MAZISHI ya Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi yalifanyika jana katika
Kijiji cha Busoka kilichoko wilayani Rungwe, Mbeya na kuhudhuriwa na
mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa. Katika mazishi hayo, viongozi hao wawili kila mmoja
alitangaza kuwasomesha watoto wa marehemu Mwangosi ambaye alifariki
dunia Septemba 2, mwaka huu baada ya kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa
ni bomu wakati polisi walipokuwa wakisambaratisha mkutano wa Chadema.
Akitoa
salamu zake katika mazishi hayo, Profesa Mwandosya alisema yupo tayari
kumsomesha mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Mwangosi, Nehemia ambaye
anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali.
Alisema
atamsomesha mtoto huyo kidato cha tano na sita na ikiwa atafaulu na
kukosa mkopo wa elimu ya juu, atamsomesha mpaka atakapomaliza elimu yake
ya juu.
Dk Slaa kwa upande wake, alisema amewasiliana na rafiki
yake ambaye yupo tayari kuwasomesha watoto wawili wa Mwangosi ambao wote
wapo shule ya msingi. Mtoto wa mwisho wa marehemu hajaanza masomo.
Pamoja na kuwasomesha watoto hao, alisema Chadema kimetoa Sh2 milioni za rambirambi kutokana na msiba huo.
Vijembe msibani
Awali,
Profesa Mwandosya na Dk Slaa walitoa kauli zinazoonyesha kupigana
vijembe vya kisiasa, baada ya waziri huyo kumtaka Dk Slaa aache kufanya
kampeni za kuingia Ikulu mwaka 2015 msibani.
Kauli hiyo ya Profesa
Mwandosya ilikuja baada ya Dk Slaa kutaka polisi waliohusika na mauaji
hayo wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanajulikana.“Tunashangaa
wamekamatwa watu wengine na kuwaacha waliohusika na mauaji hayo,
tunawajua kwa sababu wameonekana hadharani, hakuna siri kwa hilo,”
alisema Dk Slaa.
Akizungumza baada ya kauli hiyo ya Dk Slaa,
Profesa Mwandosya aliwataka wanasiasa wa vyama vya upinzani kuacha
kutumia misiba kutafuta kura za urais mwaka 2015.“Natoa pole
sana kwa familia na tasnia nzima ya habari nchini. Hiki ni kipindi
kigumu, lakini tuviachie vyombo husika vifanye uchunguzi wa mauaji
haya,” alisema Profesa Mwandosya na kuongeza:
“Lakini nichukue fursa
hii kuwaomba wanasiasa waache kutumia misiba ili kujipatia umaarufu
katika kutafuta kura za urais mwaka 2015.”Katika mahubiri yake
msibani hapo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Busoka, Mathayo Mwanjemele alikemea mauaji hayo na kuwaomba
wahusika wajitokeze hadharani kabla Mungu hajawaumbua.
“Waliohusika na mauaji haya wajitokeze na kutubu kwa wananchi kabla adhabu ya Mungu haijawakuta,” alisema.
Alisema ufike wakati Serikali iwe inakiri uzembe unaofanywa na watendaji wake ambao umekuwa ukitokea mara kadhaa.
IGP Mwema asimamia uchunguzi
Kabla
ya mazishi hayo, mwili wa Mwangosi ulifanyiwa uchunguzi na wataalamu wa
afya kutoka Dar es Salaam, huku IGP Said Mwema akishuhudia.Baada ya kumalizika uchunguzi huo, usiku mwili wa marehemu ulisafirishwa kuelekea Mbeya kwa mazishi.
Mwili
huo ulipofika Tukuyu, umati mkubwa ulijipanga barabarani na kupunga
mkono, huku wengine wakiusindikiza kwa baiskeli na pikipiki hadi
kijijini, Busoka.
Majeruhi wengine
Akizungumzia tukio hilo,
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mafinga, Dk Peter Mwenda alisema mbali
na marehemu Mwangosi, watu wengine 10 walijeruhiwa, wawili kati yao
walitibiwa na kuruhusiwa. Alisema waliobaki hospitalini hapo hali zao
zinaendelea vizuri.Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Hussein Kweha
(27), Edson Iddy (22), Alfred Kibitanyi (27), Hamad Musa (37), Yeremia
Kulwa (45) na Christopher Pesa (30).Alisema majeruhi hao walidai
kwamba walikuwa katika mkutano wa ndani wa Chadema na askari waliwataka
kutulia kabla ya kuwashambulia kwa marungu na vitu vyenye ncha kali.
Chanzo kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/25972-mwandosya-slaa-wagawana-watoto-wa-hayati-mwangosi.html
Post a Comment