HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 AGOSTI, 2012
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kila mwisho wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa taifa letu na watu wake. Leo nina
mambo mawili ya kuzungumza nanyi. Lakini, kama ilivyo mazoea yetu
hatuna budi kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wetu, kwa
kutujaalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezesha kuwasiliana leo
tarehe 31 Agosti, 2012.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa
ya Watu na Makazi lililoanza tarehe 26 Agosti, 2012 ambalo linatarajiwa
kumalizika tarehe 01 Septemba, 2012. Mtakumbuka kuwa tarehe 25 Agosti,
2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze kwa wingi na muwape
ushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa watakapopita majumbani mwenu
kutekekeza wajibu wao. Tumebakisha siku moja kufikia kilele cha sehemu
ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Napenda kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu wote
kwa kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa. Mpaka sasa mwelekeo ni mzuri na
ugumu ulioonekana kuwepo pale
mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi siku kadri utekelezaji wa zoezi
ulivyokuwa unaendelea. Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwa
Sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote
ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo. Naomba waitumie siku moja iliyosalia
yaani tarehe 1 Septemba, 2012 kufanya hivyo. Aidha, namuomba
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya Muungano na
Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa
kasoro zo zote zilizopo mahali po pote zinatafutiwa ufumbuzi ili mambo
yakamilike bila upungufu wowote.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kazi ya Makarani wa
Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, tarehe 2 Septemba, 2012,
linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu ambao watakuwa bado
hawajahesabiwa. Itakuwepo fursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa.
Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa Wenyeviti wao wa
Serikali za Mitaa au Vijiji. Taarifa hizo zitafikishwa kwa Kamishna wa
Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la
kuhesabu watu litakuwa limefika mwisho. Yule ambaye atakuwa hakutumia
fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katika hesabu ya Watanzania
ya mwaka 2012. Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu
kutumia siku ya tarehe 1 Septemba, 2012 kuhesabiwa na kama hapana budi
basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa Mwenyekiti wako wa Mtaa au
Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku hiyo ili nawe ujumuishwe.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kazi ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili
kufikia mwisho, itaanza kazi ya uchambuzi na kuunganisha takwimu na
taarifa zilizokusanywa. Kazi hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitaji
umakini na uangalifu wa hali ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la
Sensa litaingia dosari. Nafarijika kuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa
na Wakuu wa Idara za Takwimu za Serikali zetu mbili, kwamba wanatambua
ukweli huo na wajibu wao. Wameniarifu kwamba kama mambo yatakwenda kama
ilivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi
ya watu na jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa
nyingine zitafuata baadaye. Narejea kuwasihi Watanzania wenzangu kuwapa
nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupate matokeo
yaliyo sahihi.
Mpaka na Malawi
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu
mpaka baina ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwa
miaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe.
Sisi, Tanzania, tunasema mpaka upo katikati ya ziwa wakati wenzetu wa
Malawi wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande wa Tanzania. Kwa
maneno mengine wanasema ziwa lote ni mali ya nchi yao.
Utata kuhusu mpaka wetu katika Ziwa Nyasa haujaanza leo. Ulikuwepo
tangu wakati nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na
kuendelea baada ya Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa. Jambo kubwa lililo
tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamua kukaa
mezani na tunalizungumza suala hilo.
Chimbuko la Mzozo
Ndugu Wananchi;
Chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina ya nchi zetu mbili
jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, ni makubaliano baina ya
Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetu yaliyofanywa
tarehe 1 Julai, 1890. Makubaliano hayo yajulikanayo kama Mkataba wa
Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland Treaty) yalitiwa saini kule
Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na Wajerumani. Wakoloni
hao walikubaliana kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na
wakoloni wengine waliopakana nao. Kwetu sisi hayo ndiyo makubaliano
yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake.
Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na Wajerumani walikubaliana kuwa
mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa
nchi ya Malawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpaka ulikuwa ufukweni upande
wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Katika kipengele cha Sita (Article VI) cha Mkataba huo, wakoloni
hao walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali po pote kama
itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi
ya mahali hapo. Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho
mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa. Ilianzia kazi katika Mto Songwe
kuhakiki mpaka baina ya nchi yetu na Malawi. Tume ilikubaliana kuhamisha
mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati
ya mto. Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika, mwaka 1901
mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.
Tume iliendelea na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha
mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa
mwaka 1910. Tume iliendelea katika ziwa Jipe ambapo mpaka ulihamishwa
pia hadi katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Bahati mbaya Tume hiyo haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia
kati ya mwaka 1914 – 1918. Kama tunavyokumbuka, Waingereza na
Wajerumani waligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini. Baada ya
vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa (The
League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika. Hivyo,
Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.
Ndugu Wananchi;
Wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya
Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na kazi. Matokeo yake,
mwaka 1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891
ulioweka mpaka wa Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani
kwenye ufukwe wa Msumbiji, na kuuhamishia katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kustaajabisha ni kuwa, Waingereza walioona umuhimu na
busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi na Msumbiji, hawakuona
umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi. Inashangaza, kwa
sababu wakati huo Uingereza ilikuwa mtawala wa nchi zetu mbili hivyo
kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi, lakini hawakufanya hivyo. Na, baya
zaidi ni kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotaka kupatiwa
ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa.
Watu walitaka ufafanuzi kwa sababu inasemekana kati ya mwaka 1925 na
1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa ziliweka mpaka katikati
ya ziwa. Lakini, kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala la mpaka wa Malawi lilijitokeza
tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati ule lilijulikana kuwa
Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO). Hoja ya
Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpaka kuwekwa kwenye ufukwe wetu
kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kando kando ya ziwa haki
yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samaki na kupata
manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya Serikali ya
Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana wakati ule. Hoja
iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya Tanganyika ijadiliane na
Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa Uingereza ili
ufumbuzi upatikane. Wakoloni hawakujali na wala hakuna hatua
zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuru wake tarehe 9 Desemba,
1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.
Juhudi za Kubadili Mpaka wa Ziwa Nyasa Baada ya Uhuru
Ndugu Wananchi;
Wakati tulipopata Uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu
mpaka wa Tanganyika na Malawi uliendelea Bungeni, ambapo ilitolewa hoja
kwamba zifanyike juhudi za makusudi za kuanzisha na kuendeleza
mazungumzo ya kurekebisha mpaka huo kwa manufaa ya wananchi wote
wanaoishi pembezoni mwa ziwa. Iliamuliwa kwamba tusubiri mpaka wenzetu
wa Malawi wapate uhuru ili yafanyike mazungumzo baina ya nchi mbili
huru. Kulijengeka matumaini kuwa mambo yangekuwa rahisi. Bahati mbaya
haikuwa hivyo na kwamba mambo yakageuka na kuwa magumu na ya uhasama.
Miaka mitatu baada ya Malawi kupata Uhuru wake (1964), kunako tarehe 3
Januari 1967, Serikali ya Tanzania iliandika barua kwa Serikali ya
Malawi kuelezea tatizo la mpaka wa ziwani na kupendekeza nchi zetu mbili
zizungumze na kulitafutia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri tarehe 24 Januari, 1967, Serikali ya Malawi ikajibu
kukiri kupokea barua hiyo na kuahidi kuwa itatoa majibu baada ya muda si
mrefu. Hata hivyo, tarehe 27 Juni, 1967, Rais Kamuzu Banda
akilihutubia Bunge la Malawi, alikataa maombi ya Tanzania. Alisema
hayana msingi na alidai kuwa kihistoria Songea, Mbeya na Njombe ni
sehemu ya Malawi. Hivyo basi, mazungumzo yakafa.
