Social Icons

Loading...

Hauhitaji Fedha, Kuzalisha Fedha...!

 Katika maongezi mengi watu wamekuwa wakisema na kujiaminisha kauli kama hizi, “Tumia fedha kupata fedha”, “Siwezi kuanza biashara wakati sina fedha”, “Bila chochote ni vigumu kupata kitu”, “Wenye fedha ndio wanaofanikiwa” na nyingine nyingi zinazofanana na hizo. Kiharaka haraka kauli kama hizo zinaonekana kuwa sahihi na zinazokubalika, lakini zina sumu kubwa sana katika maendeleo ya mtu anayehitaji kuanza ama anaeendelea na juhudi za kujikwamua kiuchumi kwa kuongeza kipato.

 Ninapoendelea ngoja nitoe kisa kimoja kutoka katika Biblia. Historia ya Wana wa Israeli inaonesha kuwa kuna wakati wakiwa utumwani Misri kulitokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Farao aliyekua anawatetea kufariki. 
 
Farao ‘mpya’ alikua ni mkorofi na aliwatesa sana kutokana na kuwapa kazi ya kufyatua matofali ya kujengea mapiramidi yote yanayoonekana pale Misri hadi leo. Enzi hizo za mateso akatokea nabii Musa ambae alitumwa na Mungu kuwaokoa ili awapeleke Kaanani. Harakati za Nabii Musa zilimwongezea chuki Farao dhidi ya Waisrael na akaapa kuongeza mateso. Awali walikua wakifyatua matofali kwa kutumia majani yaliyokua yanaandaliwa na wasimamizi wao(wawakilishi wa Farao).

 Baada ya hasira ya Farao kuwaka akaamuru mambo mawili; mosi, Waisraeli wasiandaliwe tena majani ya kufyatulia matofali; pili, kila Mwisraeli aongezewe maradufu idadi ya matofali aliyokuwa akifyatua awali wakati akipewa majani. 

Huu ulikua wakati mgumu sana kwao hasa ikizingatiwa kuwa tangu wanazaliwa walijua kua “haiwezekani kufyatua matofali bila kutumia majani”. Lakini kutokana na adhabu na mateso ya Farao, Waisraeli walitafuta mbadala na kujikuta wakiendelea na kazi ya kufyatua matofali tena kwa idadi mpya waliyopangiwa. Kilichowasukuma hadi kutafuta mibadala ilikua ni adhabu na mateso waliyokuwa waliyopata kwa kushindwa kutekeleza ufyatuaji wa matofali. Kutoka katika kisa hicho kuna mambo matatu tunapata. 

Mosi, ili mtu upambane kupata kitu inategemea na nguvu iliyopo nyuma yako inayokusukuma utafute kitu hicho. Pili, utegemezi unapoondoka akili huwa inakusanya uwezo usiotumika bado kuhakikisha kuwa unaanza kujitegemea. Tatu; ‘nguvu ya asili’ (Mungu) huwa inafanya kazi na watu wanaopanga, kufikiri na kujishughulisha. 

Nianze na nguvu inayokuwepo nyuma ya mtu kutafuta kitu fulani, ambapo kwa hapa tunaongelea kutafuta fedha. Kuna nguvu mbili zinazoweza kusukuma mtu kutafuta fedha, ya kwanza ni ile ambayo kwa Kiingereza inaitwa, “Push Power” na ya pili ni ile inayoitwa “Pull Power”.

 Katika nguvu ya kwanza unasukumwa kuondoka katika mazingira duni, wakati ile ya pili inakuvuta kuingia katika mazingira bora zaidi hata kama haupo katika hali mbaya sana kimaisha. Iko hivi, unaweza kuzaliwa katika mazingira ya umasikini wa kutupwa na umasikini ukawa unakutesa na kukuumiza kichwa sana. 

