TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko Kuhusu Yaliyojiri Katika Mkutano wa Hadhara wa CHADEMA Uliofanyika Kata ya Ndago Siku ya Jumamosi Tarehe 14 Julai 2012
1.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliandaa mikutano ya
hadhara katika Jimbo la Iramba Magharibi. Mikutano hiyo ilitolewa
taarifa polisi na jeshi hilo lilitoa baraka zake kama utaratibu wa
sheria unavyotaka kwa barua yake ya tarehe 12 Julai 2012 Kumb. Na.
KIO/B1/1/VOL.V/268
2.
Mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika Kata ya Ndago katika
viwanja vilivyo karibu na kituo cha mabasi ambapo pia ni hatua chache
karibu kabisa na Kituo cha Polisi Ndago. Mkutano huu ulipangwa kuanza
saa nane mchana.
3.
Msafara wa kitaifa unaofanya ziara ya ukaguzi wa chama, katika
mkoa wa Singida chini ya uratibu wa Ofisa wa Sera na Utafiti Makao
Makuu, Mwita Mwikwambe Waitara, (ikiwa ni maandalizi ya operesheni
nyingine kubwa mkoani humo itakayofanyika baadae), uliwasili katika eneo
la Mkutano majira ya saa tisa na nusu alasiri. Tulikuta wananchi wengi
wakiwa wanatusubiri. Kabla ya Mkutano kuanza tulipewa taarifa kwamba
kuna kikundi cha vijana kimeandaliwa kuvuruga mkutano wa CHADEMA kwa
kufanya fujo, ikiwemo kurusha mawe ili mkutano huo usifanyike. Suala
hilo lilielezwa mkutanoni mapema na Mheshimiwa Waitara, mbele ya askari
polisi.
4.
Wakati tukijiandaa kuanza hotuba, vijana wapatao wanane walianza
chokochoko kwa kutoa matusi na punde mawe yakaanza kurushwa kutoka
sehemu mbalimbali. Wakati fujo zinaanzishwa na kile kikundi, Mheshimiwa
Waitara alikuwa bado anazungumza na wananchi kuwaandaa kusikiliza
wazungumzaji wengine. Vurumai hiyo ilizimwa na wananchi wenyewe wa Ndago
waliokuwa na hamu ya kusikiliza ujumbe wa viongozi wa kitaifa wa
CHADEMA.
5.
Kwa kweli tunawashukuru wananchi wengi wa Ndago walioonesha
ujasiri mkubwa kuweza kuwaondoa vijana wale eneo la mkutano, kisha
mkutano ukaendelea, huku wananchi wakionesha kila hamasa ya kufurahia
hoja kutoka kwa wazungumzaji, akiwemo Mheshimiwa John Mnyika, ambaye
aliombwa ahudhurie ziara hiyo kwa nafasi yake ya Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa CHADEMA.
6.
Mpaka tunamaliza mkutano huo ambao wananchi waliufurahia sana kwa
namna ulivyohutubiwa kwa amani na utulivu huku wazungumzaji wakijenga
hoja juu ya mstakabali wa jimbo na taifa lao kwa ujumla, mamia ya
wananchi waliohudhuria walitaka tuendelea kuhutubia, lakini tulibanwa na
ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, eneo la Kinampanda
7.
Lakini kutokana na vurugu hizo zilizokuwa zikisababishwa na
kikundi cha vijana ambao tayari ilishatolewa taarifa yao kwenye mkutano
huo, lakini askari waliokuwepo hawakuthubutu kuchukua hatua,
tulilazimika kuomba msaada kutoka kwa OCD na R.P.C, ambapo baadae wakati
mkutano unakaribia kuisha tuliona gari la polisi kutoka Mjini Singida
likiwa na askari waliojipanga rasmi kwa ajili ya kuzuia vurugu likifika
pale eneo la mkutano, lakini wakati huo hali ilishatulia na hotuba
zimetolewa vizuri.
8.
