Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza
furaha na shangwe yake kufuatia ushindi wa jana, Jumanne, Novemba 6, 2012 wa
Rais Barack Obama wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.
Katika
salamu zake za pongezi kwa kiongozi huyo wa Marekani ambaye amechaguliwa tena
na wananchi wa nchi hiyo kwa kipindi cha pili, Rais Kikwete amesema mapema leo,
Jumatano, Novemba 7, 2012:
“Nimepokea
kwa furaha na shangwe habari za kuchaguliwa tena kwako kuwa Rais wa Marekani
kwa kipindi cha pili. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukutumia wewe na
kupitia kwako Chama cha Democratic pongezi nyingi kwa ushindi wako wa maana
sana.”
Ameongeza
Rais kikwete katika salamu zake hizo: “Kuchaguliwa kwako tena kuendelea kuongoza
nchi yako muhimu na wananchi wake, ni ishara ya wazi ya uaminifu na imani
ambayo wananchi wa Marekani wanayo katika uongozi wako wa mfano.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Wakati unajiandaa kuchukua tena uongozi wa nchi hiyo katika kipindi
chako kipya, napenda kukuhakikishia msimamo wangu binafsi na ule wa Serikali
yangu kuwa tutaendelea kufanya kazi kwa karibu kabisa na wewe na Serikali yako
ya kutukuka, ili kuendeleza uhusiano bora ulioko kati ya nchi zetu mbili
ndugu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
7
Novemba, 2012.
Post a Comment