Katika
maongezi mengi watu wamekuwa wakisema na kujiaminisha kauli kama hizi,
“Tumia fedha kupata fedha”, “Siwezi kuanza biashara wakati sina fedha”,
“Bila chochote ni vigumu kupata kitu”, “Wenye fedha ndio wanaofanikiwa”
na nyingine nyingi zinazofanana na hizo. Kiharaka haraka kauli kama hizo
zinaonekana kuwa sahihi na zinazokubalika, lakini zina sumu kubwa sana
katika maendeleo ya mtu anayehitaji kuanza ama anaeendelea na juhudi za
kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza kipato.
Ninapoendelea
ngoja nitoe kisa kimoja kutoka katika Biblia. Historia ya Wana wa
Israeli inaonesha kuwa kuna wakati wakiwa utumwani Misri kulitokea
mabadiliko ya kiutawala baada ya Farao aliyekua anawatetea kufariki.
Farao
‘mpya’ alikua ni mkorofi na aliwatesa sana kutokana na kuwapa kazi ya
kufyatua matofali ya kujengea mapiramidi yote yanayoonekana pale Misri
hadi leo.
Enzi hizo za mateso akatokea nabii Musa ambae alitumwa na Mungu kuwaokoa
ili awapeleke Kaanani. Harakati za Nabii Musa zilimwongezea chuki Farao
dhidi ya Waisrael na akaapa kuongeza mateso. Awali walikua wakifyatua
matofali kwa kutumia majani yaliyokua yanaandaliwa na wasimamizi
wao(wawakilishi wa Farao).
Baada
ya hasira ya Farao kuwaka akaamuru mambo mawili; mosi, Waisraeli
wasiandaliwe tena majani ya kufyatulia matofali; pili, kila Mwisraeli
aongezewe maradufu idadi ya matofali aliyokuwa akifyatua awali wakati
akipewa majani.
Huu
ulikua wakati mgumu sana kwao hasa ikizingatiwa kuwa tangu wanazaliwa
walijua kua “haiwezekani kufyatua matofali bila kutumia majani”.
Lakini kutokana na adhabu na mateso ya Farao, Waisraeli walitafuta
mbadala na kujikuta wakiendelea na kazi ya kufyatua matofali tena kwa
idadi mpya waliyopangiwa. Kilichowasukuma hadi kutafuta mibadala ilikua
ni adhabu na mateso waliyokuwa waliyopata kwa kushindwa kutekeleza
ufyatuaji wa matofali.
Kutoka katika kisa hicho kuna mambo matatu tunapata.
Mosi,
ili mtu upambane kupata kitu inategemea na nguvu iliyopo nyuma yako
inayokusukuma utafute kitu hicho. Pili, utegemezi unapoondoka akili huwa
inakusanya uwezo usiotumika bado kuhakikisha kuwa unaanza kujitegemea.
Tatu; ‘nguvu ya asili’ (Mungu) huwa inafanya kazi na watu wanaopanga,
kufikiri na kujishughulisha.
Nianze
na nguvu inayokuwepo nyuma ya mtu kutafuta kitu fulani, ambapo kwa hapa
tunaongelea kutafuta fedha. Kuna nguvu mbili zinazoweza kusukuma mtu
kutafuta fedha, ya kwanza ni ile ambayo kwa Kiingereza inaitwa, “Push
Power” na ya pili ni ile inayoitwa “Pull Power”.
Katika
nguvu ya kwanza unasukumwa kuondoka katika mazingira duni, wakati ile
ya pili inakuvuta kuingia katika mazingira bora zaidi hata kama haupo
katika hali mbaya sana kimaisha.
Iko hivi, unaweza kuzaliwa katika mazingira ya umasikini wa kutupwa na
umasikini ukawa unakutesa na kukuumiza kichwa sana.
Unapojaribu
kutoka katika lindi la umasikini unakua ukitumia nguvu ya ‘push power’.
Lakini unaweza ukawa umezaliwa kwenye mazingira ya kawaida ama ya
kitajiri isipokua ukatamani kufanikiwa na kufikia hatua fulani ya
kibiashara ama ya kimaisha. Kitendo cha kuvutwa na mafanikio yaliyopo
mbele yako ndio tunakiita ‘pull power’.
