Dr Azaveli Rwaitama |
Soma maelezo ya mwandishi nguli nchini, Ndimara Tegambwage hapa chini
kuhusu kisa hiki cha aina yake cha kufungulia mwaka bilashaka:
Dk. Lwaitama alitoka Dar es Salaam leo asubuhi. Akatua Mwanza. Alikuwa
anakwenda Bukoba. Alipanda ndege ya kampuni ileile iliyomtoa Dar es
Salaam leo hii – PrecisionAir. Hii ya kwenda Bukoba ilikuwa Na. PW 0492.
Alikwenda hadi kwenye kiti chake Na. 2B. Hapa ndipo kuna milango ya
dharura kwa pande zote mbili za ndege – kulia na kushoto.
Ndipo akaja mfanyakazi wa ndege. Akamuuliza iwapo anajua Kiingereza.
Baada ya mzaha wa kawaida katika kuuliza iwapo ni lazima kujua
Kiingereza, ndipo mfanyakazi akamwambia kuwa kama hajui lugha hiyo basi
ahame kiti na kukaa kwingine kwani kuna maelezo rasmi ambayo yanatolewa
kwa "lugha ya anga" – Aviation Language.
Ilikuwa katika kujibizana kwanini lugha ya anga isiwe lugha ambayo
abiria wengi wanaelewa – huku Dk. Lwaitama akisema katika ndege nyingi
alizosafiri kote duniani alikokwenda, lugha za anga huwa zile za
wasafiri wengi wa eneo husika na lugha nyingine za kimataifa; huku
akishauri kuwa maelezo yangekuwa kwa Kiswahili na Kiingereza – ndipo
mhudumu alikimbilia mwenzake ambaye naye hakutaka kumsikiliza Lwaitama
na wote wawili wakakimbilia kwa chumba cha rubani kushitaki kuwa kuna
mtu "anafanya fujo." Tayari Dk. Lwaitama akawa abiria "hatari."
Rubani hakutaka kusikiliza abiria wake anasema nini; hakumuuliza hata
mwenzake waliokaa pamoja juu ya fujo alizoripotiwa; alimwambia hawezi
kusafiri. Akaita polisi ambao pia hawakuuliza lolote juu ya fujo zake
bali walifanya kazi moja ya kumtoa nje mkukuku.
Ni rafiki yake aliyemwita Diallo na mwanaharakati Sungusia ambao
anasema aliwapigia simu wampelekee mawakili ili aweze kuandika maelezo
yake mbele yao. Mawakili walifika na yeye kuadika maelezo. Mizigo yake
imepelekwa Bukoba. Yeye amebaki Mwanza na kompyuta yake ndogo ya
mkononi.
Dk. Lwaitama anasema, "Sina mgogoro na kampuni ya PrescisionAir, bali
wahudumu ambao hawataki hata kupata maoni ya abiria. Kwanza, walipata
bahati ya kuona mtu anahiari maoni moja kwa moja. Pili, kama wanafanya
kazi kwenye ndege watakuwa wamesafiri katika ndege za wengine ambako
niliyokuwa nayasema ni maneno na vitendo vya kawaida. Sasa fujo ni nini
katika hili?
Mwalimu huyo mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, "Hata
polisi ni wa kushangaza. Mtu anakwambia huyu kafanya fujo, wewe huulizi
ni fujo gani. Unambeba tu mzegamzege. Sidhani kama huu nao ni utendaji
bora katika nchi iliyohuru; ambako polisi wanapaswa kuwa na utulivu wa
akili na kufanya kazi kwa kufikiri kuliko kwa kuambiwa tu."
Dk. Lwaitana anaamkia kituo cha polisi uwanja wa ndege kesho asubuhi kuambiwa "uamuzi wa polisi."
Haikufahamika iwapo mhudumu wa ndege mswahili, aliyekuwa anaongea
Kiswahili, hakuwa na tafsiri ya maneno ya Kiingereza ambayo alitaka
kumwambia abiria wake.
Post a Comment