Viongozi mbalimbali wa Chadema wameanza kupiga kampeni za urais mwaka 2015 kupitia Operesheni Pamoja Daima.
Akihutubia
mamia ya wakazi wa Mkoa wa Njombe huku mvua kubwa ikinyesha jana,
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa aliwatahadharisha vigogo
wa Serikali wanaoiba fedha za umma kuwa, atawashtaki na kuwafilisi iwapo
chama hicho kitashinda uchaguzi mwaka 2015.
Alisema chama hicho kikishinda dola, kitaboresha masilahi kwa watumishi waadilifu lakini mafisadi wanaotafuna fedha za Serikali watapata wakati mgumu.
"Tutakuwa wakali kwa walarushwa," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema watendaji walarushwa na wezi watashtakiwa ili mali walizowaibia Watanzania zirejeshwa Serikalini.
"Ninawapa
miezi 15 kabla ya uchaguzi mkuu, vigogo hao kurudisha mali walizoiba
vinginevyo watajuta kwa sababu tutawashtaki tutakapoingia madarakani."
alisema.
Naye Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo alisema chama hicho kitatumia kila aina ya 'silaha' kilichonayo kuhakikisha majimbo yote ya Mkoa Kilimanjaro yananyakuliwa na chama hicho 2015.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Ndesamburo alisema hakuna kikwazo kuyatwaa
majimbo hayo kwa vile CCM, kimeshindwa kuwaletea Watanzania maisha bora
kama waliyojinadi mwaka 2010.
Kwa sasa
Chadema kinashikilia majimbo ya Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo
(2000-2015), Jimbo la Hai na Jimbo la Rombo wakati Chama cha Mapinduzi
(CCM) kikishikilia majimbo matano.
CCM kinashikilia majimbo ya Moshi Vijijini, Siha, Mwanga, Same Mashariki na Magharibi wakati Tanzania Labour Party (TLP), kikishikilia Jimbo la Vunjo kupitia Mbunge wake, Augustine Mrema.
Akizungumza
mjini Singida jana, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu aliwataka
Watanzania kumchagua rais mwadilifu siyo anayehonga hata mapadri fedha
chafu zilizotokana na ufisadi.
Alisema
baadhi ya viongozi (bila kuwataja) hivi sasa wanapita kwenye nyumba za
ibada kutoa rushwa na kudai kwamba zamu yao ya kuwa rais imewadia.
Chanzo: mwananchi
Post a Comment