Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi jana tarehe 26 June 2012 mbele ya
waandishi wa habari kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob
Michelsen kutoka Denmark ambaye amechukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye
hivi sasa anainoa Taifa Stars.
Michelsen
ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa
TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya
kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.
Kabla
ya kuja Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza
ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la
Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka Chama cha
Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja
ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken
kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata
msimu wa 2005/2006.
TFF KUZAWADIA WAPIGA PICHA COPA COCA-COLA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litawazawadia wapiga picha za
magazetini watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya
Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mashindano
hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28
yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani
Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.
Zawadi
ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action
picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi
ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka
17.
Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
NGORONGORO HEROES KUJIPIMA KWA MISRI, RWANDA
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes)
itacheza mechi nne za kirafiki na timu za Misri na Rwanda kabla ya
kuivaa Nigeria kwenye mashindano ya Afrika.
Ngorongoro
Heroes ambayo kwa mara ya kwanza itakuwa chini ya kocha mpya Jakob
Michelsen itaanza kwa kucheza mechi mbili za Misri zitakazofanyika Julai
3 na 5 mwaka huu, na baadaye Julai 14 na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.
Mechi
zote zitachezwa nchini, na kama ilivyo Ngorongoro Heroes, Misri na
Rwanda nazo ziko kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi za kucheza
Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
zitakazofanyika mwakani nchini Algeria.
Katika
raundi ya kwanza, Ngorongoro Heroes iliitoa Sudan ambapo katika raundi
ya pili imepangiwa Nigeria, na mechi ya kwanza itafanyika jijini Dar
es Salaam, Julai 29 mwaka huu. Timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye
nchini Nigeria.
Iwapo
Ngorongoro Heroes itafanikiwa kuitoa Nigeria, katika raundi ya mwisho
itacheza na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Afrika Kusini.
MABINGWA COPA WALALA KWA RUVUMA
Ruvuma
imeanza vizuri michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa
watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo
asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam.
Kigoma
ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa
juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila
kipindi.
Mabao
yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji
huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika
dakika ya 84.
Katika
mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka
sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers
ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mkoani
Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati
Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo uliochezwa
Uwanja wa Tamco.
Chanzo:
Post a Comment