Wakati mwingine tukubali kujitazama kwa macho ya wengine na
tutofautishe hali hii na kupewa ushauri katika mambo mbalimbali ya
maisha.
Ninataka kutofautisha kujitazama kwa macho ya watu
wanaotuzunguka na kupewa ushauri na watu wanaotuzunguka. Ushauri
unaweza kupewa na kila mtu. Kila mmoja atakupa mawazo yake kutokana na
uwezo wake wa kufikiri. Ushauri unaweza kupewa baada ya kuuomba au kuna
wengine mabingwa wa kutoa ushauri wa bure watakufuata kutokana na
misukumo mbalimbali ndani yao. Huu unaweza kuupuza kwa kuwa si kila
unachoambiwa ufanye ni sahihi. Wengine watakushauri kutokana na makuzi
yao, imani zao, uwezo wa kufikiri n.k. Ukifika hapa inabidi tu ukumbuke
hadithi ya Mbayuwayu.
Yupo atakayekufuata kukushauri ubadili mwenendo
fulani kwa kuwa kwa mtazamo wake wewe umetoka ‘nje ya reli’, wapo
marafiki watakushauri uachane na mpenzi wako kwa kuwa ni kicheche na
wazazi wanaweza kukushauri uachane na rafiki fulani kwa kuwa si mwema.
Huo ni ushauri ambao ninaamini umeshawahi kupewa
mpaka nyingine zikakuvunja mbavu, kwa maana mtu anakushauri uache kitu
ambacho mwenyewe unaamini bora ufe kuliko kukiacha hicho. Mfano ni pale
mlokole anapomfuata kijana wa ‘dot com’ akimshauri aache kwenda disko na
kuvaa mlegezo
Kujitazama kwa macho ya wengine ni tofauti kabisa
na kushauriwa, hii ni taswira ambayo unaipata baada ya kusikia maneno
kadhaa yakirudia masikioni mwako kutoka kwa watu wa karibu yanayokuhusu
wewe.
Kuna maneno umeyasikia mara kadhaa yakizungumzwa
juu yako, wakati mwingine si kwa kukuteta bali wapo waliokwambia usoni
kwako kuwa uko hivi na vile.
Hayo maneno ndiyo hasa taswira yako kwa wingine
ambayo kwa uwezo wa kawaida wa kibinadamu si rahisi kujua. Hapa ndipo
linakuja suala la kujitazama kwa macho yaw engine.
Mara ngapi umeambiwa wewe ni mvivu, mwoga, mzembe, chakubimbi,hupendi kujifunza na mengine kadha wa kadha?
Binafsi tangu mdogo nilikuwa naambiwa kuwa mzembe
na si mfuatiliaji wa mambo muhimu. Ninakumbuka wakati niko shule ya
sekondari kila mtu alikuwa ananiambia kama ukiacha kucheza na kusoma
utakuwa wa kwanza nchi nzima kwasababu nilikuwa na akili sana lakini
sisomi wala kuandika notisi.
Nimeendelea hivyo hata kazini bosi wangu alikuwa
akinisifu kuwa ninaweza kazi lakini siweki bidii ya kutosha kwani
nikifanya hivyo ninaweza kuwa ‘best of the best’ katika kizazi changu
kwasababu uwezo ninao.
Ilifika wakati nikafungua masikio na kuyasikiliza
macho ya wengine yananitazamaje, nikagundua udhaifu wangu kupitia wao.
Ingawa kwa miaka mingi niliupuuzia mtazamo huo lakini haukuweza
kubadilisha ukweli.
Ni mara ngapi wewe mwenzangu umeambiwa upungufu
wako, je umeyakubali au unawanunia watu na kuwaona wanakuonea. Sikiliza
sauti hizi kwa makini, zikijirudiarudia jua kuna ukweli ndani yake.
fualitilia zaidi : http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Kuna-wakati-tujitazame-kwa-macho-ya-wengine/-/1597592/1869294/-/ievsba/-/index.html
fualitilia zaidi : http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Kuna-wakati-tujitazame-kwa-macho-ya-wengine/-/1597592/1869294/-/ievsba/-/index.html
Post a Comment