“Ili
kuleta maendeleo Tanzania ni lazima malengo yetu yaelezwe,tusiseme ni kilimo
huku ikiwa bado wakulima asilimia 70 wanatumia jembe la mkono.Tusiseme elimu
huku tukitenga asilimia 1.4% ya bajeti wakati Rwanda wakitenga 5.8% na Kenya
7%? Ukienda Rwanda kila mmoja anafahamu nchi yake inelekea wapi na wajibu wake
ni nini.Kila mmoja anapigana na Rushwa na Kutaka utawala bora.Nchi ambayo kila
mtu na lwake haiwezi kuendelea”.
Imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa nchi za Afrika kuwa na
safari nyingi za ulaya na amerika kwenda kujifunza namna ya kuendelea.Wakirudi
utasikia wakisema,”huko wameendelea sana”,”wametuacha
mbali hatuwezi kuwafikia hivi karibuni”.Hata katika kujifunza kuimudu sekta
ya gesi walienda Sweden na Trinidad na Tobago,lakini nchi ya jirani ya msumbiji
ambako nao wanatekeleza mradi kama wa hapa kwetu hawakukanyaga kabisa.Nadhani
ili tujifunze vizuri ni muhimu tujifunze pia kwa wale tunaofanana nao japo
kidogo kihistoria.
Miaka 19 iliyopita tulishuhudia
nchi ya Rwanda ikiwa katika mauaji makubwa yaliyotikisa dunia.Ni uadui wa
kikabila kati ya walio wengi wahutu na wale walio wachache ila walibahatika
kusoma na kushika madaraka katika nchi,Watutsi.
Ndani ya siku mia moja(100)
yalishuhudiwa mauaji ya kimbari ya watu wapatao karibu laki nane(800,000)
ikimanisha angalau kwa kila siku waliuawa watu wapatao 8000.Nchi ilijaa damu,miundo
mbinu iliharibiwa;shule,hospitali,barabara na viwanda.Ilikuwa ni hali ya
kukatisha tamaa kwa kila mnyarwanda.
Baada ya vurugu hizi kuisha Rais
Paul kagame alichukua nchi kwa mapinduzi akiwa na chama chake cha RFP.Tangu
kuingia kwakwe madarakani nchi hii imepiga hatua kubwa sana kiuchumi na katika
huduma za kijamii.Wakosoaji wa maendeleo ya Rwanda wanatoa hoja kadhaa kuwa
ndiyo sababu ya kuendelea kwao kwa kasi katika kukuza uchumi wao.
Wapo wengine wanaosema nchi ya Rwanda ni ndogo
sana hivyo ni rahisi kuiletea maendeleo,wanasahau hapa kwetu hata katika mikoa
midogo bado maendeleo hakuna.Hata hivyo udogo haiwezi kuwa kigezo cha mandeleo
kwani ziko nchi ndogo zaidi ya Rwanda kama ilivyo shelisheli yenye km za mraba
455 ukilinganisha na zile za Rwanda kilometa za mraba 26,318 au ukubwa wa
Gambia wa kilomita za mraba 11,295 hizi zote ni ndogo kwa eneo kulinganisha na
Rwanda lakini bado Rwanda iko juu kimaendeleo ukilinganisha na nchi hizi.
Mfano huku Rwanda ikiwa uchumi
wake unakua kwa kasi ya 6.5% kwa mwaka nchi ya Gambia uchumi wake hukua kwa
5.2%. Nchini Rwanda kiwango cha elimu kiko 70.4% huku nchini Gambia ikiwa ni
asilimia 40.1%.Na hapa lazima tuzingatie kuwa Rwanda ni zaidi ya mara mbili ya ukubwa wa Gambia na pia ina
idadi ya watu 10,746,300 karibuni mara kumi ya idadi ya watu wa Gambia.Kwa
kuzingatia haya,udogo si hoja ya kujitetea kabisa.
