Social Icons

Loading...

Nazikumbuka shule hizi, leo hii ziko wapi jamani?

NILIHITIMU masomo yangu ya kidato cha nne miaka 19 iliyopita katika Shule ya Sekondari ya Nyakato, iliyopo mkoani Kagera. Nakumbuka mengi katika shule hii iliyopo umbali wa kilometa saba hivi kutoka mjini Bukoba.Kwa wale waliosoma shule za sekondari za Mkoa wa Kagera, ulio pembezoni mwa Ziwa Victoria enzi zetu, waliotutangulia na wale waliofuata miaka mitano hivi baada yetu, ukitaja Nyakato watakumbuka pia shule kama Kahororo, Ihungo, Rugambwa, Bukoba Sekondari na kidogo Bugene.

Ni shule ambazo zilikuwa na sifa za aina yake, zikiwa na baadhi ya mambo, ambayo yalizifanya zifanane, siyo kwa bahati mbaya, la hasha, bali kutokana na mipango iliyokuwa ikipangwa na wakuu wa shule hizo na bodi husika.Shule kama Nyakato nilikosoma mimi, ilikuwa ni taasisi kamili ya elimu. Kulikuwa na utaratibu wa kishule uliojitosheleza kuanzia madarasa, mabweni, viwanja vya michezo, ofisi za walimu, maabara za masomo ya sayansi, ofisi za viongozi wa wanafunzi, maabara, stoo za kutunzia vifaa, vyoo, ukumbi wa chakula (bwalo) na hata mashine ya kusukumia maji.
 Kwa upande wa ratiba ya siku, halikuwa ni jambo la dharura au bahati mbaya, kila kitu kilikuwa wazi. Kwamba siku ya kukimbia mchakamchaka ilifahamika, taratibu za kufanya usafi kwa ujumla wake ulifahamika, muda wa kuingia madarasani ulijulikana, siku za kazi zilikuwa wazi na hata siku za michezo ziliheshimiwa.Nakumbuka mradi wa ukarabati wa shule uliokuwa ukifadhiliwa na Serikali ya Denmark kupitia shirika lake la misaada DANIDA, (Elimu DANIDA – School Maintenance Project). Kupitia mradi huu, shule hizi za Serikali zilifanyiwa ukarabati wa hali ya juu.
 Mabati yalibadilishwa, umeme uliwekwa, mifumo ya maji ilijengwa na mengine kadha wa kadha. Kwa hakika DANIDA ilizirejesha shule zetu katika hadhi yake. Shule zikawa mahali siyo pa adhabu, bali mahali panapokalika kutokana na mazingira yalivyokuwa.Baada ya kumaliza kazi yao ya ukarabati, ambao haujapata kufanywa tena katika shule zetu za Serikali, DANIDA kabla ya kuondoka walianzisha programu ndogo, iliyoitwa Regular Preventive Maintenance (RPM), ambayo lengo lake lilikuwa ni kuwezesha utunzaji wa mazingira na kulinda ukarabati walioufanya.
 Kupitia RPM kulikuwa na mashindano ya kimkoa, kwamba ni shule gani ambayo wanafunzi wake wanaweza kulinda vizuri mazingira yao. Yalikuwapo mashindano ya kikanda, yaliyozihusisha shule zote za mikoa ya Kanda ya Ziwa.Chini ya RPM baadhi yetu tulipata kutembelea Shule za Sekondari za Bwiru Wavulana na Bwiru Wasichana, lengo likiwa ni kujifunza wenzetu walivyokuwa wakimudu kufanya vizuri, licha ya kwamba mazingira yao hayakuwa rafiki kama yetu.
 Nakumbuka Bwiru Wasichana ni shule iliyokuwa ya kupigiwa mfano, kutokana na jinsi mabinti wale walivyokuwa wasafi na jinsi walivyokuwa na uwezo wa kutunza mazingira ya shule yao.Nakumbuka moja ya maajabu tuliyoyaona wakati ule ni uwezo wa wanafunzi wa Bwiru Wasichana kuweka udongo juu ya mawe na kupanda maua juu ya mawe hayo.
 Tulipokuwa tukirejea shuleni kwetu, tulijadiliana kuhusu kile tulichokiona katika ziara zetu na kushauri jinsi tunavyoweza kusonga mbele.RPM siyo mpango uliopendwa na wananfunzi, kwani tunafahamu kwamba tuwapo shuleni wengi wetu hatukupenda kazi, lakini mazingira ya shule na uhalisia wa maisha ulitufanya kuuchukulia mpango ule kuwa sehemu ya maisha yetu ya shule.
 Yako mengi ya kusimulia, lakini niseme kwamba nimeeleza machache tu na kwa haraka kila mmoja anaweza kukumbuka shule alikosoma, iwe ni shule ya Serikali au ya binafsi. Hali ilikuwaje? Maisha ya wanafunzi yalikuwaje, ratiba za vipindi, walimu je? Na mambo mengine kama hayo.Tukizigeukia shule zetu hii leo, tunaona kitu gani? Tukiachana na shule za binafsi, hata hizi za Serikali ambazo zilisaidiwa ukarabati wake, zikoje sasa?
 Wakuu wa Shule kama akina Samuel Lutanjuka aliyekuwa Nyakato na baadaye Ihungo, walimudu usimamizi wa shule kwa viwango hivi miaka 20 iliyopita, leo hii ina maana Serikali haina watu wa aina hii? Kimetokea nini?Shule ziko katika hali mbaya, siyo kimajengo tu bali hata mazingira yake ni hatarishi. Kwa wale tuliosoma safu ya mada ya Jumamosi siku chache zilizopita kuhusu mazingira ya sasa ya Shule ya Moshi Ufundi (Moshi Technical) mtakubaliana na ninachokisema.
 Shule ile ambayo ilipata kuvuma sana katika nchi hii, leo iko taabani. Mkuu wa shule na walimu wake anaotamba kwamba wapo zaidi ya 80 wameshindwa kabisa kuisimamia. Shule iko katika mazingira machafu ya kupindukia. Hapa tatizo siyo fedha, bali ni uzembe au udhaifu wa kupindukia.

Zipo shule nyingi ambazo leo hii tukizitazama tunaweza kulia machozi. Hazina hadhi tena ile ya kwanza, zimetelekezwa na zimekuwa kama watoto yatima.  Tukumbuke Kantalamba, Maswa Wasichana, Shy Bush, Mirambo, Tabora Wavulana na Wasichana, Kilakala, Galanos, Ndanda na nyingine nyingi.
 Serikali iamke na kuchukua hatua sasa, mawaziri wetu wakumbuke walikosoma na wachukue hatua.  Msipofanya hivyo, tutabaki na magofu.
Makala  kwa  hisani  ya   http://www.mwananchi.co.tz/kolamu/Siasa-wiki-hii/-/1614818/1618042/-/tx3b6j/-/index.html
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top