Social Icons

Loading...

KWELI ULAYA NI MBALI, TUJIFUNZE KWA JIRANI ZETU RWANDA.

“Ili kuleta maendeleo Tanzania ni lazima malengo yetu yaelezwe,tusiseme ni kilimo huku ikiwa bado wakulima asilimia 70 wanatumia jembe la mkono.Tusiseme elimu huku tukitenga asilimia 1.4% ya bajeti wakati Rwanda wakitenga 5.8% na Kenya 7%? Ukienda Rwanda kila mmoja anafahamu nchi yake inelekea wapi na wajibu wake ni nini.Kila mmoja anapigana na Rushwa na Kutaka utawala bora.Nchi ambayo kila mtu na lwake haiwezi kuendelea”.
Imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa nchi za Afrika kuwa na safari nyingi za ulaya na amerika kwenda kujifunza namna ya kuendelea.Wakirudi utasikia wakisema,”huko wameendelea sana”,”wametuacha mbali hatuwezi kuwafikia hivi karibuni”.Hata katika kujifunza kuimudu sekta ya gesi walienda Sweden na Trinidad na Tobago,lakini nchi ya jirani ya msumbiji ambako nao wanatekeleza mradi kama wa hapa kwetu hawakukanyaga kabisa.Nadhani ili tujifunze vizuri ni muhimu tujifunze pia kwa wale tunaofanana nao japo kidogo kihistoria.
Miaka 19 iliyopita tulishuhudia nchi ya Rwanda ikiwa katika mauaji makubwa yaliyotikisa dunia.Ni uadui wa kikabila kati ya walio wengi wahutu na wale walio wachache ila walibahatika kusoma na kushika madaraka katika nchi,Watutsi.
Ndani ya siku mia moja(100) yalishuhudiwa mauaji ya kimbari ya watu wapatao karibu laki nane(800,000) ikimanisha angalau kwa kila siku waliuawa watu wapatao 8000.Nchi ilijaa damu,miundo mbinu iliharibiwa;shule,hospitali,barabara na viwanda.Ilikuwa ni hali ya kukatisha tamaa kwa kila mnyarwanda.
Baada ya vurugu hizi kuisha Rais Paul kagame alichukua nchi kwa mapinduzi akiwa na chama chake cha RFP.Tangu kuingia kwakwe madarakani nchi hii imepiga hatua kubwa sana kiuchumi na katika huduma za kijamii.Wakosoaji wa maendeleo ya Rwanda wanatoa hoja kadhaa kuwa ndiyo sababu ya kuendelea kwao kwa kasi katika kukuza uchumi wao.
 Wapo wengine wanaosema nchi ya Rwanda ni ndogo sana hivyo ni rahisi kuiletea maendeleo,wanasahau hapa kwetu hata katika mikoa midogo bado maendeleo hakuna.Hata hivyo udogo haiwezi kuwa kigezo cha mandeleo kwani ziko nchi ndogo zaidi ya Rwanda kama ilivyo shelisheli yenye km za mraba 455 ukilinganisha na zile za Rwanda kilometa za mraba 26,318 au ukubwa wa Gambia wa kilomita za mraba 11,295 hizi zote ni ndogo kwa eneo kulinganisha na Rwanda lakini bado Rwanda iko juu kimaendeleo ukilinganisha na nchi hizi.
Mfano huku Rwanda ikiwa uchumi wake unakua kwa kasi ya 6.5% kwa mwaka nchi ya Gambia uchumi wake hukua kwa 5.2%. Nchini Rwanda kiwango cha elimu kiko 70.4% huku nchini Gambia ikiwa ni asilimia 40.1%.Na hapa lazima tuzingatie kuwa Rwanda ni zaidi  ya mara mbili ya ukubwa wa Gambia na pia ina idadi ya watu 10,746,300 karibuni mara kumi ya idadi ya watu wa Gambia.Kwa kuzingatia haya,udogo si hoja ya kujitetea kabisa.
