Itakumbukwa
tarehe 16/06/2013 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa
baadhi ya kata nchini. Uchaguzi huo umefanyika kwenye kata ishirini na
mbili (22) kati ya kata ishirini na sita (26) zilizotangazwa kufanya
uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi wazi.
Matokeo
tuliyoyapata toka kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi yanaonyesha kuwa
kati ya kata 22 zilizofanya uchaguzi CCM tumeshinda kata 16 sawa na
asilimia 72.72% na wenzetu wamechukua kata 6 zilizobaki sawa na asilimia
27.28%.
Tunawashukuru
sana kote walikoonyesha imani yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa
dhamana ya kuendelea kuwatumikia. CCM inawaahidi utumishi uliotukuka.
Hata wale 27.28% walioamua kuwajaribu wenzetu, tunawatakia kila lakheri,
kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua wanaodhani
watawasaidia kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Uchaguzi kwenye kata
hizi zote umeisha sasa tuwatumikie wananchi.
Kata nne za jiji la Arusha hazikufanya uchaguzi baada ya kuahirishwa
kufuatia tukio la kusikitisha la kulipuka kwa bomu kwenye mkutano wa
kampeni wa Chadema mjini Arusha tarehe 15/06/2013.
CCM tunalaani
tukio hilo la mlipuko wa bomu na matukio yanayofanana na hayo katika
nchi yetu. Tunawapa pole wale wote walioathirika na tukio hilo. Ni
vizuri serikali ikalichunguza swala hili kwa kutumia muda mfupi na
kuhakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pamoja na
kulaani na kuitaka serikali kukomesha vitendo hivi nchini, ni wakati
muafaka kwa vyama vya siasa nchini kujitazama upya kwani kuna kila
dalili kuwa tukio hili kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya
habari mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema Taifa kuwa ni la kupangwa,
inawezekana limepangwa na Chadema wenyewe.
Hali ya kisiasa jijini Arusha kuelekea uchaguzi huo ilikuwa wazi kuwa
wana Arusha walishaamua kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM, hasa baada ya
kuchoshwa na maandamano na vurugu za kila siku jijini Arusha. Aidha
kauli za kukata tamaa za viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili
tosha kuwa tukio hili lilipangwa na Chadema wenyewe.
CCM
tunaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za wenzetu kujaribu kujenga
umaarufu wa chama chao juu ya damu za Watanzania. Juhudi hizi zinapaswa
kulaaniwa na wazalendo wote ndani na nje ya nchi. Tukumbuke asiyekubali
kushindwa, si mshindani. Si busara wala uungwana na ni kinyume na utu
kutumia majanga ya kutengeneza kama mtaji wa kisiasa.
Lakini CCM tunalaani pia kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu
kutumia baadhi ya misiba na majeruhi wa tukio hili kisiasa na mwisho wa
siku kwenda kuwatelekeza hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi kubeba
gharama zote za matibabu na mazishi.Tunaipongeza serikali kwa kuingilia
kati na kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha wanapata huduma
inayostahili.
CCM inarudia
kueleza masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la kinyama na
kikatili lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. Kama Chama tumeguswa sana
na tukio hili pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania tushindane na
kutofautiana bila kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya amani na
utulivu. Katika demokrasia ya vyama vingi swala la kuvumiliana ni swala
la msingi sana katika kufikia ukomavu wa demokrasia hiyo.
Imetolewa;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi.
17/06/2013
Post a Comment