Tanzania haikukata tamaa. Alipochaguliwa Rais wa Pili wa Malawi,
Mheshimiwa Bakili Muluzi, juhudi zilifanyika lakini nazo hazikufika
mbali. Bahati nzuri tarehe 9 Juni, 2005, Rais wa Tatu wa Malawi,
Mheshimiwa Bingu Wa Mutharika, ambaye sasa ni marehemu, alimuandikia
barua aliyekuwa Rais wa nchi yetu wakati ule, Mheshimiwa Benjamin
William Mkapa, kushauri nchi zetu zifanye mazungumzo kuhusu mpaka wa
ziwani. Alipendekeza iundwe Tume ya Pamoja itakayojumuisha Mawaziri na
Wataalamu kutoka nchi zetu mbili. Tume hiyo itatoa mapendekezo kwa
Marais wa nchi zetu mbili ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina
yao. Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuwa ilikuwa kipindi cha mpito kuelekea kuchaguliwa Serikali ya
Awamu ya Nne, Rais Benjamin Mkapa hakuwahi kuishughulikia barua hiyo.
Nilipoletewa barua hiyo nikaijibu kukubali ushauri na mapendekezo yake.
Aidha, nilipendekeza Wizara na Idara zipi za Serikali zetu
zishirikishwe katika Tume hiyo. Bahati nzuri Rais wa Malawi alikubali
mapendekezo yangu pamoja na lile la kwamba Malawi waitishe mkutano wa
kwanza wa Tume hiyo.
Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa mikutano mitatu ya Tume ya Pamoja imeshafanyika, wa
kwanza ulifanyika tarehe 8 – 10 Septemba, 2010. Mkutano wa pili
ukafanyika tarehe 27 – 28 Julai, 2012 hapa Dar es Salaam na wa tatu
ukafanyika Mzuzu na Lilongwe tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Hatua kadhaa
zimepigwa lakini bado muafaka haujapatikana kwa maana ya madai yetu ya
kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa na madai yao kuwa mpaka ubaki ufukweni
kwetu kama ilivyo kwenye Mkataba wa Heligoland wa Julai 1, 1890. Hoja
ya wenzetu ni kuwa huo ndiyo mpaka tuliorithi wakati wa uhuru.
Wanataka tuthibitishe hivyo na kwamba tuzingatie kauli ya OAU ya
kuheshimu mipaka tuliyorithi kwa wakoloni. Wananukuu kauli ya Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisisitiza hoja hiyo katika mkutano wa
OAU mwaka 1963.
Hoja za Msingi za Kutaka Mpaka Uwe Katikati ya Ziwa
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu tumekuwa na hoja kadhaa za kutaka mpaka uwe
katikati ya ziwa. Ya msingi kabisa ni ukweli kwamba Mkataba wa
Heligoland umekosewa kwa kuamua kuwanyima wananchi wa Tanzania wanaoishi
ufukweni mwa ziwa haki yao ya msingi ya kutumia maji na rasilimali
zilizomo katika Ziwa Nyasa. Zipo sababu kadhaa kwa upande wetu kudai
hivyo. Mojawapo ni sheria ya kimataifa inayoelekeza kwamba po pote
kwenye maji ya asili kama vile ziwa na mito iliyopo kati ya nchi mbili
mpaka huwa katikati. Ndiyo utaratibu unaotumika duniani kote, na mifano
iko tele. Kwa nini iwe tofauti katika ziwa Nyasa na kwa upande wa
Tanzania tu wakati kwa upande wa Msumbiji mpaka upo katikati ya ziwa?
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mto Songwe, mpaka baina ya nchi zetu mbili upo
katikati. Iweje hapa kanuni hiyo itambulike na kuheshimiwa lakini isiwe
hivyo ziwani? Kama nilivyoeleza awali, mwanzoni Mto Songwe wote
ulikuwa umewekwa upande wetu, lakini Tume ya Mipaka iliyoundwa mwaka
1898 ilifanya marekebisho na kuweka mpaka katikati ya mto. Kama
nilivyokwishagusia kwenye ziwa hilo hilo la Nyasa kwa upande wa Msumbiji
mwaka 1954 mkataba wa mwaka 1891 ulioipa Malawi ziwa lote ulirekebishwa
na mpaka kuwekwa katikati. Kwa nini isifanyike hivyo hivyo kwa upande
wa Tanzania? Hivi hasa ni kipi ambacho wenzetu wa Msumbiji
walichotuzidi na kustahili kupata haki yao ya msingi ya kumiliki na
kutumia maji ya Ziwa Nyasa ambacho sisi Tanzania tumepungukiwa?