Kuna wale ambao wanataka pia kuhalalisha kutoendelea kwa nchi yetu Tanzania wakidai kuwa Rwanda wanapata maendeleo yao kutokana na kupendelewa kupewa misaada lukuki hasa ikitokana na huruma za mataifa mbalimbali kwa kile kilichotokea mwaka 1994.Hii nayo ni mbinu ya wavivu wa kufikiri,kwani kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na kijitabu cha pocket world in figures kinachotolewa na jarida la The economist,ilionyesha kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza kwa kupewa misaada Afrika mashariki,ya tatu Afrika na ya sita duniani.Wakati Rwanda ikiwa imepokea misaada ya dola za kmarekani milioni 785.9 kwa mwaka 2010,Tanzania tulipata msaada wa dola za kimarekani Bilioni 2.9.Kama misaada ingekuwa ndio chanzo cha maendeleo,Tanzania tungetakiwa kuwa mbali zaidi.
Wako watu ukianza kulinganisha maendeleo yetu na yale ya nchi zingine za ulaya au marekani wanakuwa wakali na kusema hatufanani kabisa.Nadhani watu wenye fikra hii watakubaliana na mimi kama nitailinganisha Tanzania yenye uhuru wa miaka 50 na Rwanda iliyoanza kujijenga miaka 19 iliyopita.Nchi ya Rwanda ndio inayoongoza kwa kuwa na usafi katika nchi za Afrika mashariki,hili nalo linahitaji misaada ya nje?
NINI SIRI YA MAFANIKIO YA RWANDA?
Mafanikio ya Rwanda hayatokani na Jambo moja tu,yako mambo mengi yanayochangia katika maendeleo yao ya kasi yanayotamaniwa sana na mataifa mengi,leo nitalizungumzia moja.
Siri ya mafanikio ya Rwanda imejengwa katika UONGOZI MADHUBUTI WENYE MAONO,tangu Rais kagame aingie madarakani amefanikiwa kuonyesha njia kwa vitendo.Hajaacha mipango yake iwe ndani ya makaratasi tu,amehakikisha wananchi wote wanaelewa kwa undani maono ya nchi yao ni nini,na kushikamana katika kuyatekeleza.
Suala la ukabila ambalo ndio kilikuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya mwaka 1994 alikishughulikia bila kificho na alifanya hivyo kwa uwazi.Alikemea ukabila akiwa ndani na akiwa nje pia,hakuna mnyarwanda asiyejua kuwa kagame hakubaliani na sera za ukabila.Ameonyesha kwa vitendo katika uteuzi wake wa viongozi mbalimbali pia.Leo hii ni marufuku kwa mnyarwanda yeyote kusema mimi wa kabila Fulani,kila mmoja anatakiwa ajitambulishe MIMI NI MNYARANDWA.Viongozi wetu hapa Tanzania,ni lazima pia wafikishe wananchi wao hapo katika suala la udini kama mwalimu Nyerere alivyolisimamia ili kujenga nchi ya usawa.
Katika maono yake kwa nchi ya Rwanda ya hadi mwaka 2020,kagame ameelezea jinsi anavyokusudia kuibadilisha Rwanda kutoka katika nchi ya kutegemea kilimo uchwara na misaada na kuwa nchi yenye uchumi ulio thabiti na unaotegemea uwekezaji katika elimu na biashara.Maono haya yanaeleweka kuanzia waziri hadi dereva wa daladala.Kuanzia kiongozi hadi mwananchi wanazungumza lugha moja na kuwa na msimamo mmoja.Hivi hapa kwetu wote tunaelewa tunakoelekea?Hiyo vision 2025 inajulikana kwa kiasi gani na kila mtu.Hata wale waliofika chuo kikuu ukiuliza vision 2025 inaeleza nini asilimia kubwa watakuuliza,hicho ni kitu gani?badala ya kujadili mwelekeo wan chi yetu malumbano sasa yamejikita katika siasa na kuharibiana sifa mbele ya jamii(character assassination).
