Mhe: Tundu Lissu |
UTANGULIZI
Julai
13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha Maoni yake kuhusu
Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka
wa fedha 2012/2013. Pamoja na mambo mengine, Maoni ya Kambi yalihusu
utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.
Maoni
ya Kambi yalizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge huku wachangiaji
wengi wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa “kuidhalilisha” Mahakama na/au
“kuwadhalilisha majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe CCM); “kuwavunjia
heshima majaji” (Naibu Spika Job Ndugai); kuwatukana na kuwadhalilisha
majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa Kaskazini); “kuwa-offend, kuwadhalilisha
na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter Mshama-Nkenge CCM); “kufedhehesha
Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema).
Aidha,
Msemaji wa Kambi alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye na
akili timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni CCM)); na “kujiamini kwamba
yeye anajua zaidi kuliko watu wengine wote” (Mangungu). Kwa upande wake,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alilihakikishia Bunge
kwamba “... haijatokea hata siku moja katika nchi hii Rais akamteua Jaji
wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo yaliyopelekwa kwake na hii
Tume ya Uajiri wa Mahakama.” Zaidi ya hayo, “... labda Mheshimiwa Lissu
anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa
tu mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna… hawa majaji wote
walioteuliwa wamepitia mchakato huu wa kikao kizito sana cha watu ambao
ndiyo wenye sheria ya nchi hii.”
Baadaye
Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta kauli yake kuhusu uteuzi wa majaji
usiofuata utaratibu uliowekwa na Katiba. Msemaji wa Kambi alikataa
kufuta kauli hiyo ambako Mwenyekiti wa Kikao alielekeza Msemaji wa Kambi
apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hatua
zaidi. Alichukua uamuzi huo ili masuala hayo yapatiwe ufafanuzi ili
wananchi wapate picha kamili na ya kweli kuhusu jambo hili muhimu.
Maelezo haya yana lengo la kutoa ufafanuzi huo.
Katika
maelezo yake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya BUnge, Lissu
alisema, “Nitajitahidi kwa kadri inavyowezekana kutoa ushahidi
unaothibitisha kwamba siyo tu kwamba utaratibu wa kikatiba katika uteuzi
wa majaji umekiukwa mara nyingi, bali pia majaji wengi walioteuliwa kwa
utaratibu wa nje ya Katiba wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa kila
hali hawakufaa kukabidhiwa Madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.”
TATIZO LA MUDA MREFU
Kuna
ushahidi mkubwa kuthibitisha kwamba kuna watu wameteuliwa kuwa Majaji
wa Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko
katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha
kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya
karibuni.” Ni muhimu kuweka wazi hapa kwamba utamaduni huu haukuanza
baada ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais, bali ni tatizo la
muda mrefu. Kwa mfano, marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji Madina Muro na
majaji Stephen Ihema, Juxton Mlay, Augustine Shayo na Vincent Lyimo
waliteuliwa majaji wa Mahakama Kuu baada ya utumishi wa muda mrefu
kwingineko katika utumishi wa umma.
Majaji
Masaba na Muro waliteuliwa huku wakiwa wagonjwa mahututi na – kwa kadri
ninavyofahamu - hawakuwahi kuandika hukumu hata moja kabla ya mauti
kuwafika! Jaji Lyimo aliteuliwa Machi 28, 2007 mwaka mmoja kabla ya muda
wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika Oktoba 26,
2007 Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo Phillemon Luhanjo alimtaarifu Jaji
Mkuu kwamba Rais Kikwete “... ameamua kusogeza mbele muda wa kustaafu
wa Mheshimiwa Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo kwa miaka mitatu kuanzia
Machi 28, 2008 siku ambayo angestaafu kwa lazima”!
Kwa
upande wao, Majaji Ihema, Mlay na Shayo walijizolea umaarufu kwa kuwa
majaji wasioandika hukumu na hivyo kuwa wacheleweshaji wakubwa wa kesi
katika Mahakama Kuu. Jaji Ihema alitia fora kwenye jambo hili kiasi
kwamba Juni 16, 2003 Mwenyekiti wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute, alilazimika kumwandikia Rais
Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania “kwa uzembe na kukosa maadili.”
Mzee
Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’
uamuzi kwa zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo
na kukabidhiwa Jaji mwingine aliyeandika uamuzi ndani ya wiki tatu!