Kutokana na hali hiyo ya vurugu, zilitolewa taarifa Kituo cha
Polisi cha Ndago, ambapo lilifunguliwa jalada NDG/RB/190/2012. Katika
jalada hilo tulitaja baadhi ya majina ya watu waliokuwa vinara wa kundi
lililokuwa likifanya fujo kwenye mkutano mbele ya askari polisi. Majina
hayo ni; 1. Daniel Sima, 2. Tito Nitwa, 3. Bakili Ayubu, 4. Yohana
Makala Mpande, 5. Ernest Kadege, 6. Abel John, 7. Athuman Ntimbu, 8.
Martin Manase, 9. James Ernest, 10. Simion Makacha, 11. Anton John, 12.
Frank Yesaya
9.
Kwa hakika askari polisi wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya
kutochukua hatua yoyote dhidi ya fujo tulizofanyiwa ikiwemo kupondwa
mawe na kikundi kidogo cha wahuni, fujo zilipozidi askari wote
walikimbia eneo la mkutano, akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana
dhahiri kutotaka kuchukua hatua stahili. Hakuonekana kufanya juhudi
zozote za kuhakikisha amani inalindwa na ulinzi unaimarishwa katika eneo
la mkutano na hatua zinachukuliwa dhidi ya watu walioonekana kudhamiria
kufanya fujo. Mtu yeyote makini angeweza kuona kuwa askari wale
waliokuwepo pale mkutanoni ‘almuradi’ tu lakini kama vile walikuwa na
maelekezo maalum ya kuhakikisha hawachukui hatua yoyote katika kuzuia
mpango wowote wa kusababisha vurugu na kuvunja amani.
10.
Baada ya kumaliza mkutano wa Ndago kwa amani, tulikwenda Kinampanda
ambako tulifanya mkutano mwingine mzuri kwa amani kabisa, ambapo mbali
ya wananchi kuwa wametusubiri kwa hamu kubwa na kutusikiliza kwa makini
hoja zetu, polisi katika eneo hilo walitupatia ushirikiano mzuri tangu
wakati tunafika mpaka tulipomaliza mkutano huo.
11.
Jioni wakati tumerudi hotelini, tukasikia kuna taarifa zinasambazaa
kuwa kuna mtu/watu wamekufa katika eneo la Ndago. Habari hizo zilikuwa
zinakanganya kwa sababu zilikuwa zikitaja idadi tofauti tofauti. Lakini
kwa vyovyote vile kama ni kweli kuna tukio la mtu kufariki, CHADEMA
tunasikitika sana kwa tukio hilo la uhai wa mtu.
12.
Tunalaani taarifa zinazozidi kusambazwa ambazo zinawataja polisi kuwa
wanatuhusisha CHADEMA na tukio la mtu aliyefariki. Hii ni ajabu kubwa
kwamba tumetoka kwenye mkutano ule kwa amani kabisa mpaka tumemaliza
mkutano wa pili kwa amani na polisi wakiwepo sehemu zote mbili, kisha
tunasingiziwa masuala ambayo wenyewe hatukuwa na habari nayo tangu
mkutano wa kwanza ukiwa unaendelea mpaka mkutano wa mwisho
ulipomalizika.
13.
Kutokana na habari hiyo ya kifo cha mtu inavyoenezwa kwa kuihusisha
CHADEMA, tumebaini kuwepo kwa mbinu na mikakati ya chama tawala pia
vyombo vya dola vikihusika kutaka kuwatisha wananchi wa Singida,
Watanzania wote wapenda mabadiliko na viongozi wa CHADEMA katika mkoa
huu, wasifanye kazi ya kisiasa kwa kuwabambikizia tuhuma na kesi na pia
kuwafanya waonekane ni watu wa vurugu.
14.
Tunapenda kusema hapa kuwa njama hizo hazitafanikiwa. Zitashindwa kama
zilivyoshindwa njama zingine zote ambazo zimekuwa zikifanywa na vyombo
vya dola, viongozi wa serikali na chama tawala dhidi ya CHADEMA na
vuguvugu la mabadiliko nchini.
15.
Tunawataarifu wananchi kuwa ratiba ya kufanya Operesheni nyingine kubwa
katika Mkoa wa Singida, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Willibrod Slaa,
itafanyika baadae kama ilivyoazimiwa na kikao cha Kamati Kuu.
Imetolewa leo Singida, Julai 15, 2012 na;
Waitara Mwita Mwikwabe
Afisa wa Sera na Utafiti CHADEMA Makao Makuu
Post a Comment