Kuna
utafiti nimewahi kuusoma unaoeleza nadharia ya watu wa kabila la
Wakinga na Wachagga walivyofanikiwa katika ujasiriamali. Utafiti huu
ulieleza kuwa wakinga wamekua wakifanikiwa kibiashara kwa kutokana na
‘push power’ wakati Wachagga wanafanikiwa kutokana na ‘pull power’.
Inapotokea
ndani yako ukawa na moja kati ya hizi nguvu kwa kiwango kikubwa na cha
kutosha, ni rahisi na tena inawezekana ukapata upenyo wa kuzalisha fedha
ama kupata mafanikio pasipo kua na fedha. Cha kufahamu ni kwamba, nguvu
hizi hazitokei kwa bahati mbaya isipokua huamuliwa na muhusika
mwenyewe.
Kadiri unavyouchukia sana umasikini ulionao unajenga nguvu ya kukutoa
hapo. Kadiri unavyojenga hamasa ya kupata fedha ama mafanikio makubwa
ndivyo nguvu ya kukufikisha huko inavyojengeka ndani yako. Ukijua
unapoelekea ni rahisi kutafuta njia ya kukufikisha huko.
Nitoe mchapo mwingine unaonihusu mimi mwenyewe.
Kiujumla
tangu zamani nilitokea kuyachukia sana mazingira ya ukawaida wa
kiuchumi katika familia niliyozaliwa. Hii ilijenga nguvu kubwa sana ya
kunifanya nipambane kujikwamua na hali ile. Wakati fulani huko nyuma
nilidhamiria kununua basi dogo kwa ajili ya biashara ya usafirishaji wa
abiria. Wakati ninapata wazo hilo, mfukoni mwangu nilikua na shilingi
laki nane tu.
Gari
nililotaka kununua lilikua la milioni tisa; sikua na rasilimali
nyingine yeyote wala rekodi za kibenki kuniwezesha kupata japo mkopo.
Nilichofanya niliorodhesha majina ishirini ya watu ambao nitawafuata na
kuwaeleza mpango wangu wa biashara kisha kuwakopa fedha za kuwezesha
biashara hii.
Kila
jina moja nilipanga kukopa shilingi milioni mbili.
Niliweka majina 20 kwa sababu nilitambua kuwa wengi wao hawatanipa
milioni mbili zote, wapo watakaonipa pungufu na wapo ambao hawatanipa
kabisa. Ndivyo ilivyotokea kuna walioniazima milioni, wapo walionipa
elfu hamsini na kuna walioniambia hawana kitu lakini katika orodha hiyo
wapo walionikatisha tamaa wakidai, ninaota ndoto za mchana kuwaza
kununua gari tena la biashara!
Katika kila niliyekua ninaenda nilimueleza hivi, “….nina milioni saba,
nimepungukiwa na milioni mbili.
Ukiniazima
hizo nitazirejesha ndani ya miezi sita/mwaka/mwezi mmoja….”. Wakati
nikifanya ukusanyaji huu nilikua nikitembea na mchanganuo wa biashara
unaoonesha namna biashara hiyo inavyolipa.
Hatimaye nilinunua gari niliyoikusudia na kuanza biashara ya
usafirishaji kwa kutumia shilingi laki nane tu! Hauhitaji kuambiwa
kilichotokea baada ya hapo, kwa sababu nilikua nimejiongezea thamani.
Sitaki
kueleza katika makala haya changamoto zilizonipata baada ya kukamilisha
lengo hili; lakini baada ya hapo mambo yalikua nafuu tofauti na mwanzo.
Kwanza nilipata mtandao wa matajiri wa magari (kwa sababu nilikua na
gari), pili ikawa ni rahisi kumwambia mtu niazime kiasi fulani cha fedha
kwa sababu anajua sio wa kubabaisha na tatu hata taasisi za fedha
zinanza kukugombea kwa sababu unakopesheka.