Mwezi mmoja kabla ya barua ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake
walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu Barnabas Samatta kulalamikia
ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao walidai: “Hadhi na
heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi ya miaka
mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi
ya pingamizi.” Licha ya malalamiko haya dhidi yake, Jaji Ihema alipatiwa
mkataba wa ajira wa miaka miwili mara baada ya kustaafu mwaka 2005.
MAJAJI WA MIKATABA
Agosti
2, 2005 Jaji Kiongozi Hamisi Msumi alitoa taarifa kwa majaji wote wa
Mahakama Kuu kwamba Jaji Ihema alikuwa amepewa mkataba mpya baada ya
kustaafu kama Jaji wa Mahakama Kuu. Taarifa hiyo ilimfanya Jaji Bernard
Luanda, wakati huo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, kuhoji
‘Uhalali Kikatiba kwa Majaji Kufanya Kazi kwa Mkataba Baada ya
Kustaafu.’ Katika taarifa yake kwa Jaji Kiongozi Msumi, Jaji Luanda
alisema kwamba “... suala la majaji kupewa mikataba ... linaenda kinyume
na Katiba.” Jaji Luanda alifafanua: “Kwa kuwa Jaji amestaafu, basi
kiapo chake nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike
kazi hizo za ujaji.... Ni hoja yangu kwamba Majaji waliostaafu na kupewa
mikataba si Majaji kwa mujibu wa Katiba.”
Msimamo
wa Jaji Luanda uliungwa mkono mwaka mmoja baadaye na Jaji wa Rufaa,
Augustino Ramadhani wakati huo akiwa Kaimu Jaji Mkuu. Katika ‘Mawazo
Kuhusu Vifungu Vinavyohusu Mahakama na Majaji’ aliyomwandikia Jaji Mkuu
Samatta na kunakiliwa kwa Majaji wa Rufaa wote, Jaji Ramadhani alisema
kwamba “... sio sahihi kwa Jaji Mkuu kustaafu na kupewa mkataba wa
kuendelea na wadhifa huo kupindukia umri wa miaka 65 (ambao ndio umri wa
kustaafu kwa lazima kwa Jaji wa Rufaa na Jaji Mkuu).” Baadaye Jaji
Luanda aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wakati Jaji Ramadhani alikuja kuwa
Jaji Mkuu wa Tanzania.
Kauli
ya Kambi kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa Katiba kuhusiana na uteuzi wa
majaji inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya Serikali na hasa Ofisi ya
Rais, Ikulu yenyewe. Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji
waliostaafu ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Katibu
Mkuu Kiongozi Luhanjo. Wajumbe wengine walikuwa pamoja na Mwanasheria
Mkuu Johnson Mwanyika na Naibu wake Sazi Salula, Katibu Mkuu Utumishi
George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura na Susan
Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Kwa
mujibu wa Kumbukumbu za Mkutano huo, “kwa utaratibu unaotumika sasa,
baadhi ya Majaji wanaofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya
110(1) kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Ibara ya 120(1) ya Katiba
wanaongezewa muda wa kuendelea na utumishi wao kwa mkataba baada ya wao
kuwasilisha maombi rasmi.” Baada ya mjadala juu ya jambo hili, wajumbe
wa mkutano walikubaliana kwamba “utaratibu wa kuongeza muda kwa njia ya
mkataba unakiuka masharti ya Katiba na kuleta mkanganyiko kama Majaji
hao wanastahili kulipwa mshahara au pensheni au vyote kwa pamoja.”
Matokeo
ya mkutano wa Ikulu ilikuwa ni kuundwa kwa ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya
Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu’ chini ya
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kikundi Kazi
kiliwasilisha Taarifa yake Machi 7, 2008. Katika Taarifa yake Kikundi
Kazi kinakubaliana na msimamo wa kikatiba kwamba “kwa kuzingatia Ibara
za 110 na 120 za Katiba inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba
kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri
wa kustaafu ni kinyume cha Katiba.” Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hadi
mwezi Machi 2008, “... walikuwepo Majaji wawili ... wa Mahakama ya
Rufani na Majaji tisa ... wa Mahakama Kuu, ambao wapo katika ajira za
mkataba, na Jaji mmoja ... wa Mahakama Kuu aliyeongezewa muda wa ajira
kwa mujibu wa masharti ya Katiba....”
