Loading...
Maximo afunguka kuhusu kuja kuinoa Yanga
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Mbrazil Marcio Maximo akiri kuwa ni kweli yupo katika mazungumzo na klabu ya Yanga ila bado hawajakubaliana siku ya kuja na si rahisi kama wanavyodhani.
Maximo kwa sasa anafundisha kwa mafanikio makubwa klabu ya Democrata F.C ya Mjini Rio de Jeneiro Brazil.
Maximo aliondoka nchini baada ya mkataba wake kumalizika Agosti mwaka 2009 ambapo Shirikisho la soka nchini TFF lilishindwa kumuongezea mkataba kwa kutoridhishwa na utendaji wake na nafasi yake kuchukuliwa na Mdenmark Jan Poulsen ambae pia alishindwa kuitoa Tanzania kimasomaso.
Akizungumza na Dimba kwa njia ya mtandao Maximo alisema bado yupo katika mkataba na klabu yake hivyo si rahisi yeye kukurupuka na kuondoka ni lazima afuate mkataba unavyosema.
“Ni kweli nipo katika mawasiliano na Yanga lakini tupo katika mazungumzo kwani nina mkataba na klabu ya Democrata si rahisi mimi kuja huko kwa sasa bila kufuata taratibu, hata hivyo hadi sasa hatujapanga na Yanga tarehe ya kuja huko, nashangaa kusikia kuwa watu wanasubiria kuwasili kwangu.
“Mimi naheshimu sana mkataba na kama kuja ni lazima nifuate taratibu kwanza na si kukurupuka, si rahisi labda wasiwe wanajua nini maana ya mkataba, sijapangiwa na wala tiketi sina kwa kuwa hatujafikia huko,” alisema Maximo.
Maximo alieleza kuwa amefurahishwa na nia ya Yanga kumtaka na kama wataafikiana basi hana budi kuja kujiunga nao kwa ajili ya kuifundisha timu.
Alisema anaifatilia kwa makini ishu ya Yanga kwasababu anaona wakurugenzi wa Yanga wana nia thabiti ya kuendeleza klabu hiyo hivyo hataki kuwaangusha.
Kocha huyo ambae alileta hamasa kwa timu ya Taifa na kuifanya ipendwe na iwe gumzo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, amepata mawasiliano mengine toka kwa timu ya St. George ya Ethiopia na timu za Taifa za Zimbabwe na Rwanda ambayo ipo chini ya kocha Milutin Sredojevic ‘Micho’
Hata hvyo klabu ya Yanga jana ilijulisha umma kuwa Maximo alietarajiwa kufika jana sasa atawasili nchini mwishoni mwa wiki hii kitu ambacho Maximo hakijui.
Katika taarifa ya Yanga jana, ilieleza kuwa Maximo tayari amekwishatumiwa tiketi ya safari ya kuja hapa nchini na ameshindwa kuwasili jana kutokana na Klabu yake anayofundisha ya Democrata kukabiliwa na mchezo mgumu siku ya Jumamosi wiki hii kitu ambacho hakina ukweli.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Marcio mara baada ya kuwasili nchini atafanya mazungumzo na Uongozi wa Klabu ya Yanga ikiwemo kusaini Mkataba na Klabu ya Yanga kabla ya kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho.
Kocha huyo kabla ya kuondoka nchini Brazil amewaahidi Wanachama na Wapenzi wa Klabu ya Yanga kuwa atafanya jitihada za kukiimarisha kikosi cha Mabingwa wa Soka wa Afrika Mashariki na Kati katika kuinua vipaji mbalimbali kupitia soka la Vijana wenye umri mdogo kwa ajili ya kupata wachezaji Bora.
Ilieleza ambo mengine aliyoyapanga Kocha huyo ni pamoja na kuimarisha nidhamu kwa Wachezaji atakaokuwa akiwafundisha na mara baada ya kuanza kibarua chake cha kukinoa kikosi hicho atakuwa na mtihani wa kwanza kwa kukabiliwa na michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 23 hadi Agosti 7 Mwaka huu.
Post a Comment