Kuna wale ambao wanataka pia
kuhalalisha kutoendelea kwa nchi yetu Tanzania wakidai kuwa Rwanda wanapata
maendeleo yao kutokana na kupendelewa kupewa misaada lukuki hasa ikitokana na
huruma za mataifa mbalimbali kwa kile kilichotokea mwaka 1994.Hii nayo ni mbinu
ya wavivu wa kufikiri,kwani kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na kijitabu cha
pocket world in figures kinachotolewa na jarida la The economist,ilionyesha
kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza kwa kupewa misaada Afrika mashariki,ya tatu
Afrika na ya sita duniani.Wakati Rwanda ikiwa imepokea misaada ya dola za
kmarekani milioni 785.9 kwa mwaka 2010,Tanzania tulipata msaada wa dola za
kimarekani Bilioni 2.9.Kama misaada ingekuwa ndio chanzo cha maendeleo,Tanzania
tungetakiwa kuwa mbali zaidi.
Wako watu ukianza kulinganisha maendeleo
yetu na yale ya nchi zingine za ulaya au marekani wanakuwa wakali na kusema
hatufanani kabisa.Nadhani watu wenye fikra hii watakubaliana na mimi kama nitailinganisha
Tanzania yenye uhuru wa miaka 50 na Rwanda iliyoanza kujijenga miaka 19
iliyopita.Nchi ya Rwanda ndio inayoongoza kwa kuwa na usafi katika nchi za
Afrika mashariki,hili nalo linahitaji misaada ya nje?
NINI SIRI YA MAFANIKIO YA RWANDA?
Mafanikio ya Rwanda hayatokani na
Jambo moja tu,yako mambo mengi yanayochangia katika maendeleo yao ya kasi yanayotamaniwa
sana na mataifa mengi,leo nitalizungumzia moja.
Siri ya mafanikio ya Rwanda
imejengwa katika UONGOZI MADHUBUTI WENYE MAONO,tangu Rais kagame aingie
madarakani amefanikiwa kuonyesha njia kwa vitendo.Hajaacha mipango yake iwe
ndani ya makaratasi tu,amehakikisha wananchi wote wanaelewa kwa undani maono ya
nchi yao ni nini,na kushikamana katika kuyatekeleza.
Suala la ukabila ambalo ndio
kilikuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya mwaka 1994 alikishughulikia bila kificho
na alifanya hivyo kwa uwazi.Alikemea ukabila akiwa ndani na akiwa nje
pia,hakuna mnyarwanda asiyejua kuwa kagame hakubaliani na sera za
ukabila.Ameonyesha kwa vitendo katika uteuzi wake wa viongozi mbalimbali
pia.Leo hii ni marufuku kwa mnyarwanda yeyote kusema mimi wa kabila Fulani,kila
mmoja anatakiwa ajitambulishe MIMI NI MNYARANDWA.Viongozi wetu hapa Tanzania,ni
lazima pia wafikishe wananchi wao hapo katika suala la udini kama mwalimu Nyerere
alivyolisimamia ili kujenga nchi ya usawa.
Katika maono yake kwa nchi ya
Rwanda ya hadi mwaka 2020,kagame ameelezea jinsi anavyokusudia kuibadilisha
Rwanda kutoka katika nchi ya kutegemea kilimo uchwara na misaada na kuwa nchi
yenye uchumi ulio thabiti na unaotegemea uwekezaji katika elimu na biashara.Maono
haya yanaeleweka kuanzia waziri hadi dereva wa daladala.Kuanzia kiongozi hadi
mwananchi wanazungumza lugha moja na kuwa na msimamo mmoja.Hivi hapa kwetu wote
tunaelewa tunakoelekea?Hiyo vision 2025 inajulikana kwa kiasi gani na kila mtu.Hata
wale waliofika chuo kikuu ukiuliza vision 2025 inaeleza nini asilimia kubwa
watakuuliza,hicho ni kitu gani?badala ya kujadili mwelekeo wan chi yetu
malumbano sasa yamejikita katika siasa na kuharibiana sifa mbele ya jamii(character assassination).