Hii
ina maana kwamba, kulikuwa na Majaji kumi na moja ambao walikuwa
wanafanya kazi kinyume cha Katiba na – kwa maneno ya Jaji wa Rufaa
Luanda – hawakuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba! Aidha, kwa mujibu wa
ushahidi wa nyaraka hizi, kulikuwa na Jaji mmoja tu ambaye alikuwa
ameongezewa muda wa ajira ya ujaji kwa mujibu wa Katiba. Katika
mapendekezo yake, Kikundi Kazi hakikumung’unya maneno:
“Mikataba
iliyopo hivi sasa iko kinyume cha Katiba.... Hii ina maana kwamba
Majaji hao wanafanya kazi ya Jaji kinyume cha Katiba, hivyo kazi zote
ambazo wamezifanya na wanaendelea kuzifanya wakiwa chini ya ajira mpya
za mikataba hazina uhalali wowote kisheria. Kazi hizo ni sawa kama vile
zimefanywa na mtumishi mwingine yeyote asiye na madaraka ya Jaji. Hivyo
basi, Rais ashauriwe kuifuta mikataba hiyo mara moja kwa vile ina
madhara makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa Majaji wapya kuchukua
nafasi zao. Majaji waliofutiwa mikataba waendelee na pensheni zao kama
kawaida.”
Miaka
minne imepita tangu Kikundi Kazi kiwasilishe mapendekezo yake Ikulu
lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo. Aidha,
licha ya msimamo wa majaji Luanda na Ramadhani kuwa na umri wa takriban
miaka saba, utaratibu wa uteuzi wa majaji wastaafu haujaachwa na mamlaka
husika ya uteuzi. Ajira ya sasa ya Jaji Kiongozi Fakih Jundu iko katika
kundi hili la watu wasiokuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba.
JAJI KIONGOZI FAKIH JUNDU
Jaji
Kiongozi Fakih Jundu aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais Mkapa
mwaka 2003. Julai 29, 2009, Jaji Jundu wakati huo akiwa Jaji Mfawidhi
wa Kanda ya Iringa, alitoa taarifa ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, mara baada ya kutoa taarifa hiyo, Jaji Jundu siyo tu alipewa
mkataba wa ujaji kwa miaka mitatu, bali pia alipandishwa cheo na
kufanywa Jaji Kiongozi.
Kama
hiyo haitoshi, inasemekana sasa kwamba Jaji Kiongozi Jundu ameongezewa
mkataba mwingine tena wa miaka miwili kuendelea kuwa Jaji Kiongozi
kuanzia Julai 29, 2012! Huu ni ukiukaji wa Katiba. Kwanza, kwa mujibu wa
Taarifa ya Kikundi Kazi, “... umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi ni
miaka sitini.... Hivyo, iwapo Rais atamuongezea Jaji Kiongozi muda wa
kufanya kazi, hatamuongezea kama Jaji Kiongozi.”
Kwa
maana nyingine, kama ilikuwa makosa kikatiba kumpa Jaji Jundu mkataba
wa ajira kama Jaji wa kawaida, ilikuwa makosa makubwa zaidi kikatiba
kumpandisha cheo na kumfanya Jaji Kiongozi wakati alikwishafikisha umri
wa kustaafu wa Jaji Kiongozi! Pili, kwa utamaduni uliozoeleka Tanzania,
majaji wamekuwa wanaongezewa kipindi kimoja cha miaka miwili ili
wamalizie kesi walizokuwa nazo hadi muda wao wa kustaafu unawadia. Kwa
msimamo wa kikatiba ulioelezwa na Jaji wa Rufaa Luanda, Jaji Mkuu
Ramadhani na Kikundi Kazi, siyo sahihi kwa Jaji Kiongozi Jundu kustaafu
na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia muda wake wa
kustaafu kwa mujibu wa Katiba!
Nyongeza
hii ya pili ya mkataba wa Jaji Kiongozi Jundu imewafanya watu
wanaojiita ‘Watumishi wa Mhimili wa Mahakama’ kumwandikia Msajili wa
Mahakama ya Rufani ya Tanzania kulalamikia jambo hilo. Kwa mujibu wa
barua yao, ambayo pia ilinakiliwa kwa Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu,
watu hao wamesema yafuatayo kuhusu Jaji Kiongozi Jundu: “Sisi watumishi
wa Mahakama tunafahamu udhaifu mkubwa kiutendaji alionao Jaji Kiongozi
wetu wa sasa. Kimsingi hamudu madaraka haya. Ipo mifano mingi ya udhaifu
wa Jaji Jundu. Mfano alimhamisha hakimu kutoka kituo chake cha kazi
kama adhabu kwa vile hakimu huyo alitoa maamuzi ambayo yeye
hakuyafurahiya kwenye ile kesi maarufu ya kibaragashia. Ni busara za
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, ndizo zilizomsaidia hakimu huyo.”
