RAIS Mtaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amesema Bara la Afrika
linapaswa kudhibiti utoroshaji wa rasilimali zake kwenda nje ya bara
hilo, kwani ni moja ya sababu za maisha ya watu wake kuendelea kuwa
duni.Rais Mbeki alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa
taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa rasilimali zenye thamani zaidi ya
Dola za Kimarekani Bilioni 50 hutoroshwa kila mwaka kutoka nchi za
Afrika na kwenda kuwanufaisha watu wengine nje ya bara hilo.“Taarifa
zinaonyesha kuwa rasilimali zenye thamani zaidi ya Dola za Kimarekani
Bilioni 50 hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya Afrika, lakini kwa
mtizamo wangu mimi ni kwamba thamani halisi inaweza kuwa hata mara mbili
(Dola za Kimarekani Bilioni 100) kwa mwaka,”alisema Mbeki.
Mbeki alikuwa akizungumza kwenye mjadala kuhusu
“uongozi wenye malengo kwa ajili ya mabadiliko ya Afrika” ulioandaliwa
kwa pamoja baina ya taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) ya hapa
nchini na Mbeki Faoundation ya Afirka Kusini.
Kiongozi huyo alisema utoroshaji wa rasilimali
hizo ni matokeo ya udhahifu katika usimamizi wake, na kwamba lazima
Serikali za Afrika zichukue hatua kudhibiti utoroshaji huo.
Kauli ya Mbeki imekuja wakati Tanzania ikiwa
katika mjadala mkali kuhusu taarifa kwamba baadhi ya vigogo wameficha
mabilioni ya fedha nchini Uswisi, hivyo kuwapo shinikizo la kutaka
wahusika watajwe na fedha hizo zirejeshwe nchini.Taarifa hizo ziliibuliwa na mapema mwaka huu na
baadhi ya vyombo vya habari likiwamo Gazeti hili na baadaye ilibainika
kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27 wakiwemo wanasiasa na
wafanyabiashara. Gazeti hili pia lilibaini kwamba mmoja wa walioficha
fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6
bilioni).
Katika uchunguzi wake, Mwananchi imebaini pia kuwa
kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni
jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (Karibu Sh300 bilioni) kwa viwango
vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo
anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne, ambapo anayefuatia
anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine Dola 20 milioni (Sh32
bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki Dola 10 milioni (Sh16
bilioni).
Chanzo : Gazeti la Mwananchi
Chanzo : Gazeti la Mwananchi
Post a Comment