Rais kagame ametengeneza kijitabu
kidogo kinachoeleza kwa undani wajibu wa serikali yake na matarajio yake kutoka
kwa wananchi ikiwemo mambo ya msingi(values) ya utaifa wao.Haya yanafundishwa
kwa kila mtu katika vikao vya ngazi za chini vya wananchi,ni lazima
uyafahamu,uyaishi na uyasimamie.Hii hutengeneza nguvu ya pamoja kuendeleza
taifa lolote.Misingi yetu kama Taifa ni ipi?
Maendeleo ya Rwanda yameanzia
katika fikra na mitazamo,wananchi wamefundishwa kuchukia misaada na kujiamini
kuleta maendelo yao wenyewe.Hapa kwetu kiongozi mzuri anaonekana ni Yule
anayefahamiana vyema na mataifa ya kimaagharibi,dio maana ni kawaida siku hizi
kwenye kampeni watu kuahidi kuwa wakichaguliwa wataenda kuomba misaada na
kusaidia wanaowaongoza,wamesahahu thamani ya rasilimali zao wenyewe.Rwanda ni
tofauti,ukipiga kampeni za namna hiyo,haupati cheo chochote kile.
Nakumbuka kisa kimoja
kilichotokea mwaka jana 2012 ambapo wanafunzi wapatao 27 kutoka nchi za
magharibi walitembelea Virunga National Park,Rwanda.John Fox ambaye alikuwa
mmoja wa wanafunzi hao alisema kuwa walimpa zawadi ya peni mtoto mmoja
aliyekuwa maeneo ya hifadhi ya virunga.Mtoto alipokea na kukimbia kwa furaha
kupata zawadi hiyo kutoka kwa wazungu.Wakiwa wanarudi kutoka ndani ya hifadhi
hiyo walisimamishwa na askari wa hifadhi na kuambiwa wamefanya kosa kubwa
sana,walipouliza kosa lao Yule askari wa hifadhi akawambia”Haturuhusu kuwapa
watoto zawadi kwa namna hiyo kwani unawajengea mtazamo wa kuwa ombaomba na
tegemezi”.Nadhani tunamuhitaji askari huyo haje kuzungumza na viongozi wa
kitaifa hapa kwetu…!
Ukuaji wa uchumi wa Rwanda na
maendeleo ya huduma za kijamii yanatokana
na imani ya wananchi katika utawala bora na haki kutendeka.Wakati Kenya
walishindwa kuaminiana katika kusikiliza kesi na kuhukumu waliohusika katika
vurugu za baada ya uchaguzi mwaka 2008,Rwanda wameweza hilo.Mahakama za ndani
zilizoimarishwa nchini Rwanda(Gachacha) zipatazo 1,200 kwa nchi nzima,zimeweza
kuhukumu kesi zipatazo milioni 1.2 kwa muda mfupi na kwa haki.Amani katika nchi
ni matunda ya imani ya upatikanaji wa haki katika vyombo vya sheria.Hapa kwetu Tanzania
Ripoti ya Transparency international inaonyesha kuwa Tanzania polisi na
mahakama ndivyo vyombo vinaovyoongoza kwa rushwa nchini.
Ili kuleta maendeleo Tanzania ni
lazima malengo yetu yaelezwe,tusiseme ni kilimo huku ikiwa bado wakulima
asilimia 70 wanatumia jembe la mkono.Tusiseme elimu huku tukitenga asilimia
1.4% ya bajeti wakati Rwanda wakitenga 5.8% na Kenya 7%? Ukienda Rwanda kila
mmoja anafahamu nchi yake inelekea wapi na wajibu wake ni nini.Kila mmoja
anapigana na Rushwa na Kutaka utawala bora.Nchi ambayo kila mtu na lwake haiwezi
kuendelea.
Kweli ulaya ni mbali,basi
tujifunze kwa jirani zetu Rwanda…
Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii
Joel Nanauka
March 2013.
Post a Comment