JAJI THOMAS MIHAYO
Thomas
Bashite Mihayo aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Oktoba 8,
2003. Januari 16, 2006 Jaji Mihayo alitoa notisi ya kustaafu kwa mujibu
wa Katiba kuanzia Juni 8, 2006 atakapokuwa ametimiza umri wa miaka
sitini. Hata hivyo, Machi 8 ya mwaka huo, Jaji Mihayo alitaarifiwa na
Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete alikuwa amempa “... mkataba wa miaka
miwili kuanzia Juni 9, 2006.” Mkataba huo ulifikia mwisho wake Juni 8,
2008. Hata hivyo, Jaji Mihayo alipatiwa mkataba mwingine tena wa mwaka
mmoja ulioanzia Juni 9, 2008 hadi Juni 8, 2009 na baada ya hapo
hakupatiwa mkataba mwingine.
Inaelekea
Jaji Mkuu Ramadhani alisahau msimamo wake wa awali kuhusu ajira za
mikataba kwani ndiye aliyependekeza Jaji Mihayo “... apewe mkataba
mwingine wa mwaka mmoja...” Na wala si Jaji Mihayo pekee aliyepatiwa au
kuongozewa mkataba katika mazingira tatanishi kama haya. Kwa mujibu wa
nyaraka za Idara Kuu ya Utumishi, Jaji Donasian Mwita alipatiwa mkataba
wa ujaji Juni 28, 2004. Mkataba huo wa miaka miwili ulianza kutumika
Julai 1, 2004. Vile vile, Jaji Joseph Masanche alisaini mkataba wa aina
hiyo hiyo na Idara Kuu ya Utumishi ulioanza kutumika kuanzia Machi 7,
2006.
MAADILI YENYE SHAKA
Msemaji
wa Kambi hakuzungumzia masuala yanayohusu maadili ya majaji. Hata
hivyo, kutokana na mjadala uliojitokeza ndani na nje ya Bunge kutokana
na hotuba yake, ushahidi umepatikana unaoonyesha kwamba baadhi ya majaji
wameteuliwa bila ya kwanza kuwafanyia uchunguzi juu ya maadili yao.
MAJAJI KASSIM NYANGARIKA NA ZAINAB G. MURUKE
Kassim
Nyangarika alikuwa wakili wa kujitegemea na wakili mwenza wa Jaji
Kiongozi Jundu kabla ya uteuzi wake kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka
2003. Kama wakili, Bwana Nyangarika aliwahi kumwakilisha mlalamikaji
katika kesi ya Peter Muti dhidi ya CIELMAC Ltd., Kesi ya Madai Na. 314
ya 2003 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. Katika
kesi hiyo mteja wa wakili Nyangarika alishinda.
Hata
hivyo, kufuatia rufaa dhidi ya uamuzi huo, Mahakama Kuu ilifutilia
mbali mwenendo wa kesi hiyo baada ya kugundua kwamba Wakili Nyangarika
alikuwa amefanya vitendo vyenye kuashiria uvunjifu mkubwa wa maadili.
Kwa mfano, Mahakama Kuu iligundua kuwa Wakili Nyangarika alimwelekeza
hakimu – kwa kutumia ‘kipande cha karatasi cha rafu na kilichoandikwa
kirafiki’ - namna ya kuendesha kesi hiyo. Mahakama Kuu iligundua makosa
makubwa zaidi ya hilo. Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, “... kulikuwa na
mawasiliano yasiyokuwa rasmi kati ya Mahakama na Wakili.” Jaji Kalegeya
alikuta ushahidi wa uwezekano mkubwa kwamba Wakili Nyangarika ndiye
aliyeandaa uamuzi wa Mahakama katika kesi hiyo. Aidha, Mahakama Kuu
iligundua kwamba Wakili Nyangarika “... aliielekeza Mahakama kutokutoa
uamuzi kwa tarehe iliyopangwa badala yake aliielekeza itoe uamuzi huo
tarehe nyingine.”
Kwa
mujibu wa Jaji Kalegeya, kama kilichoonyeshwa katika mawasiliano ya
Wakili Nyangarika na Mahakama ya Wilaya kilikuwa cha kweli basi “...
utoaji haki katika Mahakama hiyo uko katika hatari kubwa kama sio jina
la Mahakama yote, kitu kinachohitaji marekebisho ya haraka.” Kwa sababu
hiyo, Jaji Kalegeya alielekeza kwamba “mamlaka husika zichukue hatua za
kufichua ukweli kuhusu barua ya Wakili Nyangarika ya tarehe 18/03/2004.”