Mbinu
hii niliitumia mimi na ilileta matunda kwangu. Sikupi ‘garantii’
uitumie kama ilivyo kwa sababu inategemea mazingira uliyonayo, kiwango
chako cha uthubutu pamoja na ukubwa wa nguvu nilizozitaja (push power na
pull power). Lakini kuna mambo nataka uyabaini kutokana na mchapo wangu
huu.
Yapo mambo ambayo unaweza kuyatumia kama bidhaa ya kubadilisha na fedha.
Mambo haya yanajumuisha, mahusiano mema na watu, taarifa sahihi, utu
wema, umaarufu, uaminifu unaotambulika na watu, uwezo wako kiakili na
mengine yanayofanana na hayo.
Hata
hivyo lazima ijulikane kuwa suala la kupata mafanikio (katika fedha na
maeneo mengine) ni suala linalohitaji uwekezaji endelevu wa mwenendo wa
maisha ya kawaida.
Uhusiano na watu unategemea tabia yako kimaisha (upendo, kuwajali watu,
kuwaheshimu n.k), taarifa sahihi zinatokana na kujisomea, kuongea na
watu na kujielimisha. Vile vile uaminifu unatokana na uwakili wako
katika kazi, elimu na mambo mengine.
Mambo
haya yanaweza kukupatia fedha ikiwa utaamua kuyaunganisha na kusudio
lako la kutafuta fedha.
Kwenye mchapo wangu nimesema niliorodhesha watu 20 ambao niliwafuata na
kuomba wanikopeshe fedha. Kilichonipa ujasiri wa kuwafuata ni jinsi
navyoishi nao na ile kujua kuwa wananiamini.
Jambo
la pili nililolitumia ni kuwa na taarifa sahihi kuhusu biashara ya
kusafirisha abiria; kwa maana hiyo wazo langu nilikua naliwasilisha
kiujasiri na uthubutu mkubwa.
Huwezi kuwa unaishi maisha ya ovyo, kama ufujaji wa fedha halafu
utegemee watu wakuamini katika fedha na kukupa mtaji. Huwezi kuwa mvivu
wa kutafuta taarifa (kujisomea, kubadilishana mawazo, n.k) halafu
utegemee kupata ‘deals’ za fedha.
Vile
vile unatakiwa kuwa makini sana na aina ya watu unaohusiana ama
kuwasiliana nao. Haiwezekani uwe unafanya mawasiliano ya ‘ovyo’ kwa
asilimia mia moja kwa kutumia simu ama mtandao wa kompyuta halafu
utegemee kukutana na watu wa maana. (potential people).
Vile vile katika kutafuta fedha ni muhimu sana mtu kuachana na
visingizio, kwa sababu visingizio ni matokeo ya kukata tamaa hata kama
muhusika hujitambui.
Kila
mtu mahali alipo ana fursa fulani ambayo bado hajaitumia inayoweza
kumwezesha kuzalisha fedha. Si lazima fedha uione kwa macho, si lazima
uishike mkononi, na si lazima uikamate siku hiyo hiyo; lakini unaweza
kuibua mazingira ama mawazo yatakayokuwezesha kuzalisha fedha.
Kule kwenye kisa cha Wanaisraeli nimetaja jambo la pili ambalo ni akili
kutumia uwezo usiotumika bado inapotokea utegemezi umeondolewa.
Watu
wengi wamekua wakiishi kwa utegemezi ndio maana kuna mambo wanakwama
ikiwemo kutafuta fedha. Kwa bahati mbaya suala la utegemezi linahusisha
fikra, ndio maana kuna mtu anaweza kuwa ameondolewa utegemezi lakini
bado akawa hajafunguka kutokana na kutofunguka kifikra na kimawazo.
Albert
Sanga ni mfanyabiashara, mchambuzi & mshauri wa biashara na
uchumi. Pia ni mwanasafu wa ANGA ZA UCHUMI & BIASHARA katika gazeti
la Jamhuri linalotoka kila Jumanne, nchini Tanzania. Maskani yake ni
mjini Iringa.
Kwa hisani ya : Mjengwa Blog
Loading...
Post a Comment