Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga kauli za Serikali,
Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa
kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani
Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi huru ufanyike haraka kwa
mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).
Kauli
zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda
Jeshi la Polisi ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa
mauaji, badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa
wahusika.
Hivyokutokana
na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA
kinatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara
ya 33 ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie
na kuwezesha uchunguzi wa kina.
Ikumbukwe
kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua
risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa
CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano
halali wa CHADEMA na wengine waliokuwa wakiendelea na shughuli zao eneo
la Msamvu, hivyo kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na
kujeruhi wengine wawili.
CHADEMA
kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo
mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola
inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.
CHADEMA
hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu
tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani
tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa
zisizo za kweli kutoka kwa maofisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya
watuhumiwa wa mauaji husika.
CHADEMA
haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza
tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha
mauaji kwa kuwa tayari serikali na Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye
kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na
ushahidi wa picha za eneo la tukio.
Wakati
Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa
umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda
wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja
akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na mabomu ya machozi
yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na kudondoka.
Mashuhuda
wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa
na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa
baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa
wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.
Mara
baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi
lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa
ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na
kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na
eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya
kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.
Kauli
zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya
CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya
watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu
wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa
suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye
Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA
kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo
lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada
ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za Jeshi hilo Simon Siro na
hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa wananchi
waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.
Ikumbukwe
kwamba awali CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika
Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa
Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Hata
hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa
kisingizio cha Sikukuu ya Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana
na ile ya mikutano ya CCM, sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na
msingi wowote.
Baada
ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia
matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria
kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya
kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27
Agosti 2012 ambayo Jeshi la Polisi liliikubali.
Polisi
walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia
wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti
2012 Jeshi la Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba limetoa kibali
cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake kisheria) na pia limekataza
maandamano.
CHADEMA
kikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi
ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia
mbadala na tarehe 26 Agosti 2012 mazungumzo yakaendelea kwa lengo la
kukagua barabara.
Hata
hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro
Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa
mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za mikutano, polisi
ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu na
badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu za misingi ya kisheria na
zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi
kwa kutumia magari.
Maelezo
ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na
mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa kuwa
Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka
utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.
Jeshi
la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu
CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda
mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia nguvu kubwa na
kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na kuathiri
wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.
Iwapo
wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na
kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi
lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo hakuna kiongozi
yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa katika kituo chochote
cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.
Kinyume
chake Jeshi la Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa
mapokezi yafanyike kwa msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27
Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa wananchi na wanachama
wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu wakiwasubiri viongozi
bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika matembezi ya miguu
kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na vyombo vingine vya
usafiri.
Kitendo
cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na
kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda mrefu kiliwafanya
wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla kutawanyika kuelekea eneo la
mkutano na wengine kuingia barabarani kutembea kuelekea eneo la mkutano
na hatimaye polisi walipoona wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda
misafara hiyo mpaka eneo la mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi
kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo yasingetokea madhara yoyote.
Kwa
kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na
Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea,
CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya
Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.
CHADEMA
kwa mara nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika
kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka
ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya
Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za
mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.
CHADEMA
kinaikumbusha Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni na Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za
mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri
Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi bungeni kwamba sheria hiyo itaanza
kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.
Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.
Kwa
upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na
familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti
2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na CHADEMA kuwasilisha
rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu ushiriki kwa CHADEMA
kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano yanayoendelea na familia.
CHADEMA
kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena
tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha Operesheni za Maandamano na
Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa rai iliyotolewa na
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kupisha kukamilika kwa zoezi la sensa
ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka zingine za kiserikali.
CHADEMA
inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa
yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu
za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa yakiendelea katika barabara
kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio hicho.
Aidha,
wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya
tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua
ambayo ilifanywa pia na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza
ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe hiyo.
Tume
hiyo inaendelea na mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi
katika kata za mikoa mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa
likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni
kuingilia sensa.
CHADEMA
inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana
mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko
linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa maisha ya wachache yanaweza
kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa maslahi ya wengi.
CHADEMA
itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya
uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem) uliofanyika tarehe 28
Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au kukataa mwito wa kutumia
Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) kuwezesha uchunguzi huru.
Imetolewa tarehe 29 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
Post a Comment