WAZIRI Samuel Sitta |
Sitta alisema hayo jana mjini hapa katika mahafali ya 11 ya Shule ya Msingi Kwema yaliyoenda sambamba na uzinduzi wa Shule ya Sekondari Kwema. Alisema watu waliojitokeza kugombea ni mapandikizi na vibaraka wa mafisadi hao. "Hivi karibuni tumepata aibu kubwa ndani ya chama chetu, wakati chaguzi zetu zikiendelea viongozi wamepitisha vipaza sauti vya mafisadi, kazi yao kubwa ni kulinda masilahi ya mabwana zao na kuwafurahisha," alisema na kuongeza: "Wameajiriwa kwa lengo la kupiga kelele, kupiga vijembe, kuwapamba wafalme wao ambao wamefanikisha kuwa wanapata madaraka hayo, lakini kubwa zaidi ni kuwa vibaraka."
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki alisema lengo kubwa la mafisadi hao ni kuhakikisha wanashika kila sehemu ya nchi ili iwe rahisi kwao kuendelea kutafuna rasilimali za nchi kwa kupitia watu wao. Alienda mbali zaidi na kutoa mfano wa miaka ya zamani ambapo nchi za Uingereza na Ufaransa kulikuwa na wafalme ambao walikuwa wakiwaajiri watu ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kumchekesha mfalme huyo hata kama atakuwa amekosea.
"Wachekeshaji wa mfalme wao wanawajibika kwa mfalme, kumsifia, kuremba kupiga vijembe, kuwa vibaraka, kujipendekeza, kumpamba, lakini kubwa zaidi ni kumchekesha mfalme hata kama amefanya mabaya,” alisema. Sitta alisema wachekeshaji hawana aibu kwani lengo lao ni kuhakikisha kuwa mfalme anafurahi kwa kila kitu hata siku akitembea uchi wao wanasema mfalme umependeza na kanzu yako inang'aa dhahabu. Alisema kuwa hali inazidi kuwa mbaya zaidi pale watu hao ambao ni vibaraka wanapojivunia kuwa vibaraka wa watu fulani huku wakipita na kujisifu usiku na mchana wakiwatambia wajumbe.
Waziri huyo alisema umefika wakati wa chama hicho kuzaliwa upya vinginevyo kitaendelea kupata upinzani hata kutoka katika vyama vidogo. Hata hivyo, Waziri huyo alisema ataendelea kusema na wala hataogopa kitu chochote na atakayenuna na anune kwani yeye ni 'Chuma cha Pua' kwa kuwa anaamini anasimamia katika ukweli. "Ndiyo maana wengine nikisema huwa wananuna, wananuna kwa sababu hawawatendei haki Watanzania. Nchi imejaa mali na rasilmali, lakini zinatumiwa na watu wachache wenye uchu badala ya kuzitumia sote," alisema na kuongeza: "Mimi ni msemakweli ndiyo maana kule kwetu Urambo wananiita 'Chuma cha Pua.' Watu wengine wanasema nailaumu Serikali wakati mimi nipo serikalini na kwamba hiyo ni aibu... Sasa aibu ipo wapi? Hapa mimi nipo ndani ya Serikali lazima niseme vitu hivi kamwe siwezi kunyamaza na kuacha mambo yakiharibika."
Sitta alilaani tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali wanaonyamazia maovu kwa kuwa tu wanaogopa kuonekana wabaya ndani ya jamii. Alisema viongozi wengine wamekuwa wanafiki kwa kuwa wako ndani ya Serikali na mambo yanaharibika wananyamaza hivyo nao kuwa kama wachekeshaji wa mfalme. Alisema watu wanatumia vibaya madaraka, kuna watu wazima wanafikiri kwa kutumia matumbo yao badala ya akili wakati mwingine wanajisahau na kuwa na matumbo makubwa mpaka yanawashinda. Aliwataka watu wote wanaohusika kuleta viongozi katika chaguzi hizo watumie fursa hiyo kuweka viongozi bora na si bora viongozi ambao wana masilahi yao binafsi.
Wakati hali katika chaguzi hizi zikienda ovyo, Waziri Sitta alisema pia kuwa amepata fununu mafisadi hao wanafanya kila njia kuhakikisha wanaweka vibaraka wao katika uongozi wa wilaya hiyo ili kuhakiksha wanaendelea kunufaika na migodi iliyopo katika wilaya hiyo. "Nimepata taarifa kuwa eti umeme unapatikana katika migodi ambayo inazunguka wilaya hii saa 24, lakini cha ajabu wananchi hawafaidiki na umeme huu. Hii inamaanisha nini hasa? Yaani wawekezaji ni bora sana kuliko wananchi? alihoji Sitta. Mahafali hayo pia yalihudhuriwa na Mbunge wa jimbo hilo, James Lembeli ambaye alisema shule hiyo imeujengea sifa mji wa Kahama kwa kuwa mwaka jana ilikuwa ya pili kitaifa na kutoa wanafunzi bora watatu katika 10 bora ambao walishika nafasi ya kwanza, tatu na ya nne.
Lembeni ambaye ndiye aliyeonyesha wazi kuanza kuchochea moto huo wa Sitta alisema kuwa wahitimu wa shule hiyo ndio wanaohitajika katika taifa la Tanzania kwa kuwa wamekuzwa katika misingi ya kutokupenda rushwa, kwani hata kujiunga na shule hiyo inahitaji uadilifu wa hali ya juu. Mkurugenzi wa Shule hiyo, Pauline Mathayo alisema hata siku moja hawezi kuruhusu vitendo vya kifisadi katika shule yake kwani anaamini elimu ikitumika vibaya inaweza kuzalisha watu hatari sana katika taifa. "Wote ni mashuhuda, sasa wizi wa benki kwa njia ya mtandao umezidi kuongezeka yote hii inatokana na kutumia elimu vibaya,"alisisitiza Mathayo.
Chanzo gazeti la Mwananchi
Post a Comment