Wakati raia tisa wa China wakibainika kuugua ugonjwa wa dengue na kulazwa hapa nchini, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kuagiza wizara zake mbili kukabiliana na ugonjwa huo kwa dharura.
Ugonjwa huo uliingia nchini tangu mwaka 2010
lakini mlipuko wake mkubwa ulibainika Machi mwaka huu na hadi jana
wagonjwa zaidi ya 400 walikuwa wameambukizwa, huku watatu wakiripotiwa
kufariki dunia, akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Gilbert
Buberwa anayezikwa leo, Dar es Salaam.
Rais jana aliziagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii na ile ya Fedha kushirikiana Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuchukua
hatua za dharura kupambana nao kwa kuhakikisha vinapatikana vipimo vya
kutosha na dawa.
Wachina walazwa
Taarifa kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dar es
Salaam zilieleza kuwa wagonjwa waliobainika kuugua homa hiyo hadi jana
ni raia hao wa China na Watanzania wachache wenye historia ya kusafiri
nje ya nchi hasa China, Ufilipino na Kusini mwa India.
Muuguzi katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza
cha Aga Khan, Nyangee Lugoe alisema hospitali hiyo ilianza kupokea
wagonjwa tangu Machi mwaka huu na kuanzia Aprili, raia wengi wa China
wamegundulika kuwa na homa hiyo, ingawa baadhi walitibiwa na kuruhusiwa.
Agizo la Rais Kikwete
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi
Duniani huko Arusha, Rais Kikwete alisema: “Hili ni jambo la dharura la
kitaifa lazima hatua muafaka zichukuliwe kudhibiti ugonjwa huu, ambao
asili yake ni nchi za Asia na Bara la Amerika.”
Alisema dalili za ugonjwa huo ambao unasababishwa
na mbu aina ya Aedes Egyptie anayeuma mchana ni homa kali ya kuumwa
kichwa, maumivu ya viungo na kutoka damu puani na kwenye fizi na
kupoteza fahamu.
“Napenda kutoa wito mtu yoyote ambaye atapata
dalili za ugonjwa huu, aende mara moja hospitalini ili afanyiwe vipimo
badala ya kunywa dawa,” alisema.
Tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imetangaza kuanza kuchukua hatua za dharura kukabiliana na ugonjwa huo,
ikiwa ni pamoja na uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuchukua
tahadhari.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Charles Pallangyo
alisema jana kuwa wizara yake imetoa hadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa
waganga wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini na itatoa mafunzo maalumu
kwa watumishi wa afya ikiwajumuisha madaktari na mafundi maabara ili
kuwajengea uwezo.
Post a Comment