Serikali, mashirika binafsi na wadau wa usafiri ndani na nje ya
nchi wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na msongamano wa
magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Msongamano huo ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa
na uduni wa miundombinu ikiwemo barabara, umekuwa ni kero kwa wananchi
na Serikali kwa jumla.
Serikali imewekeza katika Mradi wa Mabasi Yaendayo
Kasi (BRT) na usafiri wa treni ndani ya Jiji la Dar es Salaam kama njia
mojawapo ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari na foleni.
Msingi wa tatizo
Chanzo kikubwa cha foleni jijini Dar es Salaam si
wingi wa abiria bali ni wingi wa magari binafsi na njia finyu
zisizokidhi mahitaji ya watu walioko katika jiji hilo.
Njia muhimu ya kupunguza foleni na msongamano wa
magari ni kupunguza wingi wa magari barabarani na kuweza kuzipanua
barabara ili kuwe na uwezekano wa kupita kwa urahisi.
Kutokana na foleni na uduni wa huduma za usafiri
wa umma watu wa kundi la kati, wamekuwa wakikimbilia kununua magari
binafsi kwa ajili ya kwenda nayo kwenye shughuli zao kwa urahisi.
Aidha, katika kuendeleza harakati za kupambana na
tatizo la usafiri, Kampuni ya Transevents Marketing ya Tanzania kwa
kushirikana na Kampuni ya Dutch Amphibious Transport Vehicles (DATV) ya
Uholanzi inaendelea na mchakato wa kuleta usafiri wa mabasi ya abiria
yenye uwezo wa kusafiri nchi kavu na majini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Transevents, Peter Nzunda
anasema teknolojia hiyo ya mabasi ya nchi kavu na majini (amphibious)
ina lengo la kupunguza tatizo la foleni kwenye barabara za Dar es Salaam
hususan katikati ya jiji kwa kuwa mabasi hayo huweza kupita nchi kavu
na majini.
Hii ina maana kuwa hata katika maeneo yenye
barabara zisizo nzuri au zenye tope, magari hayo huweza kupita hivyo
kutosababisha foleni kama ambavyo hutokea sasa katika baadhi ya maeneo
hasa mvua zinaponyesha na kuharibu barabara.
kwa hisani ya gazeti la mwananchi
kwa hisani ya gazeti la mwananchi
Post a Comment