Unapojaribu kutoka katika lindi la umasikini unakua ukitumia nguvu ya ‘push power’. Lakini unaweza ukawa umezaliwa kwenye mazingira ya kawaida ama ya kitajiri isipokua ukatamani kufanikiwa na kufikia hatua fulani ya kibiashara ama ya kimaisha. Kitendo cha kuvutwa na mafanikio yaliyopo mbele yako ndio tunakiita ‘pull power’. 

 Kuna utafiti nimewahi kuusoma unaoeleza nadharia ya watu wa kabila la Wakinga na Wachagga walivyofanikiwa katika ujasiriamali. Utafiti huu ulieleza kuwa wakinga wamekua wakifanikiwa kibiashara kwa kutokana na ‘push power’ wakati Wachagga wanafanikiwa kutokana na ‘pull power’. 

 Inapotokea ndani yako ukawa na moja kati ya hizi nguvu kwa kiwango kikubwa na cha kutosha, ni rahisi na tena inawezekana ukapata upenyo wa kuzalisha fedha ama kupata mafanikio pasipo kua na fedha. Cha kufahamu ni kwamba, nguvu hizi hazitokei kwa bahati mbaya isipokua huamuliwa na muhusika mwenyewe. Kadiri unavyouchukia sana umasikini ulionao unajenga nguvu ya kukutoa hapo. Kadiri unavyojenga hamasa ya kupata fedha ama mafanikio makubwa ndivyo nguvu ya kukufikisha huko inavyojengeka ndani yako. Ukijua unapoelekea ni rahisi kutafuta njia ya kukufikisha huko. Nitoe mchapo mwingine unaonihusu mimi mwenyewe. 

Kiujumla tangu zamani nilitokea kuyachukia sana mazingira ya ukawaida wa kiuchumi katika familia niliyozaliwa. Hii ilijenga nguvu kubwa sana ya kunifanya nipambane kujikwamua na hali ile. Wakati fulani huko nyuma nilidhamiria kununua basi dogo kwa ajili ya biashara ya usafirishaji wa abiria. Wakati ninapata wazo hilo, mfukoni mwangu nilikua na shilingi laki nane tu.

 Gari nililotaka kununua lilikua la milioni tisa; sikua na rasilimali nyingine yeyote wala rekodi za kibenki kuniwezesha kupata japo mkopo. Nilichofanya niliorodhesha majina ishirini ya watu ambao nitawafuata na kuwaeleza mpango wangu wa biashara kisha kuwakopa fedha za kuwezesha biashara hii. 

Kila jina moja nilipanga kukopa shilingi milioni mbili. Niliweka majina 20 kwa sababu nilitambua kuwa wengi wao hawatanipa milioni mbili zote, wapo watakaonipa pungufu na wapo ambao hawatanipa kabisa. Ndivyo ilivyotokea kuna walioniazima milioni, wapo walionipa elfu hamsini na kuna walioniambia hawana kitu lakini katika orodha hiyo wapo walionikatisha tamaa wakidai, ninaota ndoto za mchana kuwaza kununua gari tena la biashara! Katika kila niliyekua ninaenda nilimueleza hivi, “….nina milioni saba, nimepungukiwa na milioni mbili. 

Ukiniazima hizo nitazirejesha ndani ya miezi sita/mwaka/mwezi mmoja….”. Wakati nikifanya ukusanyaji huu nilikua nikitembea na mchanganuo wa biashara unaoonesha namna biashara hiyo inavyolipa. Hatimaye nilinunua gari niliyoikusudia na kuanza biashara ya usafirishaji kwa kutumia shilingi laki nane tu! Hauhitaji kuambiwa kilichotokea baada ya hapo, kwa sababu nilikua nimejiongezea thamani. 

Sitaki kueleza katika makala haya changamoto zilizonipata baada ya kukamilisha lengo hili; lakini baada ya hapo mambo yalikua nafuu tofauti na mwanzo. Kwanza nilipata mtandao wa matajiri wa magari (kwa sababu nilikua na gari), pili ikawa ni rahisi kumwambia mtu niazime kiasi fulani cha fedha kwa sababu anajua sio wa kubabaisha na tatu hata taasisi za fedha zinanza kukugombea kwa sababu unakopesheka. 

