Social Icons

Loading...

Mhariri wa NIPASHE : Haikubaliki kuligeuza Bunge kibogoyo

Katika mkutano wa 10 unaoendelea mjini Dodoma tangu wiki iliyopita, umma umepigwa na butwaa kuingiwa na fazaa kubwa kutokana na mwenendo wa mambo ndani ya chombo hicho kikubwa na muhimu cha uwakilishi wa wananchi chenye wajibu wa kutunga sheria na kuisimamia serikali.
  Fazaa hii siyo ya bure ila ni kutokana ukweli kwamba ama kumekuwa na mbinu za kufanya chombo hicho kisitekeleze wajibu wake kupitia mbunge mmoja mmoja kwa sababu moja tu, ushabiki wa kisiasa ambao hauna tija. Huu ni ushabiki ambao tunathubutu kusema wazi kuwa unadimimiza siyo demokrasia tu bali pia umejikita kuilinda serikali isiwajibishwe ndani ya chombo hicho muhimu.

Wakati mkutano huu ukianza mjini Dodoma Jumanne Januari 29, mwaka huu, yaani wiki iliyopita, tulimkumbusha Spika wa Bunge kuwa ana mzigo wa viporo vya kazi ambazo ama alizitaka mwenyewe ziwasilishwe kwake kwa maamuzi, au wabunge walizipeleka kwake kwa maamuzi kutokana ama mambo kutokwenda sawa au kumtakiwa atoe maelekezo yake. Viporo hivi ni vingi na vipo tangu Bunge hili linaanza kazi mwaka 2011.
  Tulimkumbusha Spika juu viporo hivyo ili kuvitolea uamuzi, nia ikiwa ni kumkumbusha tu ili kwa kukaa kimya juu yake watu wasijekuanza kuhoji juu uimara wa kiti chake, uadilifu wa kuendesha shughuli za Bunge na utendaji wa haki kwa wabunge wote pasi na itikadi zao kwa kuwa wote wamechaguliwa na wananchi na wanatokana na mfumo halali wa kisiasa ambao taifa hili limeamua kufuata.
Tunajua mkutano wa sasa utaahirishwa Ijumaa hii, yaani keshokutwa, na inavyoelekea ni vigumu kwa maamuzi ya viporo vyote kutolewa maamuzi, lakini wakati viporo hivyo vikisumbua vichwa vya wananchi wengi huku wakihoji juu ya mwenendo mzima wa Bunge letu, mkutano huu umeshuhudia tena mambo ya aibu kubwa yakifanyika.
Ijumaa iliyopita, Jumatatu na jana, wabunge wamesema wazi mbele ya Spika kwamba kiti chake kinayumba, hakitendei haki kambi ya upinzani, kanuni za Bunge zinapindishwa ili tu kupotosha mambo, kuilinda serikali isiwajibishwe hali ambayo ni sawa na kusema kupora wajibu wa kibunge wa kuisimamia serikali.
Sakata la sasa lilianza na hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, juu ya uadilifu wa sekta ya elimu ambayo ilikuwa nzito, yenye maana na ambayo kwa kweli ilikuwa inalenga kutafuta uwajibikaji ndani ya serikali juu ya mustakabali wa elimu ya taifa hili.
Kisha ikafuata ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ambayo ililenga pia kutafuta uwajibikaji serikalini katika suala zima la upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika jiji la Dar es Salaam, huku mabilioni ya fedha yaliwa yemetumika bila kuwako kwa huduma yoyote ya maana ya maji, lakini pia ipo ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, ambayo ilitaka kujielekeza kwenye suala la utendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani. Kwa bahati mbaya sana hoja hii haikuwasilishwa kabisa, ni kama ikienguliwa juu kwa juu.

Kiti cha Spika katika sakata lote hili kinayooshewa kidole kwamba kimeshindwa kusimamia haki, kwamba kimeyumba kiasi cha kuegemea upande mmoja; ni hatari kubwa inapofikia hatua ya wabunge kwa ujasiri mkubwa wanathubutu kutuhumu kiti kuyumba kiasi cha kusababisha kukosekana kwa maelewano ndani ya Bunge.
Ni hatari kweli kweli!
Kwa wale walioangalia Bunge Jumatatu jioni watashuhudia walichokiona kwamba siyo taswira njema kwa taifa linalojitapa kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia na kuheshimu kanuni, miiko na maadili yanaokubalika kijamii na kitaifa.
Kwa bahati mbaya sana tangu kuanza kwa Bunge la sasa mwaka 2010 kufuatia uchaguzi mkuu wa 2010, kumekuwa na hisia kwamba uimara wa kiti cha Spika umetiliwa shaka kubwa hasa katika suala zima la kutenda haki sawia kwa wabunge wote bila kujali wanatokana na chama gani cha siasa wanapowasilisha hoja zao.
Tunachukua wasaa huu kuweka wazi kwamba kama Bunge likigeuzwa kuwa sehemu ya muhimili wa utawala ama kwa dhahiri au hata kwa mlango wa nyuma ni wazi hakuna tena haja ya kuwako kwa chombo hicho, ni kwa maana hii tunamshauri Spika awe mvumilivu na asimame kidete kuhakikisha kwamba muhimili anaousimamia unatekeleza wajibu wake mkuu wa kikatiba kulingana na ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania wa kuisimamia na kuishari serikali ili iwajibike ipasavyo kwa wananchi wake. Yanayoendelea mjini Dodoma kwa sasa hakika ni juhudi za kutaka serikali ilale na kukoroma na wabunge waangalie tu. Hii haikubaliki na haitakubalika asilani.

CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top