Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa John Gabriel Tupa salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kepteni (mst) James Charles Yamungu kilichotokea alfajiri ya leo, Jumatano, Agosti 22, 2012, kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa.
Katika
salamu hizo, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Tupa, “ Nimepokea kwa
huzuni na mshtuko taarifa za kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Serengeti,
Kepteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mheshimiwa James
Yamungu. “
Amesema
Rais Kikwete katika salamu hizo: “ Kifo cha Kepteni Yamungu
kimeinyang’anya nchi yetu na Serikali yetu mtumishi hodari na mwadilifu
wa umma ambaye katika utumishi wake wote tokea alipokuwa Jeshi hadi
anaingia uongozi wa siasa alithibitisha uaminifu wake kwa nchi yetu na
uongozi wake.”
“Kufuatia
msiba huu mkubwa, nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa
Tupa, salamu zangu za rambirambi, na kupitia kwako naitumia salamu
zangu za dhati kabisa familia ya marehemu, wana-Mara na Wana-Serengeti
wote ambako ndio kwanza alikuwa ameripoti kuanza kazi yake ya ukuu wa
wilaya hiyo,” amesema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Napenda
kuwajulisheni kuwa moyo wangu uko nanyi katika kipindi hiki kigumu.
Nawaombea uvumilivu na subira na naungana nanyi kumwomba Mwenyezi
Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu James
Charles Yamungu. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Agosti, 2012
Post a Comment