Rais kagame ametengeneza kijitabu kidogo kinachoeleza kwa undani wajibu wa serikali yake na matarajio yake kutoka kwa wananchi ikiwemo mambo ya msingi(values) ya utaifa wao.Haya yanafundishwa kwa kila mtu katika vikao vya ngazi za chini vya wananchi,ni lazima uyafahamu,uyaishi na uyasimamie.Hii hutengeneza nguvu ya pamoja kuendeleza taifa lolote.Misingi yetu kama Taifa ni ipi?
Maendeleo ya Rwanda yameanzia katika fikra na mitazamo,wananchi wamefundishwa kuchukia misaada na kujiamini kuleta maendelo yao wenyewe.Hapa kwetu kiongozi mzuri anaonekana ni Yule anayefahamiana vyema na mataifa ya kimaagharibi,dio maana ni kawaida siku hizi kwenye kampeni watu kuahidi kuwa wakichaguliwa wataenda kuomba misaada na kusaidia wanaowaongoza,wamesahahu thamani ya rasilimali zao wenyewe.Rwanda ni tofauti,ukipiga kampeni za namna hiyo,haupati cheo chochote kile.
Nakumbuka kisa kimoja kilichotokea mwaka jana 2012 ambapo wanafunzi wapatao 27 kutoka nchi za magharibi walitembelea Virunga National Park,Rwanda.John Fox ambaye alikuwa mmoja wa wanafunzi hao alisema kuwa walimpa zawadi ya peni mtoto mmoja aliyekuwa maeneo ya hifadhi ya virunga.Mtoto alipokea na kukimbia kwa furaha kupata zawadi hiyo kutoka kwa wazungu.Wakiwa wanarudi kutoka ndani ya hifadhi hiyo walisimamishwa na askari wa hifadhi na kuambiwa wamefanya kosa kubwa sana,walipouliza kosa lao Yule askari wa hifadhi akawambia”Haturuhusu kuwapa watoto zawadi kwa namna hiyo kwani unawajengea mtazamo wa kuwa ombaomba na tegemezi”.Nadhani tunamuhitaji askari huyo haje kuzungumza na viongozi wa kitaifa hapa kwetu…!
Ukuaji wa uchumi wa Rwanda na maendeleo ya huduma za kijamii yanatokana  na imani ya wananchi katika utawala bora na haki kutendeka.Wakati Kenya walishindwa kuaminiana katika kusikiliza kesi na kuhukumu waliohusika katika vurugu za baada ya uchaguzi mwaka 2008,Rwanda wameweza hilo.Mahakama za ndani zilizoimarishwa nchini Rwanda(Gachacha) zipatazo 1,200 kwa nchi nzima,zimeweza kuhukumu kesi zipatazo milioni 1.2 kwa muda mfupi na kwa haki.Amani katika nchi ni matunda ya imani ya upatikanaji wa haki katika vyombo vya sheria.Hapa kwetu Tanzania Ripoti ya Transparency international inaonyesha kuwa Tanzania polisi na mahakama ndivyo vyombo vinaovyoongoza kwa rushwa nchini.
Ili kuleta maendeleo Tanzania ni lazima malengo yetu yaelezwe,tusiseme ni kilimo huku ikiwa bado wakulima asilimia 70 wanatumia jembe la mkono.Tusiseme elimu huku tukitenga asilimia 1.4% ya bajeti wakati Rwanda wakitenga 5.8% na Kenya 7%? Ukienda Rwanda kila mmoja anafahamu nchi yake inelekea wapi na wajibu wake ni nini.Kila mmoja anapigana na Rushwa na Kutaka utawala bora.Nchi ambayo kila mtu na lwake haiwezi kuendelea.
Kweli ulaya ni mbali,basi tujifunze kwa jirani zetu Rwanda…
Mwandishi  wa  makala  hii ni  mwanaharakati  wa  masuala  ya  kijamii
Joel Nanauka
March  2013.
 
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright Daniel Blog in Contemporary News
Back To Top