Indonesia wa Jakarta.
“Uendeshaji au upakiaji wa pikipiki
haujawekewa kanuni katika quran tukufu wala kwenye hadith za kiislamu
ambazo ndio chimbuko la maelekezo yetu” amesema mwanaharakati huyo
Post a Comment