Hukumu na maelekezo ya Jaji Kalegeya yalitolewa tarehe 22 Julai, 2005.
Miezi saba baadaye, Wakili Nyangarika aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania!
Wakili
mwingine mwenye maadili ya mashaka yanayofanana na ya Jaji Nyangarika
ambaye pia ameteuliwa Jaji Mahakama Kuu ni Zainab Muruke. Kama wakili,
Zainab Muruke alimwakilisha Stephen Hill Forwood ambaye alikuwa
amepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili
bila faini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Baadaye kampuni ya
mawakili ya Z.G. Muruke & Co. Advocates iliwasilisha Hati ya
Mapitio (Memorandum of Review) katika Mahakama hiyo hiyo ikiomba Bwana
Forwood abadilishiwe hukumu.
Ombi
hilo lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Kabuta na tarehe 26 Julai,
2004, Bwana Forwood akabadilishiwa adhabu kuwa faini ya shilingi 20,000
au kifungo cha miaka miwili. Jambo hili liliripotiwa kwa Jaji Kiongozi
ambaye aliamuru uchunguzi ufanywe uliopelekea kushushwa cheo cha Hakimu
Mkazi Kabuta. Jaji Kiongozi pia aliamuru Wakili Muruke atoe maelekezo ya
ushiriki wake katika sakata hilo. Hiyo ilikuwa tarehe 14 Desemba, 2004.
Mwaka mmoja na miezi miwili baadaye, Zainab Muruke aliteuliwa Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania.
MAJAJI PELAGIA B. KHADAY NA PATRICIA FIKIRINI
Bi.
Pelagia B. Khaday ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa
mwaka 2009. Kabla ya uteuzi huo Bi. Khaday alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kabla ya hapo alikuwa Hakimu Mkazi
Mkuu na Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Agosti 12,
2004, alipewa taarifa ya kusimamishwa kazi kama Msajili wa Wilaya na
kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na ‘uzito wa
shutuma’ zilizotolewa dhidi yake kwa Jaji Mkuu.
Taarifa
hiyo iliandikwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Edward
Rutakangwa, kwa maelekezo ya Jaji Mkuu na ilieleza kwamba Bi. Khaday
alikuwa anatuhumiwa kwa “kuwashinikiza au kuwashawishi baadhi ya
mahakimu mkoani Arusha kushughulikia au kuamua kwa upendeleo mashauri
yaliyowahusu ... jamaa au rafiki zake”; na “kuwaandalia sababu za rufaa
baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani na mahakama za mahakimu hapa
mkoani.”
Kabla
ya kumsimamisha Bi. Khaday kazi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alikuwa
amemteua Mheshimiwa Jacob Somi, wakati huo akiwa Msajili wa Mahakama Kuu
Kitengo cha Ardhi, kuwa Afisa Uchunguzi (Enquiry Officer) ili
kuchunguza tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Taarifa ya Uchunguzi wa Awali ya
Afisa Uchunguzi Somi inasema kwamba Bi. Khaday alikuwa amelalamikiwa na
mahakimu kwa kuwashinikiza ili watoe maamuzi ya kesi zilizokuwa
zinawakabili jamaa au marafiki zake.
Kwa
mujibu wa Taarifa hiyo, Hakimu Mkazi Elvin Mugeta “alikiri
kuwa-approached na Bi. Khaday ili atoe hukumu ya upendeleo kwa mshtakiwa
Richard Bareto ambaye inasadikiwa kuwa ni jamaa wa rafiki yake wa
karibu.” Ijapokuwa Bi. Khaday alikanusha kufanya hivyo, Afisa wa
Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “Bi. Khaday alikuwa amejiwekea
utaratibu, kama alivyodai mwenyewe, wa kuwasiliana na Mahakimu kwa lengo
la kuwafahamisha pamoja na mambo mengine malalamiko yaliyokuwa
yakimfikia dhidi yao ili kuwanusuru wasiharibikiwe.”
Hata
hivyo, Afisa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “utaratibu huu ulikuwa
kero kwa mahakimu pale alipoutumia kwa kushinikizwa na jamaa zake na/au
rafiki zake kwa lengo la kupata maamuzi ya upendeleo. Kitendo cha kumtoa
mahakamani Hakimu kwa lengo la kutaka kujua hatima ya mshtakiwa Bareto
aliyekuwa asomewe hukumu siku hiyo, ni mfano wa matumizi mabaya ya
utaratibu huo.”
