BAADHI ya masuala ambayo nimekuwa nikiyajadili yanajitokeza hivi sasa kwa mshindo mkuu.Nimekuwa nikisema kwamba tunajitahidi mno kujenga taifa dogo ndani
ya nchi kubwa. Hili linadhihirika sasa. Nimekuwa nikisema pia kwamba
tunaonekana kuwa na haraka ya kufanya mambo kama vile tunakwenda
kwingine, hapa si kwetu na wala hatujafika. Hili nalo linajionyesha.
Hivi sasa tumetekwa na kelele zinazopigwa kuhusu gesi asilia
inayochimbwa kusini mwa Tanzania, na tayari tumeanza kuona dalili za
nchi kuparaganyika kutokana na ‘utajiri’ huo.Tunachokishuhudia si mjadala wa jinsi gani tunaweza kunufaika kama
taifa kutokana na gesi inayochimbwa nchini ( na pia utajiri mwingine
unaotokana na rasilimali za nchi) bali ni ghadhabu za makundi hasimu
yanayokinzana kuhusu namna ya kugawana kidogo tulicho nacho.
Kwa muda sasa, wataalamu duniani wamekuwa wakijadili kile kinachoitwa
‘resource curse’, au laana ya rasilimali. Hii ni laana ya nchi kama
yetu ambazo zinajikuta zikiwa na rasilimali kubwa, lakini badala ya
rasilimali hizo kuzinufaisha nchi hizo inageuka kuwa ni balaa, laaana.
Hili ndilo linaelekea kutokea hapa nchini.Bado hatujui kwa uhakika ni kiasi gani cha gesi asilia tulicho
nacho. Nimesoma mahali kadhaa kwamba gesi hii ni nyingi mno na inaweza
ikaifanya Tanzania kuwa mojawapo ya nchi zenye machimbo ya gesi makubwa
duniani. Bila shaka hilo lingekuwa jambo jema kwa nchi inayoendeshwa
kwa utaratibu unaoeleweka na inayojadili masuala muhimu kwa uwazi wa
kutosha.
Kwa bahati mbaya, hii si kweli. Tumekuwa tukishuhudia usiri
unaogubika mikataba juu ya rasilimali nyingine kwa muda mrefu sasa, na
hakuna dalili kwamba tutaanza kesho au keshokutwa kuwa wawazi zaidi.Hadi leo serikali inakataa kuanika hadharani maudhui ya mikataba
inayoingia kwa niaba ya Watanzania, na serikali ikiulizwa inajibu
kwamba mikataba hiyo ni siri baina ya serikali na ‘ wawekezaji.’
Post a Comment