Ndugu Wananchi;
Maji ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wake, waitumie kwa
uhai na maendeleo yao. Iweje leo, kwa watu wanaoishi pembeni mwa ziwa
hilo hilo wengine wapewe na wengine wanyimwe haki ya kulimiliki na
kulitumia? Kwa nini wanyimwe haki ya kunufaika na zawadi hiyo? Hivi
kauli ya wakoloni waliokaa Berlin ya kusema fulani apate na fulani
asipate inatosha? Hivi kweli ni rahisi kiasi hicho?
Mpaka wa kwenye maji ni tofauti na ule wa nchi kavu. Huu una
rasilimali ambayo huwezi kuamua kumnyima mwanadamu mwingine anayeishi
pembeni yake kwa vile haina badala yake. Unapowaambia watu wa Mbamba
Bay, Liuli, Lituhi, Manda, Ngonga, Matema, Mwaya, Itungi na wengineo
waishio kando ya ziwa kuwa maji hayo si yao bali ni mali ya Malawi
hawakuelewi na watakushangaa sana. Watadhani umechanganyikiwa kwani
tangu waumbwe wamekuwepo hapo wanamiliki na kutumia maji ya Ziwa.
Unataka wafanyeje? Waende Malawi kuomba kibali cha kuyatumia? Wao
watakuuliza swali moja tu “hivi hao wenzao wanaoishi ng’ambo ya pili
wamewazidi nini katika ubinadamu wao hata wapewe maji yote na wao
wanyimwe?”
Ndugu Wananchi;
Kwa maana halisi ya Mkataba wa Heligoland tangu tarehe 1 Julai,
1890, wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwa wanakunywa, kuoga, kuvua
samaki na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yao bali ya nchi
nyingine. Na kwa kuwa wamekuwa wanafanya hivyo bila ya kupata kibali
cha Malawi wamekuwa wanaiba maji na samaki wa Malawi na kusafiri isivyo
halali katika nchi ya watu. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo.
Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.
Ndugu Wananchi;
Na hiyo pia, ndiyo maana, busara na hekima ya Sheria ya Kimataifa
kuhusu mpaka wa kwenye maji kuwa katikati. Sheria hii inazingatia
hali halisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo imekuwa
inalitegemea maisha yao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai na
maendeleo yao. Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kando ya Ziwa
Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake. Hawataelewa
wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumia maji na rasilimali za ziwani kwa
hisani ya nchi ya Malawi.
Kwa watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumba wao na wenzao wa ng’ambo
ya pili, siyo sawa na siyo haki hata kidogo kuwafanyia hivyo. Kwe
kweli ni unyanyasaji wa hali ya juu. Ndiyo maana wazee wetu walidai
suala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru. Na
ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zao katika madai haya ya haki.
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanya tudai haki ya kumiliki
na kutumia Ziwa Nyasa. La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya
Tanzania nayo inachangia kujaza maji katika ziwa. Iweje leo maji
yanayojaza ziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani, ziwa hilo si
mali yao wenye mito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali ya watu
wengine. Hivi kweli ndivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza
vyanzo vya mito hiyo na kuruhusu maji yake kutiririka na kuingia ziwani?
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kwamba mpaka wa Tanzania na Malawi kuwa ufukweni
kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikani kwa uhakika. Unategemea
mabadiliko kutokana na kujaa na kupungua kwa maji ziwani. Kunafanya
mpaka wa nchi kuwa hautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya
safari. Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwa wake nalo ni tatizo
la aina yake. Ndiyo maana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishasema, chimbuko la mzozo huu ni mkataba wa
Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina ya nchi zetu. Bahati
mbaya sana Tume ya Mipaka haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya
nchi yetu na majirani zake kufuatia kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka
1914. Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya ya
Uingereza. Bahati mbaya kwetu Waingereza waliotawala nchi zetu mbili
tangu 1918 hawakuchukua hatua za kurekebisha mpaka kabla ya uhuru wa
nchi zetu. Ni maoni yetu kuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho
hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni – Waingereza na Wajerumani.