Afisa
Uchunguzi Somi hakupata uthibitisho wa madai ya Bi. Khaday kuwaandalia
sababu za rufaa washtakiwa waliotiwa hatiani. Hata hivyo, kwa mujibu wa
Taarifa yake, “... sikuridhishwa na utaratibu wake wa kupeleka nakala ya
hukumu kwa Bi. Mushi na kumtaka aisome ili kuona kama kuna uwezekano wa
mshtakiwa Hussein Ramadhani Kitema kukata rufaa Mahakama Kuu baada ya
kufungwa jela na Bw. Mugeta.” Afisa Uchunguzi Somi alipendekeza kwamba
Bi. Khaday – “ambaye ni mtumishi wa Mahakama kwa kipindi kisichopungua
miaka 20...” - apewe nafasi ya kujirekebisha.
Baada
ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi, Jaji Mfawidhi
Rutakangwa alimteua Mh. Samuel Karua, Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo
cha Kazi, kuwa Investigation Officer. Tarehe 23 Februari 2007,
Investigation Officer Karua aliwasilisha Taarifa ya Uchunguzi wake kwa
Jaji Mkuu. Taarifa ya Investigation Officer Karua ilimkosha Bi. Khaday
kwa tuhuma zote dhidi yake.
Hata
hivyo, Taarifa ya Investigation Officer Karua ina maeneo mengi
yanayoleta mashaka. Kwanza, kama Investigation Officer Karua mwenyewe
alivyosema, shahidi muhimu katika uchunguzi wake alikuwa Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mushi. Vile vile, shahidi huyu alikuwa ‘star witness’ katika
uchunguzi wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi na ndiye aliyetoa
ushahidi wa yeye na mahakimu wengine kuingiliwa katika kazi zao na Bi.
Khaday.
Hata
hivyo, mbele ya Investigation Officer Karua, shahidi huyu muhimu
alikana kila kitu alichokisema mbele ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa kiasi
kikubwa, Investigation Officer Karua aliitumia about turn hii kumkosha
Bi. Khaday dhidi ya tuhuma zote zilizokuwa zinamkabili. Cha kushangaza
ni kwamba Investigation Officer Karua hakujiuliza na hakumuuliza shahidi
huyu sababu za kukana ushahidi wote alioutoa mbele ya Afisa Uchunguzi
Somi.
Je,
alirubuniwa au kutishwa ili amsaidie Hakimu na mtumishi mwenzake katika
Mahakama ya Tanzania asifukuzwe kazi? Kama sio hivyo, je, ni sababu
zipi zilizomfanya shahidi huyu muhimu kubadili ushahidi wake kwa kiasi
hicho? Je, ushahidi alioutoa shahidi huyu mbele ya Afisa Uchunguzi Somi
ulikuwa wa uongo? Na kama ulikuwa wa uongo, ushahidi wake wa pili kwa
Investigation Officer Karua ni wa kweli kiasi gani mpaka kumfanya
Investigation Officer Karua kutamka kuwa shahidi huyu ‘anaweza ... kuwa
anasema ukweli.’
Inaelekea
Investigation Officer Karua, Hakimu Mkuu Mkazi mwenye uzoefu wa miaka
mingi katika Mahakama, alifanya kazi yake kwa mtazamo wa kimahakama
zaidi badala ya kutumia mtazamo wa kiupelelezi na/au kiuchunguzi ambayo
hasa ndiyo ilikuwa kazi yake katika uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Bi.
Khaday. Kwa mtazamo wa kimahakama, ukweli kwamba shahidi muhimu kama
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi alikana ushahidi wake wa awali mbele ya
Afisa Uchunguzi Somi ilikuwa inatosha kumfutia Bi. Khaday hatia yote.
Kwa mtazamo wa kiupelelezi/kiuchunguzi, about turn ya shahidi huyu
ingemfanya Investigation Officer Karua kuchunguza zaidi sababu za
kigeugeu hicho.
Pili,
Investigation Officer Karua hakuipa uzito wa kutosha Taarifa ya Afisa
Uchunguzi Somi. Kwa mfano, Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi – yenye
kurasa 14 zilizochapwa - imeelezewa katika Taarifa ya Investigation
Officer Karua kwa aya moja tu! Kwa sababu hiyo, ni vigumu kukubaliana na
Investigation Officer Karua kwamba Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi
‘ilikuwa muhimu sana’ wakati umuhimu huo haujafafanuliwa wala kuelezewa
hata kidogo katika Taarifa yake.
