NILIHITIMU masomo yangu ya kidato cha nne miaka 19 iliyopita katika
Shule ya Sekondari ya Nyakato, iliyopo mkoani Kagera. Nakumbuka mengi
katika shule hii iliyopo umbali wa kilometa saba hivi kutoka mjini
Bukoba.Kwa wale waliosoma shule za sekondari za Mkoa wa Kagera,
ulio pembezoni mwa Ziwa Victoria enzi zetu, waliotutangulia na wale
waliofuata miaka mitano hivi baada yetu, ukitaja Nyakato watakumbuka pia
shule kama Kahororo, Ihungo, Rugambwa, Bukoba Sekondari na kidogo
Bugene.
Ni shule ambazo zilikuwa na sifa za aina yake, zikiwa na
baadhi ya mambo, ambayo yalizifanya zifanane, siyo kwa bahati mbaya, la
hasha, bali kutokana na mipango iliyokuwa ikipangwa na wakuu wa shule
hizo na bodi husika.Shule kama Nyakato nilikosoma mimi, ilikuwa
ni taasisi kamili ya elimu. Kulikuwa na utaratibu wa kishule
uliojitosheleza kuanzia madarasa, mabweni, viwanja vya michezo, ofisi za
walimu, maabara za masomo ya sayansi, ofisi za viongozi wa wanafunzi,
maabara, stoo za kutunzia vifaa, vyoo, ukumbi wa chakula (bwalo) na hata
mashine ya kusukumia maji.
Kwa upande wa ratiba ya siku,
halikuwa ni jambo la dharura au bahati mbaya, kila kitu kilikuwa wazi.
Kwamba siku ya kukimbia mchakamchaka ilifahamika, taratibu za kufanya
usafi kwa ujumla wake ulifahamika, muda wa kuingia madarasani
ulijulikana, siku za kazi zilikuwa wazi na hata siku za michezo
ziliheshimiwa.Nakumbuka mradi wa ukarabati wa shule uliokuwa
ukifadhiliwa na Serikali ya Denmark kupitia shirika lake la misaada
DANIDA, (Elimu DANIDA – School Maintenance Project). Kupitia mradi huu,
shule hizi za Serikali zilifanyiwa ukarabati wa hali ya juu.
Mabati
yalibadilishwa, umeme uliwekwa, mifumo ya maji ilijengwa na mengine
kadha wa kadha. Kwa hakika DANIDA ilizirejesha shule zetu katika hadhi
yake. Shule zikawa mahali siyo pa adhabu, bali mahali panapokalika
kutokana na mazingira yalivyokuwa.Baada ya kumaliza kazi yao ya
ukarabati, ambao haujapata kufanywa tena katika shule zetu za Serikali,
DANIDA kabla ya kuondoka walianzisha programu ndogo, iliyoitwa Regular
Preventive Maintenance (RPM), ambayo lengo lake lilikuwa ni kuwezesha
utunzaji wa mazingira na kulinda ukarabati walioufanya.
Kupitia
RPM kulikuwa na mashindano ya kimkoa, kwamba ni shule gani ambayo
wanafunzi wake wanaweza kulinda vizuri mazingira yao. Yalikuwapo
mashindano ya kikanda, yaliyozihusisha shule zote za mikoa ya Kanda ya
Ziwa.Chini ya RPM baadhi yetu tulipata kutembelea Shule za
Sekondari za Bwiru Wavulana na Bwiru Wasichana, lengo likiwa ni
kujifunza wenzetu walivyokuwa wakimudu kufanya vizuri, licha ya kwamba
mazingira yao hayakuwa rafiki kama yetu.
Nakumbuka Bwiru
Wasichana ni shule iliyokuwa ya kupigiwa mfano, kutokana na jinsi
mabinti wale walivyokuwa wasafi na jinsi walivyokuwa na uwezo wa kutunza
mazingira ya shule yao.Nakumbuka moja ya maajabu tuliyoyaona
wakati ule ni uwezo wa wanafunzi wa Bwiru Wasichana kuweka udongo juu ya
mawe na kupanda maua juu ya mawe hayo.
Tulipokuwa tukirejea
shuleni kwetu, tulijadiliana kuhusu kile tulichokiona katika ziara zetu
na kushauri jinsi tunavyoweza kusonga mbele.RPM siyo mpango
uliopendwa na wananfunzi, kwani tunafahamu kwamba tuwapo shuleni wengi
wetu hatukupenda kazi, lakini mazingira ya shule na uhalisia wa maisha
ulitufanya kuuchukulia mpango ule kuwa sehemu ya maisha yetu ya shule.
Yako
mengi ya kusimulia, lakini niseme kwamba nimeeleza machache tu na kwa
haraka kila mmoja anaweza kukumbuka shule alikosoma, iwe ni shule ya
Serikali au ya binafsi. Hali ilikuwaje? Maisha ya wanafunzi yalikuwaje,
ratiba za vipindi, walimu je? Na mambo mengine kama hayo.Tukizigeukia
shule zetu hii leo, tunaona kitu gani? Tukiachana na shule za binafsi,
hata hizi za Serikali ambazo zilisaidiwa ukarabati wake, zikoje sasa?
Wakuu
wa Shule kama akina Samuel Lutanjuka aliyekuwa Nyakato na baadaye
Ihungo, walimudu usimamizi wa shule kwa viwango hivi miaka 20 iliyopita,
leo hii ina maana Serikali haina watu wa aina hii? Kimetokea nini?Shule
ziko katika hali mbaya, siyo kimajengo tu bali hata mazingira yake ni
hatarishi. Kwa wale tuliosoma safu ya mada ya Jumamosi siku chache
zilizopita kuhusu mazingira ya sasa ya Shule ya Moshi Ufundi (Moshi
Technical) mtakubaliana na ninachokisema.
Shule ile ambayo
ilipata kuvuma sana katika nchi hii, leo iko taabani. Mkuu wa shule na
walimu wake anaotamba kwamba wapo zaidi ya 80 wameshindwa kabisa
kuisimamia. Shule iko katika mazingira machafu ya kupindukia. Hapa
tatizo siyo fedha, bali ni uzembe au udhaifu wa kupindukia.
Zipo
shule nyingi ambazo leo hii tukizitazama tunaweza kulia machozi. Hazina
hadhi tena ile ya kwanza, zimetelekezwa na zimekuwa kama watoto
yatima. Tukumbuke Kantalamba, Maswa Wasichana, Shy Bush, Mirambo,
Tabora Wavulana na Wasichana, Kilakala, Galanos, Ndanda na nyingine
nyingi.
Serikali iamke na kuchukua hatua sasa, mawaziri wetu
wakumbuke walikosoma na wachukue hatua. Msipofanya hivyo, tutabaki na
magofu.
Makala kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz/kolamu/Siasa-wiki-hii/-/1614818/1618042/-/tx3b6j/-/index.html
Loading...
Post a Comment