Mbinu hii niliitumia mimi na ilileta matunda kwangu. Sikupi ‘garantii’ uitumie kama ilivyo kwa sababu inategemea mazingira uliyonayo, kiwango chako cha uthubutu pamoja na ukubwa wa nguvu nilizozitaja (push power na pull power). Lakini kuna mambo nataka uyabaini kutokana na mchapo wangu huu. Yapo mambo ambayo unaweza kuyatumia kama bidhaa ya kubadilisha na fedha. Mambo haya yanajumuisha, mahusiano mema na watu, taarifa sahihi, utu wema, umaarufu, uaminifu unaotambulika na watu, uwezo wako kiakili na mengine yanayofanana na hayo. 

Hata hivyo lazima ijulikane kuwa suala la kupata mafanikio (katika fedha na maeneo mengine) ni suala linalohitaji uwekezaji endelevu wa mwenendo wa maisha ya kawaida. Uhusiano na watu unategemea tabia yako kimaisha (upendo, kuwajali watu, kuwaheshimu n.k), taarifa sahihi zinatokana na kujisomea, kuongea na watu na kujielimisha. Vile vile uaminifu unatokana na uwakili wako katika kazi, elimu na mambo mengine.

 Mambo haya yanaweza kukupatia fedha ikiwa utaamua kuyaunganisha na kusudio lako la kutafuta fedha. Kwenye mchapo wangu nimesema niliorodhesha watu 20 ambao niliwafuata na kuomba wanikopeshe fedha. Kilichonipa ujasiri wa kuwafuata ni jinsi navyoishi nao na ile kujua kuwa wananiamini.

 Jambo la pili nililolitumia ni kuwa na taarifa sahihi kuhusu biashara ya kusafirisha abiria; kwa maana hiyo wazo langu nilikua naliwasilisha kiujasiri na uthubutu mkubwa. Huwezi kuwa unaishi maisha ya ovyo, kama ufujaji wa fedha halafu utegemee watu wakuamini katika fedha na kukupa mtaji. Huwezi kuwa mvivu wa kutafuta taarifa (kujisomea, kubadilishana mawazo, n.k) halafu utegemee kupata ‘deals’ za fedha. 

Vile vile unatakiwa kuwa makini sana na aina ya watu unaohusiana ama kuwasiliana nao. Haiwezekani uwe unafanya mawasiliano ya ‘ovyo’ kwa asilimia mia moja kwa kutumia simu ama mtandao wa kompyuta halafu utegemee kukutana na watu wa maana. (potential people). Vile vile katika kutafuta fedha ni muhimu sana mtu kuachana na visingizio, kwa sababu visingizio ni matokeo ya kukata tamaa hata kama muhusika hujitambui. 

Kila mtu mahali alipo ana fursa fulani ambayo bado hajaitumia inayoweza kumwezesha kuzalisha fedha. Si lazima fedha uione kwa macho, si lazima uishike mkononi, na si lazima uikamate siku hiyo hiyo; lakini unaweza kuibua mazingira ama mawazo yatakayokuwezesha kuzalisha fedha. Kule kwenye kisa cha Wanaisraeli nimetaja jambo la pili ambalo ni akili kutumia uwezo usiotumika bado inapotokea utegemezi umeondolewa. 

Watu wengi wamekua wakiishi kwa utegemezi ndio maana kuna mambo wanakwama ikiwemo kutafuta fedha. Kwa bahati mbaya suala la utegemezi linahusisha fikra, ndio maana kuna mtu anaweza kuwa ameondolewa utegemezi lakini bado akawa hajafunguka kutokana na kutofunguka kifikra na kimawazo. 

Albert Sanga ni mfanyabiashara, mchambuzi & mshauri wa biashara na uchumi. Pia ni mwanasafu wa ANGA ZA UCHUMI & BIASHARA katika gazeti la Jamhuri linalotoka kila Jumanne, nchini Tanzania. Maskani yake ni mjini Iringa.
Kwa  hisani  ya  : Mjengwa  Blog
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top