Nilipofikiria kuandika makala kuhusu uwezo wa kushawishi watu
wengine wakubaliane na mawazo yetu niliingiwa na shaka kuwa huenda
baadhi ya watu wasione umuhimu wa mtu kuwa na stadi kama hizo. Iwapo
wewe ni miongoni mwa watu wenye fikra hizi, jiulize kama unaweza kuishi
bila kuongea na watu, Je, huwa haitokei ukamweleza mtu au watu mawazo
ambayo ungependelea wayaelewe na kuafikiana na wewe.
Katika maisha yetu ya kila siku tunatoa maelezo
mbalimbali ili kueleza maoni, fikra ama hisia zetu. Mara nyingine wale
tunaoongea nao huwa na mawazo tofauti na yetu. Hakika hufurahi sana
tunapofanikiwa kuwashawishi hadi wakaafikiana na mawazo yetu. Kuna
matukio ambayo hutufanya tuone ni muhimu sana kuweza kushawisha watu
wakubaliane na mawazo yetu. Matukio hayo ni kama tunapokwenda kwenye
ofisi mbalimbali tukiwa na mahitaji kama vile kiwanja cha kujenga
nyumba, nafasi za watoto shuleni, kuunganisha huduma ya maji au umeme
katika nyumba, kuomba mkopo au kazi na maombi mengine .
Ushawishi huweza kuwa muhimu zaidi tunapowaeleza
watoto wafuate maadili, tunapomweleza bosi uzito wa kazi na nakuomba
nyongeza ya mshahara, tunapotoa maelezo katika mashauri mahakama au
tunapowapatanisha ndugu au jamaa waliohitilafiana na kukosana. Kuna watu
wasiyo na uwezo kabisa wa kushawishi. Hivyo, badala ya kunasihi, wao
hutumia mbinu ya kukaripia au kufoka. Ushawishi wa namna hii huwa siyo
wa hiari wala kudumu. Watu wenye uwezo mkubwa wa kushawishi huwa na
haiba kubwa katika maisha. Lakini kila mmoja wetu unaweza kujifunza
jinsi ya kushawishi. Wanafalsafa wamefanya utafiti na kugundua kuwa
uwezo wa kushawishi huweza kujengeka kwa kuzingatia mbinu sita
zifuatazo:-
Kutumia ushawishi katika sehemu uliyozoea
Watu wenye uhodari wa kushawishi huweza kufanya
shughuli hiyo katika mazingira waliyoyazoea. Kanuni hii hutumika katika
utawala. Mameneja hufanya vikao na watendaji wao katika ofisi zao. Kama
unaongea na mtu au kundi ambalo lina sehemu yake na kama haiwezekani
kuzungumzia katika sehemu yako ni vyema zaidi kukutana katika sehemu
isiyo yenu wote.
Kuonekana nadhifu
Kuna watu wanao amini kuwa tunapomsikiliza mtu
akiongea huwa tunavutiwa zaidi na kile anachosema kuliko anavyoonekana.
Jambo hili siyo kweli. Utafiti umeonyesha kuwa watu huvutiwa zaidi na
muonekano wa msemaji kuliko maneno anayosema. Hii ndiyo maana hata
mavazi wanayovaa viongozi wa dini huwasaidia kuongeza ushawishi wa
maneno wanayosema kwa waumini wao. Tunaposhawishi inafaa tuwe nadhifu.
Kujinasibisha na wale tunaowashawishi
Imebainika kuwa unapokuwa ukijaribu kumshawishi
mtu huna budi kumfanya akuone wewe siyo tofauti na yeye na kwamba
unamthamini yeye na mawazo yake. Ni vyema ujenge hoja yako kuanzia
kwenye fikra au mawazo yake.
Kuzingatia uelewa na uzoefu wa unayemshawishi
Watu wenye uzoefu wa kushawishi huzingatia welewa
na uzoefu wa mtu au watu anaokusudia kuwashawishi. Huna budi kuelewa
upeo wa welewa wa mtu unayekusudia kumshawishi ili uweze kumshawishi
vizuri zaidi. Huna budi kuanzia hoja yako kwenye kiwango cha
unayemshawishi na kumchukua taratibu hadi kwenye mawazo yako.
Ni vyema kukumbuka kuwa usipoweza kumweleza mtu au
watu kwa kuzingatia upeo wa welewa wake utakuwa umefanya kazi bure.
Fikiri jinsi wazazi wanavyopata shida ya kuwaeleza watoto wadogo mahali
watoto wanakotoka.
Chanzo gazeti la Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Je-una-uwezo-wa-kushawishi-watu-wengine-/-/1597592/2151734/-/sxuobkz/-/index.html
Chanzo gazeti la Mwananchi
http://www.mwananchi.co.tz/Makala/Je-una-uwezo-wa-kushawishi-watu-wengine-/-/1597592/2151734/-/sxuobkz/-/index.html
Post a Comment