Aidha,
Investigation Officer Karua alitakiwa kueleza sababu za kutofautiana na
Afisa Uchunguzi Somi kwamba Bi. Khaday alikuwa anakera mahakimu kwa
kuwasiliana nao baada ya kushinikizwa na ndugu au rafiki zake ili
wapatiwe upendeleo katika kesi zilizokuwa zinawakabili. Investigation
Officer Karua hakufanya hivyo. Vile vile, Investigation Officer Karua
hakuona ajabu wala kujiuliza kama ilikuwa ni kitu cha kawaida kwa Bi.
Khaday kumleta Richard Bareto – mshtakiwa aliyehusishwa na shinikizo la
Bi. Khaday kwa Hakimu Mkazi Mugeta – kama shahidi wake wa utetezi.
Tatu,
Investigation Officer Karua hakutoa sababu za maana za kutochukua
ushahidi wa mahakimu wengine waliodaiwa kushinikizwa na Bi. Khaday.
Katika aya moja tu iliyowahusu mahakimu hao, Investigation Officer Karua
alisema kwamba siku ya kutoa ushahidi wao kwake, watu hao “...
walishikilia msimamo wa kauli walizotoa mbele ya Bwana Somi ... na baada
ya tafakuri ya muda ... mashahidi hawa waliachiwa.”
Mbele
ya Afisa Uchunguzi Somi, mashahidi hawa wawili, Hakimu Mkazi Msumi na
Hakimu Mkuu wa Wilaya Mlay, walikuwa wamesema kwamba “... huko nyuma
(Bwana Msumi) aliwahi kuitwa na mlalamikiwa baada ya wadhamini
walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana ... kumpelekea malalamiko ya
kukataliwa dhamana, maelezo ambayo hayakuwa na ukweli wowote.” Aidha,
kwa mujibu wa Afisa Uchunguzi Somi, “... katika hali isiyokuwa ya
kawaida Bw. Mlay, PDM hakuwa tayari kueleza kilichomsibu hadi kujiengua
katika usikilizaji wa kesi ambayo Bi. Mushi alidai ilikuwa inamkabili
rafiki yake wa karibu na Bi. Khaday.” Investigation Officer Karua
hakuona sababu yoyote ya kufuatilia ushahidi wa mahakimu hawa wawili!
Nne,
Investigation Officer Karua anakubali kwamba hali ilikuwa tete katika
Kituo cha Arusha: “Inaelekea mtuhumiwa alikuwa na mahusiano mabaya na
baadhi ya mahakimu.” Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, Investigation Officer
Karua alikuwa na wajibu wa kuchunguza chanzo cha mahusiano hayo mabaya,
hasa kwa vile kulikuwa sio tu na tuhuma bali pia ushahidi wa mahakimu
husika kwamba Bi. Khaday alikuwa anawaingilia mahakimu katika kazi zao.
Hakufanya hivyo. Badala yake Taarifa ya Investigation Officer Karua
inaonekana kama jitihada za kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma nzito za
ukosefu wa maadili ya kimahakama. Jitihada hizi zilifanikiwa kwani
miaka miwili baada ya Taarifa ya Investigation Officer Karua, Bi. Khaday
aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Na
wala siyo Bi. Khaday pekee aliyeneemeka na taarifa hiyo. Bi. Patricia
Fikirini, ambaye Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi inamwelezea kama mmoja
wa mahakimu waliosikiliza kesi ya mfanyabiashara maarufu wa Arusha,
Justin Nyari iliyokuwa chanzo cha tuhuma dhidi ya Bi. Khaday –
alihusishwa na tuhuma dhidi ya Bi. Khaday kwa maneno yafuatayo: “...
