Social Icons

Loading...

UPINZANI WATAKA JK ASISAINI MUSWADA

Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita “utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi” hivyo wanaitaka Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.
Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona ila aurejeshe bungeni,”alisema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala yake  unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa Katiba katika msingi wa maridhiano.
Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
 Chanzo  kutoka  gazeti  la  mwananchi.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top