Tukifanye sisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka 1967 hayakufanikiwa. Bahati nzuri
kufuatia uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi
zetu sasa zinazungumza. Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebisha
mpaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka. Jambo linaloleta
faraja, hata hivyo, ni kuwa sote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu
wa kutusuluhisha.
Ndugu Wananchi;
Hayo ndiyo matokeo ya mazungumzo ya Tume yetu ya pamoja tangu ngazi
ya Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwa Mawaziri, katika vikao vya Mzuzu
na Lilongwe kati ya tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Katika mkutano wao wa
tarehe 27 Agosti, 2012 Mawaziri husika wa nchi zetu chini ya uongozi wa
pamoja wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mheshimiwa Ephraim Chiume
na mwenzake wa Tanzania, Mheshimiwa Bernard Membe, wameafiki mapendekezo
hayo. Aidha, wamekubaliana kuwa pande zote mbili wakutane tena Dar es
Salaam kati ya tarehe 10 – 15 Septemba, 2012 kukubaliana juu ya
usuluhishi wa aina gani unafaa.
Ndugu Wananchi;
Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua muhimu kuelekea kwenye
kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili. Hata hivyo, bado safari ni
ndefu na huenda ikawa na magumu mengi. Maombi yangu kwa viongozi na
wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea kuunga mkono jitihada hizi.
Tuwaunge mkono wataalamu na Mawaziri wetu ili wafanikishe vizuri jukumu
lao. Tuzingatie na kuheshimu walichokubaliana Lilongwe kuwa viongozi
na wananchi wa nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au kufanya vitendo
vinavyoweza kuchafua hali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri
majadiliano yanayoendelea.
Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatia ushauri na rai hiyo ya
Mawaziri na wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuri ya mazungumzo
na kuwezesha mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kusisitiza kuwa si
makusudio yangu wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho la suala hili
kwa nguvu ya kijeshi. Nawahakikishia Watanzania wenzangu kuwa hatuko
vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vita dhidi ya jirani zetu
hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika Ziwa. Ondoeni hofu na
endeleeni na shughuli zenu za ujenzi wa taifa letu kama kawaida.
Nilimhakikishia hivyo Rais wa Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda
nilipokutana naye Maputo, Msumbiji tarehe 18 Agosti, 2012. Tanzania
haina mpango wa kuingia vitani na Malawi. Mimi na wenzangu Serikalini
tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya kukaa na ndugu zetu
Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu sote sasa tumeipata.
Hatuna budi kuitumia ipasavyo. Naamini, tukifanya hivyo, inaweza
kutufikisha pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa ajili hiyo kwa pande zetu
mbili, kuipa fursa ya mazungumzo nafasi ya kuendelea bila ya vikwazo
visivyokuwa vya lazima.
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu hiyo basi , napenda kutumia nafasi hii
kuwasihi ndugu zetu wa vyombo vya habari na wanasiasa wenzangu tuepuke
kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzo na kuchochea uhasama kati ya
nchi zetu mbili jirani na rafiki. Kuna manufaa makubwa ya kumaliza
mzozo wetu kwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita. Kufikiria
sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, si wakati wake
muafaka. Aidha, tukitumia njia ya vita, badala ya kuwa tumepata
suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa mgogoro mpana zaidi. Tuendelee
kuwaunga mkono wawakilishi wetu katika Tume yetu ya pamoja. Naahidi,
Serikali itakuwa inawapa taarifa kadri mazungumzo yetu na wenzetu wa
Malawi yatakavyokuwa yanaendelea. Nina hakika tutamaliza salama.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa Kunisikiliza
Post a Comment