Kama mtawala ... (Bi. Khaday) ... alisema aliwahi, tena kwa nia njema,
kumweleza Bi. Fikirini ... kuhusu uvumi kwamba mume wake alikwenda
gerezani na kuchukua mamilioni ya fedha kwa Bw. Nyari na hivyo kumshauri
awe mwangalifu zaidi”! Katika uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais
Kikwete mwezi Juni mwaka huu, Bi. Patricia Fikirini naye ameteuliwa kuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wapo
wanaoweza kusema kwamba Bi. Khaday hakupatikana na hatia yoyote na kwa
hiyo haikuwa makosa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, inaweza
kudaiwa kwamba Bi. Fikirini hajawahi kutuhumiwa kwa kosa lolote la
maadili na kwamba ‘uvumi’ pekee hautoshi kumnyima mtu mwenye sifa haki
ya kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa wenye hoja za aina hii jibu langu
ni kwamba kiwango cha ‘sifa maalum’ kinachotakiwa na Katiba kwa mtu
kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ni mtu ambaye “... kwa kila hali
anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu....” Kiwango hiki ni
cha juu kiasi kwamba kutokuwa na hatia pekee haitoshi kumfanya mhusika
kuwa ‘kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama
Kuu.’ Kwa maoni yangu, mtu aliyeundiwa uchunguzi wa kimaadili au ambaye
kuna uvumi unaomhusisha na rushwa ‘hafai kwa kila hali’ kukabidhiwa
madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu. Majaji Khaday na Fikirini wapo kwenye
kundi hili.
JAJI ALOYSIUS MUJULIZI
Jaji
Aloysius Mujulizi alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa
Majaji wa Mahakama Kuu mwezi Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji
Mujulizi alikuwa wakili wa kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya
Ishengoma, Masha, Magai & Mujulizi Advocates (IMMMA) ya Dar es
Salaam. Kampuni hii ya mawakili ndiyo iliyoshiriki katika kuanzishwa kwa
kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. mnamo tarehe 18 Machi 2004.
IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa Tangold Ltd.
Makampuni
haya mawili yanatuhumiwa kutumika kupitishia mabilioni ya fedha
zilizoibiwa Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 2005 na 2006. Kwa mfano,
katika kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 10,
2005 kampuni ya Deep Green Finance ilipokea jumla ya shilingi
10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya kulipia madeni ya nje (EPA)
iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania. Katika kipindi hicho hicho, kampuni ya
Tangold Ltd. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73 kutoka kwenye
akaunti hiyo ya EPA. Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili wa IMMMA
Advocates na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi
Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha kwamba Tangold Limited ilikuwa
kampuni ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius. Haya yote yalitokea
wakati Jaji Mujulizi akiwa wakili mwenza wa IMMMA Advocates.
‘SIFA MAALUM’ ZENYE SHAKA
JAJI WA RUFAA MBAROUK SALIM MBAROUK
Mbarouk
Salim Mbarouk aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania mwaka 2008. Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa Jaji wa
Mahakama Kuu ya Zanzibar. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa
zimeainishwa katika ibara ya 118(3) ya Katiba: “Majaji ... wa Rufani
watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa
watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ...
zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa watu
wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu
wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda
usiopungua miaka kumi na tano.”
Kwa
mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba ya Zanzibar, 1984, “mtu hatoweza
kuteuliwa kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu mpaka awe na shahada ya
Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha aina hiyo; au awe au
amewahi kuwa Jaji wa Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi zote za jinai
na madai katika Tanzania au sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au
Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au awe Mwanasheria wa Zanzibar au
Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka saba; au awe na uzoefu wa Jaji
au mwanasheria kwa pamoja usiopungua miaka saba.” Jaji Mbarouk
hajatimiza hata moja ya masharti hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu
hana shahada yoyote ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya
Tanzania kama inavyotakiwa na Ibara ya 109(7) ya Katiba. Jaji huyu ana
stashahada ya juu ya sheria (Post Graduate Diploma in Law) ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha
nchini Uingereza.
Uteuzi
wa Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minong’ono mingi katika
taaluma ya sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga
anasemekana kufungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka
uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo, Wakili Kalunga alifariki kabla ya
shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo liliondolewa mahakamani. Aidha,
monong’ono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk kujiunga na Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi ninapoandika Addendum
hii.
MAJAJI ‘WALIOTOLEWA MITAANI’
Katika
Maoni ya Kambi tulidai kwamba “... sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama na - kwa sababu hiyo - hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka
hiyo ya kikatiba....” Ukiacha uteuzi wa Jaji wa Rufaa Mbarouk ambao
haubanwi na masharti ya Ibara ya 109(1) na 113(1)(a) ya Katiba, majaji
wengine waliotajwa kwenye Addendum hii hawakupendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Mahakama. Majaji wengine ambao pia hawajawahi kupendekezwa
na Tume hiyo ni pamoja Fatuma Massengi, Mary Sumari, Imani Mkwawa-Aboud
na Sekela Mushi.
Chanzo Jamii forums
Post a Comment